KWANINI BIBI ZAINAB a.s

KUMBUKUMBU YA MAZAZI YA BIBI ZAINAB BINT ALI BIN ABI TALIB.

Sheikh Said.jpgHawza Imam Swadiq a.s imeungana na waislamu duniani kusherehekea kumbukumbu ya mazazi ya motto wa Imam Ali a.s, mtoto wa binti ya mtume na dada wa vijana wawili wa peponi Hasan na Hussein. Katika hafla hiyo Samahat Sheikh Said Othman alizungumza na kusema kuwa Bibi Zainab a.s hakumbukwi kama mwanamke tu wa kawaida bali anakumbukwa kama mwanamke pekee aliyefanya jitahada za kumlinda kiongozi mteule wa mbingu na imam wa zama zake ambae ndio marejeo ya neema za kimungu, Kiongozi huyo ni yule ambae mola hutawanya neema zake kwa waja wake kupitia yeye.

Sheikh ameeleza na kusema kuwa Mitume wote, manabii na maimamu wanaoteuliwa na sheria za mbingu  ambao ni wawakilishi wa Allah katika mgongo wa ardhi huwa wana kazi na faida  tatu muhimu:

  1. MAREJEO YA KISHERIA: Kiongozi wa kimungu ndio marejeo ya watu katika sheria, yeye ni muwakilishi wa Allah anaezibainisha sheria za Mungu kwa watu, kupitia kiongozi huyu watu hufahamu maamrisho na makatazo.

 

  1. MAREJEO YA KISIASA: Hukumu za Allah zimeteremshwa na kubainishwa katika vitabu ili zifuatwe, Hivyo lazima yaandaliwe mazingira ili ziweze kufuatwa kwa kuwa na siasa zilizo ndani ya misingi ya sheria, kiongozi huyu ndio marejeo ya hukumu za mtu binafsi na zile zinazofungamana au kuhusiana na kundi au jopo la watu. Hukumu hizi haziwezi kufanyika katika mgongo wa ardhi ila kwa kuwepo kwa serikali ya kiislamu, hii ndio sababu iliyompelekea mtume kuunda serikali punde tu alipofika madina kwa malengo ya kutafuta nguvu itakayomuwezesha kusimamisha sheria za Allah.

  1. MAREJEO YA KIMUNGU (TAKWINIYAH): Nguvu, ujumbe , siri na neema za Allah (Fuyudhwat Ilahiyah) haziwezi kushushwa kwa viumbe wote kwa kiwango sawa kwa sababu wanatofautiana uwezo wa ubebaji, hivyo Allah huchagua baadhi ya watu ambao ni viongozi wake na wao hushushiwa kila kitu atakacho Allah na kasha wao huwa ndio wasambazaji wa neema na ujumbe huo wa kimungu kwa wengine. Kiongozi huyu uwepo wake ndio sababu ya Baraka na maisha kuendelea kupitia uwezo wa Allah ndio maana riwayaat zinatwambia kuwa lau kama sio uwepo Hujjah (kiongozi wa kimungu) ingeporomoka ardhi na watu wake.

Bibi Zainab a.s aliishi katika zama ambazo kiongozi mwenye sifa hizi hakuishi kwa Amani mbele ya mikono na nguvu za madhalimu wa zama zake, yeye alisimama kidete katika ardhi ya Karbalaa kumnusuru kaka yake na kumlinda kwa gharama yeyote kiongozi wa zama zake baada ya Imam Hussein ambae ni Imam Ali bin Hussein Sajjad. Kwa kitendo hicho Zainab Alkubra akawa amefanikiwa kufanya kazi kubwa ambayo lau kama isingefikiwa dunia ingelikosa kiongozi wa kimungu na ardhi watu wake wangeporomoka kutokana na kukosekana mambo matatu yaliyoainishwa hapo juu.

asadiqmedia bibi zainabMwisho Samahat Sheikh alieleza kuwa inatupasa kumkumbuka Bibi Zainab kwa kuenzi ile kazi ya kuhusiha utawala wa kimungu na serikali adilifu zinazoanzia katika Nafsi zetu kwa kubadilisha aina ya maisha na kutawalisha Allah ndani yake.

Tunamuomba Allah atuwafiqishe tuwe ni wenye kutenda kheri.

Asadiqmedia, Hawza Imam Swadiq a.s

Tufuatilie kupitia:

Facebook: fb.com/asadiqmedia | Youtube: http://www.youtube.com/asadiqmedia

Insta:instagram.com/asadiqmedia

 

BWANA YESU KRISTO  (Nabii Issa a.s )NI MUENDELEZO WA FIKRA YA UKOMBOZI

12

Sheikh Hussein Kabwe,

Siku ya kuzaliwa kwa Bwana  Yesu ni katika siku ambazo Kur’an inataka zikumbukwe, kama inavyoelezwa katika Surat Ibrahim :

Kwa hakika tulimtuma Musa pamoja na miujiza yetu, kuwa watoe watu wako gizani kuwapeleka kwenye nuru. Na uwakumbushe siku za Mwenyezi Mungu….”

Majukumu hayohayo ya kuwatoa binadamu kwenye giza la ukoloni na kuwapeleka kwenye nuru ya uhuru, ndiyo ambayo Bwana Yesu (Nabii Issa) alikuja kuyaendeleza.

HISTORIA YA KUZALIWA KWA BWANA YESU KWA KADIRI YA KURAN TUKUFU.

Historia ya kuzaliwa kwa Bwana Yesu katika Kur’an, inaanzia kwa Bibi Yake, pale alipopata shauku ya kuwa na mtoto wa  kiume,na akaweka nadhiri ya kumtoa mtoto huyo wakfu, katika nyumba ya ibada, Kur’an tukufu inasimulia kisa hicho kama ifuatavyo :

Aliposema mke wa Imran: Mola wangu ! Nimeweka nadhiri kwako aliyemo tumboni mwangu kuwa wakfu.basi nikubalie kwa hakika wewe ni msikivu na mjuzi. :

 Katika aya hiyo  mke wa Imran ambaye ni bibi mzaa mama wa Bwana Yesu aliweka nadhiri ya kuwa : Nikizaa mtoto wa kiume nitamtoa  katika njia ya Mwenyezi Mungu,ili awe mtumishi katika nyumba ya ibada,lakini mambo hayakuwa kama alivyotarajia kwani mtoto aliyezaliwa alikuwa ni wa jinsia tofauti na ile aliyokuwa akiitarajia , soma aya ifuatayo :  Alipomzaa alisema : Mola wangu! Nimemzaa mwanamke (na Mwenyezi Mungu anajua sana kuwa aliye zaliwa ni mwanamke) na mwanamume si kama mwanamke,na mimempa jina la Mariam,na mimi namkinga kwako yeye na kizazi chake (uwalinde) na shetani aliye laniwa.

Mama huyo aliposema : Na mwanamume si kama mwanamke, kauli hiyo haioneshi kutoridhika na jinsia ya kike wala haimaanishi kuwa mtoto wa kiume ni bora kuliko wa kike,  bali lengo lake lilikuwa ni kupata mtoto wa kiume atakaye kuwa mtumishi katika nyumba ya ibada, kwani hali ya maumbile ya mtoto wa kiume inamruhusu kufanya kazi wakati wowote, lakini hali ya maumbile ya mtoto wa kike, haimruhusu kuingia katika nyumba ya ibada kila siku, kutokana na dharura za kimaumbile kwa mwanamke.Pia hata kazi anazozifanya mtoto wa kiume ni tofauti na zile zifanywazo na mtoto wa kike, ni kwa hoja hiyo tu, mama huyo (mke wa Imran)  alistahabu kupata mtoto wa kiume. Mke wa Imran hakupata mtoto wa kiume na badala yake alimzaa Bibi Mariam, ambaye ndiye Mama wa Bwana Yesu.

MARIAM MTAKATIFU

Bibi Mariam alikulia katika mazingira mema, chini ya himaya ya Nabii Zakaria  na uangalizi wa Mwenyezi Mungu, Bibi Mariamu alikuwa na akili kamilifu iliyomuwezesha kujua kwamba hatima ya madhambi ni kuingia katika Jehanam, na kwa misingi hiyo aliweza kujitenga mbali, na kila aina ya dhambi, hadi akakaribia daraja ya unabii. Kur’an Tukufu inasema : Na Malaika waliposema : Ewe Mariam ! Hakika Mwenyezi Mungu amekuteua na akakutakasa na akakuteua juu ya wanawake wa ulimwenguni.

KUZALIWA KWA BWANA YESU

Kur’an Tukufu inasimulia kisa cha kuzaliwa kwa Bwana Yesu, kwa mtiririko wake wa kipekee tofauti na ule uliyopo katika kitabu cha Mathayo Mtakatifu, Kur’an ina kitabu kamili kiitwacho kitabu cha Mariam, (Waislamu wanakiita Surat Mariam)  kitabu hicho ni cha kumi na tisa katika vitabu vya Kura’n.

Mwenyezi Mungu anasema : Na mtaje Mariam katika kitabu, alipojitenga na watu wake mahali upande wa mashariki.

Na akaweka pazia kujikinga nao. Tukampelekea roho Wetu, akajifananisha kwake sawa na mtu.

Akasema (Bibi Mariam) : Hakika mimi najilinda kwa Mwingi wa rehema aniepushe nawe, ukiwa ni mwenye kumuogopa.

Akasema (yelu roho) :  Mimi ni mjumbe wa Mola Wako (nimekujia) ili nikupe mwana mtakatifu.

Akasema : Nitakuwaje na mwana hali hajanigusa mtu yeyote kwa njia ya kisheria wala isiyokuwa ya kisheria.

Akasema :  Ndivyo hivyo, Mola Wako amesema, haya Kwangu ni mepesi! Na ili tumfanye kuwa ni ishara kwa watu na rehema itokayo kwetu. Na hilo ni jambo lililokwishapitishwa.

Basi akachukua mimba yake akaondoka nayo sehemu (iliyo) mbali.

MJADALA KUHUSU MUDA WA UJAUZITO

Kuna mjadala mkubwa kati ya wanachuoni kuhusu muda wa ujauzito, baadhi wanasema ujauzito huo ulidumu kwa miezi tisa, na wengine wanasema ni miezi sita, ,na wengine wanasema ni siku nzima, na kuna wanaosema ni masaa machache tu na wala si siku nzima. Na rai hii ya mwisho haiko mbali na usahihi, kwani katika aya zilizotangulia tumesoma kuwa : “  Na mtaje Mariam katika kitabu, alipojitenga na watu wake mahali upande wa mashariki”

Ibara hiyo na ile isemayo : Basi akachukua mimba yake akaondoka nayo sehemu (iliyo) mbali. Ni ushahidi tosha kuwa Bibi Mariam alitoka kwa muda mfupi tena bila kumtaafu yeyote, na kurejea nyumbani haraka kabla ya watu kuanza kumtafuta, sasa kama angekaa huko miezi tisa au miezi sita basi familia ingeanza kumtafuta kila sehemu, lakini historia haioneshi kuwa Bibi Mariam aliwahi kutafutwa na familia yake.

WAKATI MGUMU

Katika aya ya 22 tumesoma kuwa, Bibi Mariam alichukua ujauzito na kuondoka nao mbali. Lakini aya ya 23 inaainisha kuwa safari iliishia kwenye shina la mtende pale alipopatwa na udhaifu wa kibinadamu, na wala si udhaifu wa kike kwa maana Mwenyezi Mungu anasema kuwa mwanadamu ameumbwa dhaifu na wala kusema kuwa mwanamke ameumbwa dhaifu. Mwenyezi Mungu anasema : Uchungu (udhaifu wa kibinadamu)  ukampeleka kwenye shina la mtende ; akasema: Laiti ningelikufa kabla ya haya ni kawa ni mwenye kusahaulika kabisa.

Basi hapo ikasikika sauti  kutoka chini yake kama isemavyo Kur’an Tukufu : Pakanadiwa kutoka chini yake kwamba usihuzunike; hakika Mola Wako ameweka chini yako kijito cha maji.

Na litikise shina la mtende utakuangushia tende mbivu.

Basi Kula na kunywa na ujiburudishe. Na pindi ukimuona mtu yeyote  basi sema hakika mimi nimeweka nadhiri kwa Mwingi wa rehema ya kufunga. Kwa hiyo leo sitasema na mtu. Basi baada ya kuzaliwa mtoto, Bibi Mariam alirejea nyumbani akiwa kabeba mtoto, hali ambayo ilimshangaza kila mtu, na kuzua mgogoro mkubwa kati yake na watu wake.

MJADALA BAINA YA BIBI MARIAM NA  WATU WAKE

Kutokana na utakatifu aliyokuwa nao Bibi Mariam basi isingeweza kuingia akilini kwa yeyote kuwa Bibi Mariam anaweza kuwa na mtoto kwa njia isiyokuwa ya kisheria, kwa maana alikuwa hajaolewa. Mwenyezi Mungu anasema : Akaenda naye kwa jamaa zake hali ya kuwa amembeba. Wakasema: Ewe Mariam! Hakika umeleta kitu cha ajabu.

Kuzaliwa mtoto asiye na baba mwenye kutambulika kisheria hilo lilikuwa ni jambo ambalo halijawahi kutokea katika historia ya familia ya Mzee Imran. Basi kwa kuwa Bibi Mairiam alikuwa kaishapata amri ya kutosema na yeyote, basi ilimbidi aashirie kwa mkononi, kuwa wamuulize mtoto mwenyewe, nao wakaona kama vile Bibi Mariam anawadhihaki, wakasema : Ewe dada wa Harun! Baba yako hakuwa mtu muovu wala mama yako hakuwa kahaba.

Ndipo akaashiria kwake. Wakasema: Tutamsemezaje aliye bado mdogo susuni ?  Basi pale pale Bwana Yesu alianza kuongea na kutajitambulisha kwa jina la Mja Wa Mwenyezi Mungu, Kur’an Tukufu inasema : Akasema mimi ni mja wa Mwenyezi Mungu amenipa kitabu na amenifanya (kuwa) ni nabii.

Na amenifanya ni mwenye kubarikiwa popote pale ni wapo. Na ameniusia sala na zaka muda wa kuwa niko hai.

Na (ameniusia) kumtendea mema mama yangu. Wala hakunifanya niwe jeuri muovu.

Na amani iwe juu yangu, siku niliyozaliwa na siku nitakayokufa na siku nitakayofufuliwa.

Kisha Kur’an ikamalizia hadithi kwa kusema : Huyo ndiye Yesu mwana wa Mariam, neno la kweli ambalo wanalifanyia shaka.

Haiwi kwa Mwenyezi Mungu kuwa na mwana, Yeye ametakasika! Anapolipitisha jambo basi huliambia tu: kuwa! Likawa .

Na hakika Mwnyezi Mungu ni Mola Wangu na Mola Wenu basi mwabuduni. Hii ndio njia Ailiyonyooka.

Lakini makundi yakahitilafiana baina yao. Basi ole wao waliokufuru kuhudhuria siku iliyo kuu.

Ndugu wapendwa, Manabii wote walikuwa na lengo moja nalo ni kufundisha maadili mema katika jamii, maadili yatakayo wabainishia watu njia itakayowafikisha kwenye kilele cha ukamilifu, sasa kama wewe unamfuata Mtume Muhamad s.a.w.w, basi tambua kuwa maadili ya Bwana Mtume s.a.w.w, ndiyo yale yale ya Bwana Yesu, sasa unapovunja makanisa ya Wakristo bila sababu hapo unakuwa unakwenda kinyume na mafundisho kwani mafundisho ya Uislam wa Mtume Muhamad, ni Muislamu na Mkristo kukaa meza moja, kwa amani, kama ndugu wa tumbo moja,huo ndiyo Uislamu wa Mtume Muhamad s.a.w.w, na hata kipindi Waislamu walipokuwa katika wakati mgumu, wakipata mateso mbali mbali toka kwa wakuu wa tawala zilizokuwa madarakani, Bwana Mtume s.a.w.w, aliwaambia wafuasi wake wakimbilie Ethiopia, huko Ethiopia walipokolewa na kupewa hifadhi lakini Mfalme Wa Ethiopia aliyewapa hifadhi Waislamu, yeye mwenyewe hakuwa Muislamu bali alikuwa ni Mkristo, lakini aliwapa Waislamu, chakula, mavazi na malanzi. Sasa wewe Muislamu mfuasi wa makundi ya ugaidi, unapokataa kula chakula cha jirani yako siku ya Chrismass kwa madai ya kuwa wewe ni Muislamu safi, hivi wewe unaujua sana Uislamu zaidi ya Mtume Muhamad s.a.w.w ? Mbona Yeye aliishi na watu wa dini tofauti kwa kuheshimu misingi ya ubinadamu? Bali hata pale Mtume s.a.w.w, alipokuwa na Dola Ya Kiislamu hakuna aliyefanyiwa uhaini na ugaidi kama huu tunaoushuhudia leo hii. Ndugu zangu Wakristo kiongozi aliyeshika madaraka baada ya Mtume Muhamad s.a.w.w, ni Imamu Ali, Imamu huyu anasema : “Watu wako  aina mbili, ima ni ndugu yako katika dini, au ni mwenzio katika ubinadmu” Kauli hiyo inatufundisha namna ya kuishi na watu, yani yule ambaye mmechangi imani basi ishi naye kwa wema kama ilivyoamrishwa katika imani yenu, na yule ambaye mmetofautiana kiimani, basi ishi naye kwa wema kwa kuzingatia misingi ya haki za kibinadamu. Kwa hiyo Waislamu na Wakristo wanaunganishwa na kitu kiitwacho ubinadamu. Na katika ubinadamu ni wewe kushirikiana na binadamu wenzio katika shida na raha, wanapokuwa na furaha basi nenda ukawapongeze tafuta japo zawadi ndogo uwapelekee na wao wakikuletea chakula ambacho kinaruhusiwa kwa mujibu wa itikadi yako basi  pokea, na wanapokuwa na simanzi nenda ukawafariji, huo ndiyo ubinadamu.

Aliyekuwa Kiongozi wa  wa kiroho wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imamu Khomein Mungu amrehemu. Wakati alipokuwa Ufaransa, siku ya Chrismass aliuliza kuhusu mila na deturi za Wafaransa katika kusherekea Siku hiyo,akaambiwa kuwa Wafaransa wanapenda sana maua, basi Imamu Khomein alinunua vishada vya maua na akawapelekea majirani, ili kuwapongeza kwa Sikukuu hiyo.

MAAFIKIANO KATI YA WAISLAMU NA WAKRISTO

Wakristo na Waislamu wote kwa pamoja wanaafikiana kuwa Bwana Yesu alizaliwa, na kwamba kuzaliwa kwake ni muujiza katika miujiza ya Kiungu, lakini tofauti uliyopo kati yao ni kuhusiana na tarehe ya tukio hilo je, ni tarehe 25 mwezi wa kumi na mbili, au ni tarehe 10 mwezi wa nne ? Sasa tofauti ya tarehe isiwe sababu ya kuwagombanisha watu wenye akili timamu, bali ni swala la kukaa mezani kwa heshima na adabu, ili kufanya mazungumzo na kufika muafaka. Na hata kama tarehe ya kuzaliwa kwa Bwana Yesu haitafahamika hiyo haiwezi kuwa ni sababu ya kutolikumbuka tukio hilo la kihistoria, tukio litabaki pale pale na litakumbukwa hata kama siku itakuwa ni tofauti na siku ya tukio lenyewe, kwani mbona Kur’an Tukufu imelikumbuka tukio hilo na haikutaja tarehe ? Mbona Kitabu Cha Mathayo Mtakatifu kimelikumbuka tukio hilo pia, lakini tarehe haikutajwa ? Hii inaashiria kuwa cha msingi ni kukumbuka tukio lenyewe hususan ule ukombozi ulioletwa na Nabii huyo hata kama hatujui ilikuwa ni siku gani, bali ni swala la sisi kuchagua siku ya kufanya maadhimisho hayo. Na ndio maana utakuta katika jamii za Waislamu wakifanya maulidi mara kwa mara hata kama ni nje ya mwezi na tarehe ya tukio.

Kabwe Hussein

Sheikh wa Wilaya ya Mkalama T.I.C

0629 18 05 39 / 0743 96 50 13

Maoni yangu kuhusu sahaba- Sheikh Ayub

Na Samahat Sheikh Ayub Rashid, Muslim Community of England

“Mimi naamini kuwa kuna baadhi ya sahaba ambao, walisimama katika mwendo wa sawa na wengine walikengeuka baada ya Bwana Mtume (s.a.w.w. kufariki dunia). Baadhi yao walizua mambo kinyume cha dini yake; ndiyo sababu wasiruhusiwe kumfikia hata baada ya yeye mwenyewe kukumbusha kwamba hao walikuwa sahaba zake!”

Je sahaba ni nani?

Kwa mujibu wa taarifa ya Imam Ibn Hajar al-Asqalani, iliyomo uk. 10 wa Juzuu ya Kwanza ya kitabu chake kiitwacho al-lsaba, ‘sahaba ni yule aliyemkuta Mtume (s.a.w.w), sahaba ni yule aliyemuona Mtume akawa amemwamini, na akafa katika Uislamu.

 Sheikh ayubu.jpgHivyo, kwa waliomkuta (Mtume s.a.w.w.), aingia yule aliyekaa naye muda mrefu au mfupi; (aingia) na yule aliyepokea kwake au hakupokea; (aingia) na yule aliyepigana jihadi pamoja naye au hakupigana; na yule aliyemwona kwa macho japo iwe hakukaa naye, na (hata) yule ambaye hakumwona kwa kizuizi kama (cha) upofu.

Ibn Hajar katika uk. 5 wa Juzuu ya Saba ya Fathul Bari, amesema kwamba imepokewa kwa Ali b. al-Madini kuwa amesema: ‘Yeyote aliyefuatana na Mtume (s.a.w.w) au aliyemwona japo ni kwa saa moja mchana, ni miongoni mwa sahaba wa Mtume s.a.w.w.’

Na Imam Nawawi naye, katika uk. 14 wa Juzuu ya Kwanza ya Tahdhibul Asmaa Wal Lugh-ghaat, amesema: ‘Kuhusu sahaba kuna madhehebu mbili: lililo muhimu kati yao nayo ni madhehebu ya Bukhari na wanazuoni wengine wote wa Hadith, na jamaa katika wanazuoni wa fiqhi na wasiokuwa wao — ni kwamba kila Mwislamu aliyemwona Mtume s.a.w.w. japo ni kwa saa moja, na hata kama hakukaa naye na kuingiliana naye, (ni sahaba).’

Tunaposoma uk. 4 wa Juzuu ya Saba ya Fathul Bari na uk. 12 wa Juzuu ya Kwanza ya al-lsaba, tunamwona Imam Ibn Hajar al-Asqalani akisema: ‘…Lau mtu aliritadi, halafu akarejea katika Uislamu, lakini akawa hakumwona (Mtume s.a.w.w.) mara ya pili baada ya kurejea kwake (Uislamuni); lililo sahihi ni kwamba (mtu) huyo huhesabiwa ni sahaba kwa vile ambavyo wanazuoni wa Hadith wamemuhesabu hivyo Ash’ath b. Qays na mfano wake.

KISUNNI sahaba ni;

(i) yeyote yule aliyemwona Bwana Mtume s.a.w.w. na akafa hali yu Mwislamu;

(ii) wala si lazima awe amekaa naye sana, bali hata kama amemwona kwa saa moja tu inatosha;

(iii) na wala si lazima awe ni mtu mzima, bali hata kama alimwona utotoni au uchangani, na hata kama alikuwa bado yu utotoni au uchangani wakati Bwana Mtume s.a.w.w. alipofariki dunia; na

(iv) hata kama mtu huyo aliritadi, kisha akarejea Uislamuni, lakini asiwahi kumwona tena Bwana Mtume s.a.w.w. baada ya kurejea kwake huko!

Je sahaba wote ni waadilifu? Na je sahaba hawafanyi makossa? Na je haifai sisi kuzungumza yalewaliyoyafanya?

Imani yangu ni kuwa baadhi tu ya sahaba ndio waadilifu, na baadhi nyingine si waadilifu. Naamini kuwa wako masahaba wengi waliokuwa watu wazuri sana, na naamini pia wako baadhi yao waliokengeuka na kumuasi Mola wao kama binadamu wa kawaida. Kwa mfanoo;

(i) Qudaama b. Madh’un: Huyu ni miongoni mwa Waislamu wa mwanzo mwanzo. Alihama hijra mbili, akawahi hata kupigana katika Vita vya Badr. Lakini pamoja na yote hayo aliwahi kushikwa amelewa, zama za Ukhalifa wa Umar b. al-Khattab, akapigwa haddi! Jee, sahaba huyu bado ni mwadilifu? (Taz. al-lsaba, Juzuu ya Tatu, uk. 219-221; na al-lsti’ab, iliyo chini ya al-lsaba, Juzuu ya Tatu, uk. 247-251)

(ii) Abdulrahman (al-Awswat) b. Umar b. al-Khattab: Huyu, kama jina lake lionyeshavyo, alikuwa ni mtoto wa Khalifa wa Pili, na alikuwa ni sahaba vile vile. Yeye naye alikamatwa amelewa, na babake akampiga haddi! Hata inasemekana kwamba alikufa kwa kipigo hicho. (Taz. uk. 405-406 wa Juzuu ya Pili ya al-lsaba; na uk. 395-396 wa Juzuu ya Pili ya al-lsti’ab, iliyo chini ya al-Isaba) Jee, na huyo naye atakuwa ni mwadilifu?

(iii) Abu Mihjan: Huyu ni sahaba mwingine aliyekuwa akinywa pombe sana na kuzini; hata imeeelezwa kwamba Khalifa Umar b, al-Khattab aliwahi kumpiga viboko mara saba au nane kwa hilo! Akawahi hata kumfunga! (Taz. al-lsaba, Juzuu ya Nne, uk. 173-175; na uk. 181-187 wa Juzuu ya Nne ya al-lsti’ab iliyo chini ya hiyo al-lsaba.) Jee, sahaba kama huyo vipi huendelea kuwa mwadilifu?

(iv) Nu’aiman b. Amr. Huyu ni sahaba ambaye amepigana jihadi vita vyote. Lakini pamoja na hivyo, alikuwa mlevi! Mara nne Mtume Muhammad’ s.a.w.w. alimkamata sahaba huyo amelewa! Kati ya hizo, mara tatu alimpiga haddi! Mara ya nne, ndipo Umar b. al-Khattab alipotaka akatwe kichwa chake, lakini Bwana Mtume s.a.w.w. hakumkubalia. (Taz. chini ya jina la Marwan b. Qais al-Aslami katika uk. 384 wa Juzuu ya Tatu ya al-lsaba; na pia juzuu hiyo hiyo, uk. 540-541, chini ya jina la huyo Nu’aiman. Vile vile taz. Usudul Ghaba, Juzuu ya Nne, uk. 199 – 200, na Juzuu ya Tano, uk. 36 – 37.)

(v) Samura b. Jundub: Huyu ni mmoja ya wale watu watatu walio ambiwa na Bwana Mtume s.a.w.w. kwamba, wa mwisho wao kufa, ataingia Motoni. Yeye alikiuza pombel (Taz. chini ya Hadith Na. 61 katika uk. 82-84 wa Mujallada wa Kwanza wa Silsilatul Ahadithidh Dhaifa Wal Mawdhu’a ya Muhammad Nasiruddin al-Albani.)

(vi) al-Walid b. Uqba: Huyu ndiye yule ambaye Mwenyezi Mungu amemwita fasiq katika Sura 32:18 na Sura 49:6. Isitoshe; na ndiye yeye, pale alipokuwa Gavana wa mji wa Kufa zama za Ukhalifa wa Uthman bin Affan, aliyeswalisha watu swala ya asubudhi rakaa nne, na huku amelewa! Kisha akatapika kibulani, akatoa salamu na kuwauliza walioswali naye: Jee, niwaongezee? Kwa hivyo akapigwa haddi na kuondolewa kwenye Ugavana!

Ibn Abdilbar amesema amesema kwamba hakuna hitilafu baina ya wanazuoni kuwa aya hiyo iliteremshwa kwa ajili yake sahaba al-Walid bin Uqba, kama ilivyo tajwa katika uk. 601 wa Juzuu ya Tatu ya al-lsaba.

Je Mtume kasemaje kuhusu Masahaba?

Turejee Sahih Bukhari na Sahih Muslim:

(i) Imepokewa kwa Anas kwamba Mtume s.a.w.w. amesema: Watu miongoni mwa sahaba zangu watanijia kwenye Hodhi[7]. Nitakapowaona, na watakapokuwa waletwa kwangu, watazuiwa ili wasinifikie. Hapo nitasema: Sahaba zangu, sahaba zangu! Nami nitaambiwa: Wewe hujui walizua nini baada yako.

Hadith hiyo utaiona katika Sahih Muslim, ‘Kitabul Fadhaail’, Mlango wa ‘Hawdhu Nabiyyina (s.a.w.w) Waswifaatuhu.’ Kwa Kiingereza ni Hadith Na. 5706 kwenye ukurasa 1239 wa Juzuu ya Nne.

Hali kadhalika, Hadith yenye maneno karibu kama hayo yaweza kuonekana katika Sahih Bukhari, ‘Kitaabur Riqaaq’, Mlango wa ‘al-Hawdh’. Na kwa Kiingereza, ni hadith namba Na. 584 kwenye uk. 381 wa Juzuu ya Nane.

Hitimisho

Mimi naamini kuwa kuna baadhi ya sahaba ambao, walisimama katika mwendo wa sawa na wengine walikengeuka baada ya Bwana Mtume (s.a.w.w. kufariki dunia). Baadhi yao walizua mambo kinyume cha dini yake; ndiyo sababu wasiruhusiwe kumfikia hata baada ya yeye mwenyewe kukumbusha kwamba hao walikuwa sahaba zake!

Ma hiyo ni nature ya binaadamu wote. Wengine husimama mstari wa sawa na wengine hupotoka. Kwani wao hawakuwa Malaika!

 Je tuyazungumze ya masahaba au tusiyazungumze? Sisemi tuwatukane!

Kwangu ni muhimu sana kuyasimulia yaliyofanywa na masahaba bila ya kupendelea na kutia chumvi!

Kwa mfano, inajulikana kwamba miongoni mwa sahaba wako waliomsingizia bibi Aisha, mke wa Bwana Mtume (s.a.w.w) mambo machafu!

Wako waliotoka msikitini, wakamwacha Mtume (s.a.w.w) anahutubu juu ya mimbari siku ya Ijumaa, na wao wakakimbilia biashara

Mwisho

Mwenyezi Mungu anasema;

تِلْكَ أُمَّةٌ قَدْ خَلَتْ ۖ لَهَا مَا كَسَبَتْ وَلَكُمْ مَا كَسَبْتُمْ ۖ وَلَا تُسْأَلُونَ عَمَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ

‘Hao ni watu walio kwisha pita. Watapata waliyo yachuma, nanyi mtapata mtakayo yachuma; wala hamtaulizwa nyinyi waliyo kuwa wakiyafanya wao’

Sura al Baqara aya 134

Naamini kuwa wengi wa masahaba walikuwa ni watu wema sana na Mola amewaridhia na atawalipa mema kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kuuhami Usilamu na kumfuata Mtume Muhammad (s.a.w.w) na wakajitolea mali zao na maisha yao.

Msimamo wangu ni wa kati na kati, na maana yake ni kuwa, si vibaya nionavyo kuyazungumza mambo yaliyopita kwa na kati ya masahaba. Naamini pia kuwa ni vibaya kuwatukana na kuwalaani bila ya kosa lolote ambalo hawakulifanya. Naamini pia ni vizuri kuzungumza yaliyopita kati yao kwa ajili ya kupata ibra na mazingatio katika maisha yao. Siamini kuwa kukaa kimya ndio tiba. Kama kuna sahaba alifanya jambo jema ni vizuri kulisimulia, na kama kuna aliyefanya baya pia ni vizuri kulijua. Kama kuna aliyeritadi ni vizuri kujua huyo alikuwa nani na kwa nini? Mwendo huu utatusaidia kurekebisha mambo katika masiha yetu, kwani mara nyingine isi hujifunza kutokana na makossa ya watu wengine. Kama inavyosemwa ‘we learn through mistakes!

Mola awalipe mema maswahaba wema na akipenda kuwasamehe waliomkosea basi Yeye Allah ni Rauufun Rahiim.

Si kazi yangu mimi kumuingiza yeyote kati yao peopni au motoni!.

Sheikh Ayub Rashid, Muslim Community Uk.

 

elbinawi

To interact with humanity & share ideas...

felicity114

felicity is the purpose of everybody

Ladakh Express

Ladakh's 1st political and cultural online journal.

Islamic Library

Shia Islamic PDFs - Now in Collaboration with ShiaTranslate.org!

zahraa Foundation

Fatima bint Muhammad is the Symbolization of Women's Power in Islam

mmubaraka1

A fine WordPress.com site

The Pilgrim Log

Helping you live your daily pilgrimage

World Shia Forum

Identity, Equality, Unity

Source of Inspiration

All is One, co-creating with the Creator

Bill Langill's Blog

Love is the Answer

Interrupting the Silence

An Episcopal Priest's Sermons, Prayers, and Reflections on Life, Becoming Human, and Discovering Our Divinity

Morgan L. Busse

In Darkness there is Light

YOGA

When unconscious became conscious this is Samadhi

Zoroastrians.net

Parsis, Iranis, Zarathushtis, All Under One Roof

Islamic Laws

Raising Awareness on Fiqh and the Ulema

Tech Cloud

Imagine | Innovate | Implement

Mujtaba Somji

Islamic sayings

%d bloggers like this: