MTAZAMO WA KIONGOZI MUADHAMU KUHUSU MWEZI MTUKUFU WA RAMADHANI

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

Kwa hakika kuanza mwezi mtukufu wa Ramadhani ni idi kubwa kwa Waislamu na ni mahala pake waumini wapongezane na kupeana mkono wa baraka kwa kuingia mwezi huo, na wahamasishane na kushajiishana kujipinda kwa ibada katika mwezi huo mtukufu. Kwa vile mwezi huo ni wa kuwa wageni wa Mwenyezi Mungu, watu pekee wanaoweza kualikwa na kwenda katika ugeni huo ni waumini na wale tu wenye ustahiki wa kwenda katika kitanga cha ugeni wa Mola Mkarimu na Mtukufu. Dhifa na mwaliko wa karamu hiyo ya Mwenyezi Mungu si ile ya jumla jamala ya kufaidika wanaadamu wote bali na viumbe wote duniani bali kitanga cha mwaliko huo ni cha watu maalumu na ni ugeni wa waja mahsusi wa Mwenyezi Mungu.

Suala la kimsingi kuhusu mwezi wa Ramadhani ni kwamba mwanaadamu – ambaye kutokana na mambo mbalimbali ameghafilika na amemsahau Mwenyezi Mungu; amezingirwa na hawezi kumfikia Mwenyezi Mungu, huku vishawishi mbalimbali vikimsukuma na kumporomosha kwenye daraja la chini – anapata fursa ndani ya mwezi huo ya kuweza moyo wake kupanda daraja na kusafika kwani kama ilivyo, dhati ya roho ya mwanaadamu na batini yake ni kupaa na kutafuta utukufu. Mwanaadamu katika mwezi wa Ramadhani hukurubia kwa Mwenyezi Mungu, akajipamba kwa maadili yaliyoamrishwa na Allah, akanyenyekea Kwake kwa kuujua uhakika wake. Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni kipindi cha machipuo ya kujijenga upya mwanaadamu, na ni kipindi bora cha kujikurubisha kwa Allah.

Baraka za Ramadhani huanzia kwa Waislamu wenyewe wanaotaka kuingia katika mwaliko wa ugeni wa Mwenyezi Mungu na huanzia ndani ya nyoyo. Kitu cha kwanza kabisa kinachopata baraka za mwezi huo ni nyoyo za waumini wenye kufunga, ambao wanaingia katika hali takatifu iliyobarikiwa ya mwezi wa Ramadhani. Kwa upande mmoja ni funga ya mwezi huo na kwa upande mwingine ni kusoma Qur’an katika mwezi huo; aidha ni kutokana na dua, ambazo ni mahsusi kwa mwezi wa Ramadhani ndiko kunakomfanya muumini aweze kupanda daraja katika mwezi huo. Dua humsafisha mwanaadamu, huitakasa na kuieua batini yake na kuijaza nuru. Sote kwa hakika tunalihitajia jambo hilo.

Mwezi wa Ramadhani wa kila mwaka ni mithili ya kipande cha peponi. Ni kama vile baada ya Mwenyezi Mungu kututia katika moto wa kupenda kwetu mambo ya kidunia, inapoingia Ramadhani hutupa fursa ya kwenda katika dhifa na mwaliko Wake na kutuingiza peponi. Baadhi yetu hufanikiwa kuingia peponi katika siku hizo hizo 30 tu za mwezi wa Ramadhani. Lakini wengine hufanikiwa kuingia peponi mwaka mzima kwa baraka za siku hizo 30, na wengine huingia peponi katika umri wao wote. Wengine hughafilika na jambo hilo, zikapita siku 30 bila ya kujali chochote na kwa hakika huko ni kuhasirika kukubwa. Mtu ambaye anapata taufiki ya kuwa na nguvu za kupambana na hawaa za nafsi kwa baraka za Ramadhani ajue kuwa ameneemeshwa na Mwenyezi Mungu na ni wajibu wake kuzilinda na kuzihifadhi kwa nguvu zake zote neema hizo. Mtu anayeteseka kwa vishawishi vya dunia na anayezidiwa nguvu na vishawishi vya kughururisha, na ambaye hupata mwanya katika mwezi wa Ramadhani kushinda vishawishi vyote hivyo, anapaswa kuendeleza tabia aliyojifunza kwenye mwezi wa Ramadhani katika umri wake wote. Matatizo yote yanayomkabili mwanaadamu yanatokana na hawaa na matamanio ya nafsi. Dhulma zote hizi, udanganyifu wote uliopo, utovu wote huu wa uadilifu, vita vyote hivi vya kidhulma, tawala zote mbovu na batili duniani pamoja na kusalimu amri kote huku mataifa ya dunia mbele ya dhulma za madhalimu kunatokana na kufuatwa hawaa za nafsi na kusalimu amri mbele ya matamanio ya nafsi. Kama mwanaadamu atajaaliwa kupata nguvu za kushinda hanjamu za nafsi, bila ya shaka atakuwa mtu mwema kama anavyotakiwa kuwa na Muumba wake. Mwezi wa Ramadhani hukuleteeni neema hiyo.

Hivyo kitu cha msingi ni kujiweka mbali na madhambi. Tunachopaswa kufanya kabla ya kuingia Ramadhani Inshaallah, ni kuzilea nafsi zetu na kuzizoesha kujiweka mbali na madhambi. Kama madhambi yatakuwa mbali nasi, hapo ndipo njia ya kupaa kwetu na kuelekea kwenye utukufu wa samawi (mbingu) itakapokuwa rahisi kwetu na hapo ndipo mtu atakapomudu kusafiri kimaanawi na kupata mbawa za kurukia katika safari hiyo tukufu. Lakini kama mwanaadamu atajibebesha mzigo wa madhambi hilo halitawezekana kwake. Mwezi wa Ramadhani kwa hakika, ni fursa nzuri ya kujiweka mbali na madhambi.

Saumu ambayo imetajwa kuwa ni taklifu na wajibu kwa mwandaamu kutoka kwa Muumba wake, kwa hakika ni atia na neema kutoka kwa Mola Mlezi. Ni fursa yenye thamani kubwa kwa watu wanaopata taufiki ya kufunga. Tab-an saumu nayo ina tabu zake. Kazi zote zenye baraka na faida haziachi kuwa na ugumu na tabu. Mwanaadamu hawezi kufika popote kama hawezi kuhimili tabu na mashaka. Kwa kweli tabu anayoipata mja wakati wa kufunga ni mtaji mdogo kabisa anaosumbuka kuuweka ikilinganishwa na faida kubwa mno anazozipata.

Saumu imetajwa kuwa na daraja tatu. Daraja zote hizo tatu zina manufaa kwa wale wenye kujua faida zake. Daraja ya kwanza ni hii ya funga kiujumla, yaani kujiepusha na kula, na kunywa na yote yanayobatilisha funga. Hata kama saumu yetu nzima itahusiana na hiyo imsaki na kujizuia tu basi pia ina manufaa mengi kwetu. Inatupa mazoezi na wakati huo huo kutufunza. Ni somo na wakati huo huo ni mazoezi ya kuhimili tabu za maisha. Ni mazoezi na wakati huo huo ni mafunzo. Imepokewa hadithi kutoka kwa Imam Sadiq AS isemayo: Mwenyezi Mungu amefaridhisha funga ili katika saa na siku za Ramadhamani, maskini na tajiri wawe katika hali moja. Mtu fakiri na maskini hawezi kununua, kula na kunywa anachopenda katika siku nzima lakini matajiri hupata chochote wanachotaka na hula na kunywa wanachopenda katika siku nzima. Mtu tajiri hawezi kupata hisia alizo nazo maskini na mtu fakiri ambaye anakosa anachopenda; lakini katika mwezi wa saumu, mwezi mtukufu wa Ramadhani, watu wote huwa sawa na hulazimika kujinyima mengi na kuepuka yote yanayokatazwa kufanywa wakati wa saumu.

Maana ya maneno hayo anaitambua vyema mtu aliyepata uzoefu wa kuhimili njaa na kiu na wakati huo huo mtu huyo hupata nguvu za kukabiliana na ugumu na mashaka yanayotokana na jambo hilo. Ramadhani humtunuku mwanaadamu subira na uvumilimu mbele ya tabu. Subira katika kutekeleza wajibu ni mazoezi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kumuongoa mwanaadamu. Zote hizo ni faida za daraja hiyo ya kwanza ya funga. Mbali ya kusafika tumbo la mfungaji na kujiepusha na mambo ambayo ni mubaha yanayoruhusiwa katika siku za kawaida, funga humzawaida pia mwanaadamu neema kubwa ya kupata nishati, unyofu, ukarimu na upole.

Daraja ya pili ya funga ni kujiweka mbali na madhambi, yaani kudhibiti masikio, macho, ulimi na moyo – bali kwa mujibu wa baadhi ya riwaya – hata ngozi ya mwili na nywele na malaika ya mwili wa mwanaadamu, kuvidhibiti visitende maasi.

Kama ambavyo mwenye kufunga anajinyima kula, kunywa na matamanio mengine ya nafsi wakati wa funga, anapaswa kujiepusha pia na madhambi. Daraja hii ni ya juu zaidi ikilinganishwa na daraja iliyopita ya funga. Fursa hii inayopatikana katika mwezi wa Ramadhani ni muhimu sana kwa ajili ya kufanya mazoezi ya kujiweka mbali na madhambi.

Hivyo daraja ya pili ya saumu ni mtu kuweza kujiweka mbali na madhambi hususan nyinyi vijana. Itumieni vyema fursa hii. Nyinyi ni vijana. Kijana ana nguvu, uwezo na vile vile usafi na nuru moyoni ya kuweza kuitumia vyema fursa hiyo. Itumieni fursa hiyo katika kipindi chote cha Ramadhani na fanyeni mazoezi ya kujiweka mbali na madhambi ambayo ni daraja ya pili ya funga.

Daraja ya tatu ya funga ni kujiepusha na jambo lolote ambalo linaisahaulisha akili ya mwanadamu, umuhimu wa kumkumbuka na kuwa karibu na Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo daraja ya juu ya saumu. Wakati funga inapohuisha utajo na kumkumbuka Mwenyezi Mungu ndani ya moyo wa mtu, mwanga wa kumtambua Allah hunawirika katika mtima wa mja. Hivyo kitu chochote kitakachompelekea mtu asahau kumkumbuka Mwenyezi Mungu, kina madhara kwa saumu katika daraja hiyo. Pongezi na hongera ziwaendee wanaojaaliwa kufika kwenye daraja hiyo.

Mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa kuweka akiba ya taqwa. Ni mwezi ambao inatupasa tufaidike na baraka za ibada na kumzingatia Mwenyezi Mungu ili tupate nduvu za kiroho na kimaanawi na tuweze kutumia nguvu hizo za kiroho na kimaanawi kuweza kuvuuka kwa haraka na urahisi vigingi vilivyopo na kuongoza njia kwa namna inayotakiwa.

Mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa kupata nguvu na nishati mpya. Mwezi wa Ramadhani ni mwezi ambao watu na matabaka yao mbalimbali wanapaswa kujipinda kwa ibada ndani yake ili kufika kwenye hazina za ghaibu na za kimaanawi na kuchota humo kadiri na kiwango chochote wanachotaka na kujiandalia mazingira ya maendeleo ya kiroho. Kama mtu katika mwezi wa Ramadhani ataipa umuhimu sala na kutekeleza majukumu yake ya kawaida pamoja na funga na dua akaongeza na kusoma Qur’ani – ambapo imetajwa kuwa mwezi wa Ramadhani ni kipindi bora kabisa cha Qur’ani – huwa mtu huyo amepitisha kipindi bora cha kujijenga, kujiokoa na kujiangalia upya sambamba na kujiweka mbali na maovu na vitu kama hivyo. Kwa hakika kipindi hicho ni cha thamani na faida kubwa.

Aidha katika mwezi wa Ramadhani – katika siku zote usiku na mchana – zinawirisheni nyoyo zenu kwa dhikri na kumtaja Allah ili kujiandaa kuingia katika anga takatifu ya Laylatul Qadr ambapo Qur’ani inasema:

لَيْلَةُ الْقَدْرِ خَيْرٌ مِّنْ أَلْفِ شَهْرٍ. تَنَزَّلُ الْمَلائِكَةُ وَالرُّوحُ فِيهَا بِإِذْنِ رَبِّهِم مِّن كُلِّ أَمْرٍ. سَلامٌ هِيَ حَتَّى مَطْلَعِ الْفَجْر.

 

Hiyo Lailatul Qadr (usiku wa heshima) ni bora kuliko miezi elfu. Huteremka Malaika na roho katika (usiku) huo kwa idhini ya Mola wao Mlezi kwa kila jambo. Ni amani (usiku) huo mpaka mapambazuko ya alfajiri. (Qur’an 97: 3-5).

Ni usiku ambao Malaika huunganisha ardhi na mbingu, wanazimiminia nuru nyoyo na kunawirisha mazingira ya maisha kwa nuru ya fadhila na rehema za Mwenyezi Mungu. Ni usiku wa amani na usalama wa kimaanawi. Ni usiku wa usalama wa roho na nyoyo. Ni usiku wa kuponya maradhi ya kimaadili na matatizo ya kimaanawi, magonjwa ya kimaada na maradhi ya yaliyozikumba jamii za mataifa mengi ulimwenguni hata baadhi ya mataifa ya Kiislamu. Kusalimika na matatizo yote hayo kunawezekana katika usiku wa Laylatul Qadr kwa sharti kwamba mtu aingie katika usiku huo wa baraka akiwa amejitayarisha na kujiandaa mapema.

Kila mwaka Mwenyezi Mungu Mtukufu huipatia dunia fursa ya kipekee nayo ni fursa ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Nyoyo husafika katika kipindi kizima cha Ramadhani, nyoyo hunawirika na kushadidi nuru, watu huwa katika hali ya kuweko tayari kuingia wakati wowote katika uwanda wa rehema maalumu za Mwenyezi Mungu zinazowafikia watu wote kulingania na walivyojiandaa, hima na juhudi zao. Baada ya kumalizika mwezi huo mbarikiwa, hufika siku ya kuanza mwaka mpya, siku yaIdil-Fitr. Yaani siku ambayo mtu anaweza kutumia matunda aliyoyapata katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, kuendeleza mwendo katika njia iliyonyooka ya Mwenyezi Mungu, na kujiweka mbali na njia za upotofu. Idil-Fitr ni siku ya kupokea zawadi na kuona rehema za Mwenyezi Mungu baada ya mwezi wa Ramadhani.

Kuna nukta moja katika siku ya Idil-Fitr nayo ni kuchukua maamuzi makubwa na ya kimsingi ya kujiandaa na kuukaribisha mwezi mwengine mtukufu wa Ramadhani katika kipindi kizima cha mwaka. Kama tunataka kuingia kwenye ugeni wa Mwenyezi Mungu katika kila mwezi wa Ramadhani na iwapo tunataka kuwemo katika wanaofaidika na usiku wa Lailatul Qadr na nyakati nyingine za usiku ndani ya mwezi huo, tunapaswa kujiandaa katika miezi mingine yote 11 ya mwaka kuukaribisha mwezi wa Ramadhani. Jipangie kwamba, katika majaaliwa yake Mola, mwaka ujao na ndani ya mwezi wa Ramadhani ujao utatenda mambo mazuri kiasi kwamba Ramadhani itakukubali na utakuwa na uso wa kwenda katika mwaliko wa Mwenyezi Mungu na kupata baraka zake. Hiyo ni neema kubwa sana ambayo mtu anaweza kuipata na ni njia ya kuwa na ufanisi katika mambo yote duniani na Akhera. Kama tutaingia katika mwezi wa Ramadhani tukiwa tumejiandaa ipasavyo, tutaweza kuneemeka zaidi na mwaliko huo wa Mwenyezi Mungu na mwaka mwingine tutakuwa tumepanda daraja ya juu zaidi ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake. Wakati huo ndipo mtakapoweza kushushudia mambo yanayokufurahisheni na kukuridheni ndani ya nafsi na nyoyo zenu na ndani ya maisha ya jamii yote kiujumla.

About Asadiq Media

Media for publicise the message of Wilaya under Imam Swadiq

Posted on June 22, 2013, in Hotuba na Mawaidha. Bookmark the permalink. Leave a comment.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Elijah J. Magnier

Middle East Politics

elbinawi

To interact with humanity & share ideas...

felicity114

felicity is the purpose of everybody

Ladakh Express

Ladakh's 1st political and cultural online journal.

Islamic Library

Shia Islamic PDFs - Now in Collaboration with ShiaTranslate.org!

zahraa Foundation

Fatima bint Muhammad is the Symbolization of Women's Power in Islam

mmubaraka1

A fine WordPress.com site

Pilgrim Center of Hope

Catholic Evangelization Ministry

World Shia Forum

Identity, Equality, Unity

Source of Inspiration

All is One, co-creating with the Creator

Bill Langill's Blog

Love is the Answer

Interrupting the Silence

An Episcopal Priest's Sermons, Prayers, and Reflections on Life, Becoming Human, and Discovering Our Divinity

Morgan L. Busse

In Darkness there is Light

YOGA

When unconscious became conscious this is Samadhi

Zoroastrians.net

Parsis, Iranis, Zarathushtis, All Under One Roof

Islamic Laws

Raising Awareness on Fiqh and the Ulema

Tech Cloud

Imagine | Innovate | Implement

Mujtaba Somji

Islamic sayings

%d bloggers like this: