MKUTANO WA KIONGOZI MUADHAMU NA RAIS PAMOJA NA BARAZA LA MAWAZIRI

MKUTANO WA KIONGOZI MUADHAMU NA RAIS PAMOJA NA BARAZA LA MAWAZIRI

28/08/2013

20130828_smplAyatullah Udhma Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, asubuhi ya siku ya Jumatano alikuwa na mkutano wa kwanza na Baraza la Mawaziri la Serikali ya 11. Katika mkutano huo Ayatullah Khamenei alipongeza uratibu na mashauriano yaliyofanyika baina ya serikali na bunge ili kuwezesha serikali mpya kuanza kazi haraka na akasema, Janabi Rohani ni Rais ni mwenye sifa zinazotakiwa, ni mtu mwenye kuaminika na mwenye rekodi safi ya kimapinduzi. Alivitaja vielelezo muhimu vya sifa inazopasa kuwa nazo serikali ya Kiislamu ikiwemo usafi wa kiitikadi na kiakhlaqi, kuwahudumia wananchi, uadilifu, usafi wa kiuchumi na kupambana na ufisadi, kufuata sheria, kuwa na hekima na kufanya mambo kwa busara na kutegemea vipawa na uwezo wa ndani ya nchi, na akasisitiza kwa kusema: Vipeni kipaumbele uchumi na elimu, na endeleeni na zidini kuwapa matumaini wananchi juu ya mustakabali kwa kudhibiti ughali wa bidhaa, kukidhi mahitaji ya lazima ya wananchi, kustawisha uzalishaji na kuanzisha harakati na kuleta utulivu katika uga wa uchumi.

Aidha alisema kuhusu vitisho vya Marekani vya kuingilia kijeshi nchini Syria kuwa hilo ni janga lisilo na shaka kwa eneo na akasisitiza kwamba: Uingiliaji wowote na uanzishaji vita wowote hauna shaka yoyote kuwa utakuwa na madhara kwa wawashaji moto huo.

Ayatullah Khamenei alitoa mkono wa kheri na baraka kwa mnasaba wa Wiki ya Serikali kwa viongozi wote, mamudiri na wafanyakazi watumikivu katika mhimili huo wa utendaji na akaeleza kuwa: Wiki ya Serikali imepambika kwa majina ya mashahidi wawili wateule Rajai na Bahonar, na hatua zinazochukuliwa na serikali zote za kuyafanya majina na malengo ya mashahidi wawili hawa kuwa ndio dira na muongozo wao ni kitendo chenye maana kubwa.

Aliisifu hatua ya haraka na ya ufatiliaji ya Rais ya kuwatambulisha mapema mawaziri kwa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) na akasema: Kiwango kizuri cha kura ambazo Bunge liliwapigia mawaziri waliopendekezwa nacho pia kiliandaa mazingira kwa serikali mpya kuanza kazi zake haraka, na suala hili linaonyesha uratibu na mashauriano mazuri yaliyofanyika baina ya mihimili miwili ya dola na jinsi Rais na Bunge yanavyojali suala la kuanza haraka shughuli za serikali; na hili linapasa kupongezwa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema ana matumaini kwamba nukta chanya za serikali ya 11 zitaweza kuonekana kivitendo na kuendelea na kuongezeka utiaji matumaini kwa wananchi na akaongezea kwa kusema: Hapana shaka kuwa nafsi ya Janabi Rohani ambaye “amekuwa na rekodi safi ya mapambano na ya Mapinduzi na misimamo mizuri na sahihi katika miongo mitatu iliyopita” ni miongoni mwa nukta chanya za serikali mpya.

Aliashiria pia azma ya dhati ya Rais ya kutatua matatizo na akasema: Inshallah kutokana na kuwa na azma thabiti na kwa kufuata njia sahihi, Baraza la Mawaziri litaweza kutekeleza majukumu mazito liliyonayo.

Hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mkutano wa kwanza na Baraza la Mawaziri la Serikali ya 11 iliendelea kwa kubainisha vielelezo muhimu vya sifa inazotakiwa kuwa nazo serikali ya Kiislamu.

Ayatullah Khamenei alisema usafi wa kiitikadi na kiakhlaqi ni miongoni mwa sifa muhimu inayotakiwa kuwa nayo serikali ya Kiislamu na akaifafanua nukta hiyo kwa kusema: Itikadi hizi na mtazamo sahihi juu matukio halisi ya jamii vitaufanya utendaji wa serikali uwe safi.

Kuhusiana na suala hilohilo alieleza kuwa majimui ya hotuba, miongozo na misimamo ya Imam Khomeini (Radhi za Allah ziwe juu yake) ndivyo vielelezo vya msingi na akasisitizia juu ya nukta hiyo kwa kusema: Misingi na thamani za Mapinduzi zinaonekana wazi kwenye hotuba na misimamo ya Imam, hivyo kama tutashikamana nayo na kufungamana nayo kivitendo na kuifanya ndio marejeo pia pale unapokuwepo utata, kwa fadhila za Mwenyezi Mungu kazi zote zitakuwa na “mustakabali mwema”na tutapiga hatua mbele.

Katika kutoa ufafanuzi zaidi juu ya kielelezo cha usafi wa kiitikadi na kiakhlaqi, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema kuna ulazima mkubwa wa kuwa na yakini na imani kamili juu ya ahadi ya kupata msaada wa Mwenyezi Mungu na akaongezea kwa kusema: Katika tajiriba kadhaa ikiwemo ya ushindi wa Mapinduzi, Kujihami Kutakatifu na ushindi dhidi ya uasi kadhaa wa kikabila uliotokea mwanzoni mwa baada ya Mapinduzi, wananchi na viongozi nchini walikuhisi kikamilifu kuthibiti kwa ahadi za Mwenyezi Mungu; na tajiriba hizi zenye thamani ni utangulizi wa kuwa na imani kamili zaidi juu ya ahadi ya kupata auni na msaada wa Mwenyezi Mungu.

Ayatullah Khamenei aliashiria hotuba ya Rais Rohani na akasema: Kuwa na imani juu ya Mwenyezi Mungu na kuwa na mtazamo sahihi, wa kimantiki na wa busara ndivyo vitakavyowezesha kutatua masuala.

Kuwatumikia viumbe, ndicho kielelezo cha pili alichozungumzia Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kuelezea sifa maalumu inazopaswa kuwa nazo serikali nzuri ya Kiislamu.

Alisema kuwahudumia watu ndio msingi mkuu wa serikali ya Kiislamu na falsafa ya kuwepo viongozi, na akasisitiza kwa kusema: Jambo lolote lile lisiwafanye viongozi wakaghafilika na kuwahudumia wananchi.

Ayatullah Khamenei alisema: Mitazamo na utashi tofauti wa kisiasa – kiuchumi na kijamii ni masuala ya pembeni, na kuwahudumia wananchi ndilo suala la msingi, kwa hivyo msiruhusu masuala ya pembeni yaathiri lile la msingi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliitanabahisha serikali mpya juu ya kupita kwa kasi fursa ya kuwahudumia wananchi na akaongezea kwa kusema: Serikali nyengine zote zilizopita niliziambia kuwa fursa ya miaka minne au minane ya uongozi inapita kwa kasi, lakini muda huohuo wenye mpaka maalumu ndani yake una fursa zisizo na kikomo za kuwahudumia wananchi na haifai kuipoteza yoyote kati ya hizo.

Kuhusu suala la kuwahudumia wananchi, Ayatullah Khamenei alisema, kuwa na mtazamo na kuchapa kazi kijihadi ni kitu chenye thamani, na akafafanua kwa kusema: Kufanya kazi kijihadi maana yake si kufanya kazi bila ya kujali sheria. Mimi binafsi ni mtu ninayepinga ukiukaji sheria; lakini kwa kuchunga na kufuata sheria pia inawezekana kufanya kazi kwa “mtazamo wa kijihadi na wa shauku ya kufikia malengo ya juu kabisa” kinyume na mtazamo wa ufanyaji kazi uliozoeleka wa kiidara, na kwa njia hiyo kuweza kuvivuka vizuizi vilivyopo.

Ayatullah Khamenei alisema uadilifu ni kielelezo kingine muhimu cha sifa inayotakiwa kuwa nayo serikali ya Kiislamu na akaongezea kwa kusema: Kama ilivyokwishasisitizwa hapo kabla pia kwamba sisi tunataka tuwe na maendeleo au kama inavyoelezwa kwa istilahi iliyozoeleka kuwa na ustawi, lakini hakuna shaka yoyote kuwa maendeleo hayo lazima yaambatane na uadilifu la sivyo kama ilivyo katika nchi za Magharibi, jamii itakumbwa na mpasuko, ubaguzi na manung’uniko.

Usafi wa kiuchumi na kupambana na ufisadi ni kielelezo cha nne kinachotakiwa katika serikali ya Kiislamu kwa mtazamo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Kuhusiana na nukta hiyo aliwaelezaviongozi wa serikali mpya kwa kusema: Nyadhifa za utawala ni mahala panapotia wasiwasi wa madaraka na rasilimali za kimaada, hivyo muwe macho muda wote kwa kuvichunga vyombo vilivyoko chini ya uendeshaji wenu kwa namna ya mithili ya mwanga wa kurunzi unaomulika na kuangaza huko na kule muda wote ili        viweze kusalimika na wasiwasi wa ufisadi.

Ayatullah Khamenei aliashiria kuwepo vyombo vya ukaguzi na usimamizi katika mihimili yote mitatu ya dola, na akawaelekea viongozi wa serikali kwa kuwaambia: Ufisadi ni mithili wa mchwa, hivyo chukueni hatua madhubuti na kwa tadbiri ili kuzuia upenyaji wa “ufisadi, upendeleo wa kujuana, rushwa na israfu” ili kusiwepo kabisa na haja ya vyombo vya ukaguzi na usimamizi kuingilia mamlaka yenu ya uendeshaji.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliwaelezea wafanyakazi na viongozi wa vyombo vya utendaji serikalini kuwa ni watu safi na wenye muamana na akaongezea kwa kusema: Kwa bahati mbaya kuwepo baadhi ya watu wasio safi ambao ni mithili ya virusi kunatia doa juhudi na jitihada za wafanyakazi watumikivu wa vyombo vya serikali; hivyo inapasa hatua zichukuliwe kuzuia hali hii.

Ayatullah Khamenei aliutaja ufuataji sheria kuwa ni kielelezo kingine muhimu sana cha sifa inayotakiwa kuwa nayo serikali inayokubalika na akasema: Sheria inapasa iwe ndiyo njia ya kupitia reli ya serikali, na kama itatokezea kwa sababu yoyote ile reli hiyo kukengeuka na kutoka nje ya njia hiyo nchi na wananchi wataumia.

Alifafanua zaidi kwa kusema: Inawezekana baadhi ya sheria zikawa na kasoro na walakini, lakini madhara ya kutozitekeleza sheria hizo hizo ni makubwa zaidi kuliko ya kuzitekeleza, hivyo jitahidini mhakikishe ufuataji sheria unarasimishwa katika vyombo vyote.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliuashiria utekelezaji wa hati kuu ikiwemo ya Sera Kuu za Mfumo na hati ya Malengo ya Mustakabali kuwa ni miongoni mwa masharti ya lazima ya ufuataji sheria na akasema: Maazimio yaliyopasishwa na Mabaraza Makuu likiwemo Baraza Kuu la Mapinduzi ya Kiutamaduni na Baraza Kuu la Mawasiliano ya Kompyuta ambayo ni maazimio muhimu sana, yanapasa yapewe itibari na kufanyiwa kazi kulingana na maazimio hayo. Kuhusiana na suala hilo hilo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisisitiza kuwa Sera Kuu za Mageuzi ya Mfumo wa Kiidara nazo pia zina umuhimu mkubwa sana na akaongezea kwa kusema: Kwa bahati mbaya utekelezaji wa sera hizi umechelewa, hivyo inapasa zitekelezwe.

Hekima na utumiaji busara ni kielelezo cha sita alichokitilia mkazo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mkutano na Rais Rohani na baraza lake la mawaziri.

Aliiagiza serikali kwa sisitizo kubwa juu ya kuvitumia vipawa na uwezo mzuri wa wataalamu wa ndani katika nyanja na sekta zote na akaongezea kwa kusema: Inapasa kabla ya kuchukua hatua yoyote ile na au hata kutoa matamshi na kuchukua msimamo wowote, ufanyike utafiti wa kitaalamu unaohitajika, kwa sababu gharama ya kufuta athari hasi ya hatua za kiuanagenzi na matamshi yasiyo na nadhari ni kubwa mno.

Kutegemea zaidi vipawa na uwezo wa ndani ya nchi, ni nukta nyengine muhimu ambayo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliwataka viongozi wa serikali waizingatie na akasisitizia kwa kusema: Ufunguo wa utatuzi wa matatizo uko kwenye uwezo na suhula za ndani ya nchi ambazo zinapasa kutumiwa kwa busara.

Katika kutolea ufafanuzi zaidi umuhimu wa kutegemea vipawa na uwezo wa ndani wa nchi, Ayatullah Khamenei alisema: Maneno haya maana yake si kuacha kutumia uwezo wa nje, bali nukta ya msingi hapa ni kwamba tusielekeze imani na mategemeo yetu nje.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliashiria kambi ya maadui wa Mapinduzi na akasema: Ukweli wa mambo ni kuwa kambi ya uadui haiwezi na haifai kuitegemea kuwa na urafiki na upendo.

Alifafanua zaidi kwa kueleza kwamba: Fungu la kila nchi katika mahusiano ya kimataifa linategemea nguvu na uwezo wa ndani wa nchi hiyo, kwa hivyo inabidi zifanyike jitihada za kuhakikisha mwenendo wa kuongeza nguvu na uwezo wa ndani ya nchi unaendelezwa na kuimarishwa.

Katika sehemu nyengine ya hotuba yake Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliashiria nukta kadhaa kuhusu vipaumbele vya msingi na muhimu zaidi kwa serikali ya 11. Ayatullah Khamenei aliashiria nguvu mpya waliyonayo mawaziri wa serikali na wakati huohuo fursa zenye mpaka na muda wa kuzitumia fursa hizo na akasisitiza kwa kusema: Masuala ya uchumi na maendeleo ya elimu ndivyo vipaumbele viwili vikuu kwa nchi ambavyo vinapasa kuzingatiwa na kupewa umuhimu maalumu na mhimili wa serikali na pia mihimili mingine ya dola.

Kuhusu masuala ya kiuchumi aliashiria misingi mikuu ya uchumi iliyowekwa nchini katika kipindi cha miaka 10 iliyopita na akaongezea kwa kusema: Kwa kuzingatia misingi hii, hatua ya haraka inayopasa kuchukuliwa na serikali inapasa iwe ni kuleta uthabiti na utulivu wa kifikra kwa wananchi na kwa soko la biashara, kupunguza ughali wa maisha, kukidhi mahitaji ya msingi ya wananchi na kuupa msukumo na harakati uzalishaji wa taifa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alifafanua kwa kusema: Hatua hizi za haraka, hakika yake hasa ni kuanza “Hamasa ya Kiuchumi” ambayo ilisisitizwa na kutiliwa mkazo mwanzoni mwa mwaka.

Ayatullah Khamenei aliongezea kwa kusema:  Bila ya shaka kuthibiti kwa Hamasa ya Kiuchumi kunahitajia harakati ya muda mrefu, na hakuna mtu yeyote mwenye insafu anayetarajia serikali itatue matatizo yote ya kiuchumi kwa haraka lakini matarajio yaliyopo ni ya kuwepo harakati kuelekea kwenye utatuzi kwa mtazamo wa hekima na tadbiri.

Aliashiria pia kujadiliwa kwa Sera za Uchumi wa Muqawama katika Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo na akasema: Uchumi wa Muqawama maana yake si uchumi wa kujikhini bali ni uchumi utakaoweza kusimama imara kukabiliana na migogoro na dhoruba za kimataifa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliashiria pia harakati ya kasi kubwa ya kielimu iliyoanza tangu miaka 10 nyuma na akasisitiza kwa kusema: Harakati hii ya kielimu inayokwenda kwa kasi kubwa isisitishwe kwa namna yoyote ile.

Ayatullah Khamenei alisema ufunguo hasa wa utatuzi wa matatizo ya kiuchumi ya nchi ni kutegemea elimu, na akaongezea kwa kufafanua kuwa: Katika upande wa uchumi, kutegemea maendeleo ya elimu na mashirika ya uzalishaji elimu, bila ya shaka kutaufanya uuzaji mafuta na malighafi nyingi uwe na faida kubwa zaidi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema Wizara ya Sayansi na Teknolojia na Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu ndio wahusika wakuu wa harakati ya elimu nchini na akaongezea kwa kusema: Wizara na vyombo vya utoaji huduma kama vile Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko na Wizara ya Jihadi ya Kilimo zinapasa ziwe na mashirikiano ya karibu na wahusika hao wawili wakuu ili kuandaa mazingira ya kutumiwa maendeleo ya kielimu ya Vyuo Vikuu na taasisi za kielimu na kuongeza maradufu kasi ya harakati ya elimu ya Vyuo Vikuu.

Ayatullah Khamenei aliiagiza serikali kwa sisitizo maalumu kuyasaidia mashirika yanayozalisha elimu na akafafanua kwa kusema: Moja ya maudhui muhimu katika harakati ya elimu nchini ni kuukamilisha mnyororo wa sayansi na teknolojia. Katika kuutolea ufafanuzi mnyororo huo aliongezea kwa kusema: Mnyororo huu unaanza kwa dhana na fikra na kisha unafikiwa kwa sayansi na teknolojia na hatimaye unaishia kwenye uzalishaji na soko; kwa hivyo kufikia kwenye teknolojia tupu hakutoshi, bali mnyororo huu unapasa ukamilishwe hadi kufikia mwisho wake.

Katika sehemu nyengine ya hotuba yake Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliashiria maudhui ya Sera za Nje na akasisitiza kwa kusema: Ikiwa katika uga huu izza, hekima na maslahi yatafahamika kwa usahihi na kutekelezwa kwa usahihi pia sera za nje zitakuwa katika mlingano sawa na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ayatullah Khamenei aliashiria hali nyeti na ya mgogoro ya eneo na akasema: Sisi hatuna nia yoyote ya kutaka kuingilia masuala ya ndani ya Misri, lakini hatuwezi kufumbia macho mauaji ya wananchi wa Misri.

Alisisitiza kwa kusema: Sisi tunalaani mauaji ya wananchi wa Misri ambao waliuliwa ilhali hawakuwa na silaha.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliongezea kwa kusema: Kwa mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mhusika wa mauaji haya, awe mtu yeyote yule anastahili kulaaniwa.

Ayatullah Khamenei alisema: Vita vya ndani vinapasa viepukwe kikamilifu nchini Misri kwa sababu vita vya ndani nchini Misri vitakuwa ni janga na maafa kwa Ulimwengu wa Kiislamu na eneo.

Alitilia mkazo ulazima wa kurejeshwa demokrasia nchini Misri na kupewa wananchi nafasi ya kuchagua na akasema: Baada ya miaka na miaka ya utawala wa kiimla, na kwa baraka za Mwamko wa Kiislamu, wananchi wa Misri wamefanya uchaguzi safi; na mwenendo huu wa kidemokrasia hauwezi kusimamishwa.

Kuhusu matukio ya Syria, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema vitisho na uingiliaji ambao huenda ukafanywa na Marekani vitasababisha maafa kwa eneo, na akasisitiza kwa kusema: Endapo hatua kama hiyo itachukuliwa, bila ya shaka Wamarekani watapata hasara kama ilivyokuwa katika uingiliaji wa Iraq na Afghanistan.

Ayatullah Khamenei aliongezea kwa kusema: Uingiliaji wa madola ya kigeni na ya nje ya eneo ndani ya nchi yoyote hautokuwa na tija nyengine isipokuwa kuwasha moto na kuzidisha pia chuki za wananchi wa mataifa dhidi yao.

Alisisitiza kwa kusema: Uwashaji moto huu utakuwa mithili ya cheche ya moto ndani ya ghala la baruti ambalo athari zake na ukubwa wake hautoweza kujulikana.

Katika mkutano huo Hujjatul Islam Walmuslimin Rais Hassan Rohani alitoa hotuba ya utangulizi, ya kuadhimisha Wiki ya Serikali na kuadhimisha pia kumbukumbu ya mashahidi Rajai na Bahonar. Aidha alibainisha muelekeo wa ndani na wa nje wa serikali ya kumi na moja, hali ya sasa ya nchi na vilevile mazingira ya eneo na ya kimataifa.

Rais Rohani alisisitiza kwamba juhudi za serikali ya kumi na moja zitaelekezwa katika kutumia na kunufaika na tajiriba na mafanikio ya serikali zilizopita na wakati huohuo kujifunza kutokana na baadhi ya kasoro za serikali zilizotangulia na akaongezea kwa kusema: Muelekeo wa serikali katika uga wa siasa za ndani ni kudhamini usalama unaohitajika katika pande zote kwa ajili ya utulivu wa jamii na kuhakikisha wananchi wanapata haki zao za kiraia.

Dakta Rohani alisema moja ya malengo makuu ya serikali ya kumi na moja ni kuleta mwafaka, mshikamano na mfungamano wa nyoyo katika jamii, kupunguza mipasuko na kutumia vipawa na uwezo wa wale wote wenye uchungu na wenye kushikamana na “Mapinduzi, njia ya Imam na mwongozo wa Kiongozi Muadhamu” na akafafanua kwa kusema: Kutokana na hamasa ya tarehe 24 Khordad (ya uchaguzi wa Rais) imani na matumaini ya wananchi, ambayo ndiyo rasilimali kubwa zaidi ya nguvu na amani ya taifa, vimeongezeka, na serikali imekusudia kwa dhati kulinda na kuzidisha imani na matumaini hayo.

Katika kubainisha muelekeo wa serikali ya kumi na moja katika uga wa sera za nje, Rais Rohani aliashiria uingiliaji wa madola ya kigeni na hali ya machafuko makubwa inayotawala katika eneo na akasema: Katika mazingira kama haya, nchi ya Iran ina uthabiti, utulivu na usalama wa taifa kwa maana yake halisi, lakini adui anajaribu kutumia mashinikizo ya kisiasa na kiuchumi ili yawe na taathira kwa jamii na wananchi.

Hujjatul Islam Walmuslimin Rohani alisisitiza kwa kusema: Licha ya kuwepo mashinikizo yota haya taifa la Iran limeonyesha kuwa litasimama imara kukabiliana na vikwazo na wala halitobadilisha mawazo juu ya haki zake za wazi kabisa.

Rais Rohani aliongezea kwa kusema: Japokuwa vikwazo vimewaletea wananchi matatizo kadhaa lakini vikwazo hivi vitazifanya ziwe kubwa zaidi chuki za kihistoria za wananchi kwa nchi zinazotekeleza vikwazo hivi hususan Magharibi.

Dakta Rohani alifafanua kwa kusema: Serikali imeutangazia bayana ulimwengu kuwa badala ya lugha ya vikwazo itumike lugha ya heshima katika kuzungumza na taifa la Iran.

Rais Rohani aliongezea kwa kusema: Katika uga wa kimataifa serikali itatumia lugha ya kujenga maelewano na kuishi kwa amani na masikilizano na wakati huohuo lugha ya muqawama na kusimama imara.

Rais Rohani aliwasilisha ripoti pia kuzungumzia hali ya nchi na akasema: Matatizo yanayotokana na mashinikizo ya kiuchumi yamesababisha sekta mbalimbali nchini yakiwemo mabenki na mawakala wa uzalishaji wakabiliwe na matatizo kadha wa kadha.

Dakta Rohani aliashiria kutokamilika kwa sehemu ya bajeti ya mwaka huu ya tomani bilioni 210 na kuongeza kuwa: Ni kwa sababu hii serikali inajaribu kuifanyia marekebisho bajeti ya mwaka 92 (2013/14) kwa kufikiria njia mpya za utendaji kwa ajili ya kujinasua na hali ya hivi sasa.

Rais Rohani alisema kukidhi mahitaji ya bidhaa za lazima, kudhamini mapato ya ruzuku taslimu na kufanya juhudi za kuongeza uzalishaji wa mafuta na gesi ni vipaumbele vitatu vya serikali katika sekta ya uchumi na akafafanua zaidi kwa kusema: Kamisheni ya uchumi ya serikali imepewa jukumu la kuhakikisha ndani ya muda wa siku 15 inavianisha vizuizi vinavyokwamisha ustawishaji wa uchumi na kisha kuwasilisha njia za utatuzi wa muda mfupi wa kuvivuka vizuizi hivyo. Hujjatul Islam Walmuslimin Rohani aliongeza kuwa: Kila wiki hufanyika vikao viwili chini ya uenyekiti wa Rais kwa ajili ya kushughulikia utatuzi wa matatizo ya kiuchumi.

Rais Rohani alisisitiza kwa kusema: Licha ya kuwepo matatizo na masuala tata yote hayo serikali ina matumaini kamili juu ya mustakabali na imedhamiria kwa dhati kutatua matatizo.

Dakta Rohani aliwaelezea mawaziri wa serikali yake kuwa ni wana wa Mapinduzi, wafuasi wa njia ya Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu Amrehemu) na watu wenye kushikamana na miongozo ya Kiongozi Muadhamu na akaongezea kwa kusema: Viongozi wote wa serikali wako tayari kujitolea, kuwahudumia wananchi na kutatua matatizo.

Mwishoni Rais Rohani alimshukuru Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa himaya na uungaji mkono wake kwa serikali ya kumi na moja na akaipongeza Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) kwa ushirikiano iliotoa katika upigaji kura za kuwa na imani na mawaziri.

About Asadiq Media

Media for publicise the message of Wilaya under Imam Swadiq

Posted on September 8, 2013, in Habari na Matukio. Bookmark the permalink. Leave a comment.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Elijah J. Magnier

Middle East Politics

elbinawi

To interact with humanity & share ideas...

felicity114

felicity is the purpose of everybody

Ladakh Express

Ladakh's 1st political and cultural online journal.

Islamic Library

Shia Islamic PDFs - Now in Collaboration with ShiaTranslate.org!

zahraa Foundation

Fatima bint Muhammad is the Symbolization of Women's Power in Islam

mmubaraka1

A fine WordPress.com site

Pilgrim Center of Hope

Catholic Evangelization Ministry

World Shia Forum

Identity, Equality, Unity

Source of Inspiration

All is One, co-creating with the Creator

Bill Langill's Blog

Love is the Answer

Interrupting the Silence

An Episcopal Priest's Sermons, Prayers, and Reflections on Life, Becoming Human, and Discovering Our Divinity

Morgan L. Busse

In Darkness there is Light

YOGA

When unconscious became conscious this is Samadhi

Zoroastrians.net

Parsis, Iranis, Zarathushtis, All Under One Roof

Islamic Laws

Raising Awareness on Fiqh and the Ulema

Tech Cloud

Imagine | Innovate | Implement

Mujtaba Somji

Islamic sayings

%d bloggers like this: