Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Viongozi Wa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Aonana na Viongozi Wa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu
23/06/2015
20150624Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo jioni (Jumanne) ameoanana na viongozi wa Mihimili Mitatu Mikuu wa Dola (Serikali, Bunge na Mahakama) pamoja na viongozi na wakuu wengine wa ngazi za juu ya Jamhuri ya Kiislamu na sambamba na kubainisha matokea chanya, changamoto na njia mbali mbali za kuweza kuufanikisha uchumi wa kusimama kidete, ameainisha nukta kadhaa muhimu kuhusiana na mchakato wa mazunguzo ya nyuklia na huku akitoa ufafanuzi wa wazi kuhusu mistari myekundu ya kadhia ya nyuklia ya Iran amesisitiza kwamba: Inachopigania Marekani ni kuangamiza kabisa miradi ya nyuklia ya Iran. Amesema katika upande wa pili wanachotaka viongozi wote wa Iran ni kuwa na makubaliano mazuri yaani makubaliano ambayo yatadhamini kiinsafu, kiheshima na kimantiki, manufaa na maslahi ya Iran sambamba na kulindwa mistari yake myekundu.
Mwanzoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia fadhila za mwezi wa Ramadhani ambao ni mwezi wa taqwa na kumcha Mwenyezi Mungu na kusema kuwa, kuna taqwa za aina mbili, taqwa ya mtu binafsi na taqwa ya kijamii. Ameongeza kuwa: Taqwa ya mtu binafsi kwa hakika ni ile hali ya kujichunga siku zote ambayo inampa kinga mtu mbele ya mashambulizi angamizi ya matatizo ya kimaanawi na ambayo tab’an ina taathira kubwa pia katika masuala yake ya kimaada na kidunia.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuwa, taqwa ya kijamii inaweza kujumuishwa kwenye masuala ya kijamii na kiuchumi na kusisitiza kwamba: Taqwa ya kijamii katika masuala ya kiuchumi, ndio huo uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete ambao unailinda nchi mbele ya mitikisiko itokanayo na matukio mbali mbali duniani na mbele ya mashambulizi ya kiuadui ya siasa za maadui duniani.
Aidha amegusia tahadhari zake za mara kwa mara alizozitoa katika miaka ya huko nyuma kuhusiana na ulazima wa kuiimarisha nchi mbele ya mifumo ya kiuchumi ya madola ya kibeberu na kuongeza kuwa: Katika miaka hiio yote, viongozi nchini Iran wamefanya jitihada kwa kadiri ya uwezo wao kuuendesha uchumi huo lakini suala la uchumi wa kusimama kidete linahitajia kutumika nguvu na uwezo wote wa nchi kulifanikisha.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, mfano wa uchumi wa kusimama kidete umejaribiwa pia katika nchi nyingine duniani na kuzaa matunda mazuri na kuongeza kuwa, mhimili na nguzo kuu ya uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete imesimama kwenye uzalishaji wa ndani na kutegemea nguvu za ndani ya nchi. Ameongeza kuwa, kutegemea uzalishaji wa ndani hakuna maana ya kujitenga na kujiweka mbali na maeneo mengine duniani bali kuna maana ya kutegemea uwezo na nguvu za ndani bila ya kujitenga na kujiweka mbali na maeneo mengine ya dunia.
Ayatullah Udhma Khamenei ameitaja kazi za kubuni na kuandaa siasa za uchumi wa kusimama kidete kuwa imezingatia hali ya ndani ya kijamii na mashauriano ya muda mrefu na kuongeza kuwa: Baada ya kuwasilishwa siasa hizo, wataalamu wengine wa uchumi waliuunga mkono uchumi huo na hivi sasa uchumi wa kusimama kidete umeshaingia kwenye fasihi na utamaduni wa kiuchumi ulioenea sehemu zote nchini.
Vile vile amesema, modeli ya uchumi wa kusimama kidete inatofautiana kikamilifu na modeli ya kizamani ya uchumi ambao madola ya kiistikbari na kibeberu yamezitwisha nchi za ulimwengu wa tatu na kuongeza kuwa: Modeli ya zamani ya uchumi imesimama juu ya msingi ya kuangalia nguvu za nje, lakini modeli ya uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete imesimama juu ya msingi wa kujiinua kiuchumi kwa kutegemea nguvu na uwezo wa ndani ya nchi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Kuna uwezekano baadhi ya watu wakadhani kuwa, modeli ya uchumi wa kusimama kidete ni modeli na kigezo kizuri cha kiuchumi lakini haitekelezeki. Hata hivyo ninasema kwa kujiamini nikiwa na yakini kwamba, kutekeleza kigezo cha uchumi wa kusimama kidete katika mazingira ya hivi sasa ya nchi yetu na kwa kuzingatia uwezo mbali mbali tulio nao, ni jambo linalowezekana kikamilifu.
Baada ya kutoa utangulizi huo, Ayatullah Udhma Khamenei amebainisha uwezo mkubwa ilio nao Iran ambao unaweza kuwa msingi wa kuendeshea siasa za uchumi wa kusimama kidete akisema kuwa, nguvu ya vijana wasomi wenye utaalamu wa kila namna na wanaojiamini ni uwezo wa kwanza wa ndani ya nchi unaoweza kutumika kuendeshea siasa za uchumi huo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Kuwepo idadi hiyo ya nguvu kazi ya vijana wasomi nchini ni katika baraka za Mapinduzi ya Kiislamu na nguvu hiyo itaweza kuwa na manufaa makubwa nchini kama siasa zisizo sahihi zinazopelekea kuzeeka jamii na kupungua idadi ya vijana, zitarekebishwa.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia kuweko watu milioni 10 waliomaliza masomo katika Vyuo Vikuu mbali mbali nchini Iran na zaidi ya wanafunzi milioni nne wa Vyuo Vikuu wanaoendelea na msomo hivi sasa ikiwa ni ongezeko la mara 25 ikilinganishwa na hali ilivyokuwa mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu na kusisitiza kuwa: Idadi hiyo ya nguvu kazi ya wasomi na wataalamu wa kila aina na wa fani mbali mbali ni fakhari kwa Jamhuri ya Kiislamu na ni fursa kubwa sana kwake.
Aidha ameitaja nafasi ya kiuchumi nchini kuwa ni uwezo mwengine muhimu ilio nao Iran na kuongeza kuwa: Kwa mujibu wa takwimu za kimataifa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inashika nafasi ya 20 katika uchumi wa dunia, na iwapo uwezo wake wa kiuchumi utatumiwa vizuri, kuna uwezekano wa kufikia nafasi ya 12 ya kuwa na uchumi bora duniani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kuwa na nafasi ya kwnza Iran katika majimui za nchi zenye utajiri wa gesi na mafuta duniani kuwa ni uwezo mwengine muhimu unaoweza kutumika vizuri kuendeshea sisa za uchumi wa kusimama kidete na pia ameashiria nafasi muhimu na ya kipekee ya kijiografia ya Iran ikiwa ni nukta muhimu duniani ya kuyaunganisha maeneo ya kaskazini na kusini na mashariki na magharibi mwa dunia na kuongeza kuwa: Fursa ya kupakana na nchi 15 zenye jamii ya watu milioni 370, likiwa ni soko kubwa lililoko karibu sana na Iran na kutokana na Iran kuwa na idadi ya watu zaidi ya milioni 70 likiwa ni soko kubwa la ndani, ni fursa na nafasi nyingine ambayo kama soko la ndani tu litatumika vizuri basi hali ya uzalishaji wa ndani itabadilika kabisa.
Ayatullah Udhma Khamenei ameitaja miundombinu muhimu ya nchi katika sekta za nishati, usafirishaji, mawasiliano, vinu mbali mbali, mabwawa pamoja na uzoefu mkubwa wa kuendesha mambo tofauti ni uwezo na fursa nyingine muhimu ya kuweza kufanikisha uchumi wa kusimama kidete na kuongeza kuwa: Tunapaswa kuutumia vizuri uwezo huo wote kwani tatizo la nchi yetu si kutokuwepo mipango au fikra sahihi na za kiutalaamu bali tatizo kubwa ambalo linaonekana pia kati ya watu wenye vipaji, ni kutotumiwa vizuri mipango na fikra sahihi zilizopo.
Vile vile amesema kuwa, baadhi ya matatizo yanatokana na changamoto za ndani ya nchi na amebainisha sehemu moja ya changamoto hizo akisema: Changamoto kuu iliyo nayo nchi yetu hivi sasa ni kutoipa sekta ya kazi uzito unaotakiwa na kuyaangalia mambo kwa upeo wa chini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Mijadala na fikra za maneno matupu haziwezi kufanikisha chochote, bali utatuzi wa masuala unahitajia harakati, kuchukuliwa hatua na kufuatilia kwa muda mrefu masuala mbali mbali.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, kuna uwezekano matunda ya baadhi ya kazi kubwa yakahitajia muda mrefu kuonekana na kuongeza kwamba: Katika ule wakati ambapo kwenye Vyuo Vikuu kulikuwa kunazungumzwa suala la mwamko wa kielimu nchini, kulikuwa na baadhi ya watu waliokuwa hawaamini kwamba baada ya kupita miaka 10 hadi 15 kungeliweza kushuhudiwa harakati hii kubwa ya kielimu ya hivi sasa nchini kwa hima ya wahadhiri na vijana wetu wenye vipaji vya kila namna lakini leo hii ikilinganishwa na miaka hiyo ya huko nyuma, tunaona kuweko maendeleo makubwa bali katika baadhi ya nyuga maendeleo hayo ni ya kustaajabisha kabisa.
“Njia nyeupe na rahisi lakini wakati huo huo hatari na angamizi,” ni changamoto nyingine ya ndani ya nchi ambayo imegusiwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuitolea ufafanuzi akisema: Baadhi ya wakati suala la kudhamini baadhi ya bidhaa na mahitaji linawezekana kwa kutumia njia mbili tofauti, njia moja ni rahisi nayo ni ya kupitia Ulaya na nyingine ni ngumu na si ya kupitia Ulaya. Njia ya kwanza ni hatari na angamizi kwani itambana na kumuweka mtu katika hali ngumu kwa kuwafanya marafiki zake kuwa dhaifu na maadui wake kuwa na nguvu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Moja ya changamoto nyingine za ndani ya nchi na ambazo ni kosa kubwa sana na la kimsingi ni kule kudhani kwamba kwa kujiweka mbali na misingi ya kiitikadi na usuli za Jamhuri ya Kiislamu, kutapelekea njia zote kufunguka na matatizo yote kutatuliwa.
Vile vile amesema kuwa: Viongozi serikalini ambao ni watumishi wa wananchi, ni watu wenye imani na misingi na usulu za Mapinduzi ya Kiislamu na mimi sina kinyongo nao hata kidogo lakini kati ya maafisa wa serikali kuna baadhi ya watu wanadhani kuwa, kama tutalegeza kamba kwenye misingi na usuli zetu basi milango itafunguka wakati ambapo matunda ya kosa hilo kubwa tumeyaona katika baadhi ya nchi duniani kwenye miaka ya hivi karibuni.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Njia pekee ya maendeleo ya nchi ni kusimama kidete na kushikamana vilivyo na usuli na misingi husika.
Ayatullah Udhma Khamenei ametaja changamoto nyingine ya ndani ya nchi kuwa ni kwamba kuna baadhi ya watu wanadhani kuwa, wananchi wetu watashindwa kuvumilia mashinikizo. Hata hivyo amesema: Iwapo wananchi wataelezwa uhakika wa mambo kwa ukweli unaotakiwa na kwa njia sahihi, basi wananchi hao watasimama imara kulinda maslahi ya nchi yao.
Vile vile amelitaja suala la kuweko hatihati na kutouamini uwezo wa ndani kuwa changamoto nyingine na kuongeza kwamba: Tunapaswa kuwaamini na kuwategemea wasomi na watalaamu wetu vijana pamoja na wananchi wengine katika masuala ya kiuchumi na tutumie vizuri uwezo walio nao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja sharti kuu la kuweza kufanikisha uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete kwamba ni kuwa na azma na nia ya kweli na kujiepusha na kudharau mambo na kupenda mambo mepesi na rahisi pamoja na kutegemea uongozi na uendeshaji mambo wa kijihadi.
Amesisitiza kuwa: Usimamiaji na uendeshaji mambo wa kijihadi una maana ya kutawakali kwa Mwenyezi Mungu na kutumia tadibiri na mantiki na wakati huo huo kufanya kazi kwa bidii na kwa nia ya kweli bila ya kuogopeshwa na mambo ya pembeni pembeni.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kueneza utamaduni sahihi kuhusu uchumi wa kusimama kidete pembeni mwa uongozi na uendeshaji mambo wa kijihadi kuwa ni jambo la dharura na kuongeza kwamba: Shirika la Redio na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB, vyombo vingine vya habari, viongozi, Maimamu wa Sala za Ijumaa na watu wote ambao maneno yao yana taathira kati ya watu wanapaswa kushikiri katika juhudi hizi za kueneza utamaduni wa uchumi wa kusimama kidete.
Aidha amelitaja suala la kubana matumizi, kutumia bidhaa za ndani hususan katika taasisi za serikali, kulipa uzito wa hali ya juu suala la kukabiliana na uingizaji wa bidhaa za nje kiholela na bila ya mantiki, kulipa uzito wa hali ya juu suala la kupambana na magendo, kulipa mazingatio ya kipekee suala la kuvilinda na kuviimarisha viwanda vidogo vidogo na vya kati vya uzalishaji bidhaa na kuziangalia upya siasa za fedha na mfumo wa kibenki kuwa ni katika mambo ya dharura ya kufanikisha siasa za uchumi wa kusimama kidete na kusisitiza kuwa: Sharti kuu la kuweza kufanikisha mambo yote hayo ni kuweko maelewano, masikilizano na kufahamiana pamoja na mshikamano ndani ya nchi.
Vile vile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, watu wote wanapaswa kuisaidia serikali na viongozi nchini katika jitihada za kufanikisha mambo hayo na kuongeza kuwa: Kukuza mambo ya pembeni na yasiyo ya dharura ni jambo lisilokubalika hata likifanywa na mtu yeyote yule na inabidi watu wote wajiepushe na jambo hilo.
Akitoa muhtasari wa miongozo yake kuhusiana na uchumi wa kusimama kidete, Ayatullah Udhma Khamenei amesema: Tunao uwezo wa kufanya mambo makubwa katika masuala ya kiuchumi na kufanikiwa kuvuuka kwa fakhari katika kipindi hiki nyeti.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea na hotuba yake hiyo muhimu sana kwa kuzungumzia suala la nyuklia na kabla ya kutoa ufafanuzi kuhusu baadhi ya mambo ya ndani kabisa ya mazungumzo hayo na kubainisha wazi wazi matakwa na mistari myekundu ya kadhia ya nyuklia, amesisitizia kwanza nukta tatu muhimu.
Nukta ya kwanza ni kwamba, kila anachokisema kwenye vikao vya wazi ndicho hicho hicho anachokisema kwenye vikao vya faragha wakati anapokutana na Rais na viongozi wengine wanaohusika na suala hilo, hivyo madai yoyote yale ya kudai kuna baadhi ya mistari rasmi myekundu inayotajwa katika vikao vya faragha ambayo hivi sasa imewekwa pembeni, si sahini bali ni uongo na ni kinyume kabisa na ukweli wa mambo.
Nukta ya pili iliyobainishwa na Ayatullah Udhma Khamenei katika utangulizi wa matamshi yake muhimu mno kuhusu kadhia ya nyuklia ni sifa za uaminifu, ghera, ushujaa na kushikamana na mafundisho ya dini walizo nazo maafisa wanaounda timu ya Iran ya mazungumzo ya nyuklia.
Amesema, timu hiyo inafanya jitihada kubwa kwa ghera ya kitaifa, kwa uangalifu wa hali ya juu na kwa ajili ya kufungua mafundo yaliyopo pamoja na kufanikisha kazi za nchi mbele ya idadi kubwa ya wafanya mazungumzo wa upande wa pili na kwa hakika timu ya Iran ya mazungumzo ya nyuklia inatetea na kubainisha misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ushujaa mkubwa.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, kama mtu yeyote yule atajua mambo ya ndani kabisa ya mazungumzo hayo, bila ya shaka yoyote atakubaliana na matamshi yake hayo kuhusiana na timu ya mazungumzo ya nyuklia ya Iran. Amesema, inawezekana baadhi ya wakati timu hiyo ikateleza katika kuainisha mambo au katika kutendo jambo fulani, lakini timu hiyo inaundwa na watu walioshikamana vizuri na mafundisho ya dini ya Kiislamu na ni watu wenye ghera na uchungu na nchi yao.
Kundi la nne lililolengwa kwenye nukta za utangulizi zilizogusiwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, ni kundi la watu wanaokosoa mazungumzo ya nyuklia. Kiongozi Muadhamu amesema: Mimi sipingi suala la kuwepo wakosoaji, bali ninalihesabu suala hilo kuwa ni jambo la lazima na linasaidia, lakini kuna uhakika huu usiopingika kwamba kukosoa ni rahisi zaidi kulikoni kutenda, kwani kuona aibu za upande wa pili ni rahisi zaidi, lakini kudiriki na kuelewa tabu na wasiwasi wa upande huo wa pili ni jambo gumu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Matamshi yangu haya yasije yakawa sababu ya kuzuia kuweko wakosoaji, lakini tuzingatie kuwa timu yetu ya mazungumzo ya nyuklia inayaelewa vyema baadhi ya mambo yanayokosolewa, lakini kuna baadhi ya mambo ya dharura yanailazimisha timu hiyo kuchukua baadhi ya hatua ili kuamiliana vizuri zaidi na mazungumzo hayo.
Baada ya hapo, Ayatullah Udhma Khamenei ameanza kuelezea historia fupi ya mchakato wa mazungumzo baina ya Iran na Wamarekani ambapo jambo hilo linasaidia sana katika kuudiriki mchakato wa mazungumzo hayo.
Amesema: Suala la mazungumzo (ya Iran) na Wamarekani lilianza tangu wakati wa serikali iliyopita (ya Iran) ambapo (Wamarekani) walituma mtu Tehran kuja kututaka tufanye mazungumzo nao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ufafanuzi zaidi kuhusu suala hilo akisema: Wakati huo mtu mmoja muheshimiwa katika eneo hili alikuja kuonana nasi na kutueleza wazi wazi kwamba Rais wa Marekani amemuomba aje Tehran na kutujulisha nia ya Wamarekani ya kutaka kufanya mazungumzo na sisi. Wamarekani walimueleza mtu huyo kuwa wanataka – sambamba na kuielewa zaidi Iran kama dola la nyuklia – waweze pia kuitatua kadhia ya nyuklia na kuhakikisha vikwazo dhidi ya Iran vinaondolewa katika kipindi cha miezi sita. Tab’an sisi tulimueleza mtu huyo kuwa hatuwaamini kabisa Wamarekani kama ambavyo hatuna imani kabisa pia na maneno yao. Hata hivyo mtu huyo aling’ang’ania sana suala hilo, hivyo na sisi tukakubali kujaribu tena jambo hilo na wakati huo ndipo yakaanza mazungumzo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbushia nukta mbili muhimu katika mashindano ya kimataifa na kuongeza kuwa: Katika kila mapambano ya kidiplomasia, huwa kuna medani za aina mbili ambazo inabidi zizingatiwe, medani ya kwanza ni medani ya uhakika wa mambo, kazi na uzalishaji wa pato na kwamba maafisa wa masuala ya kidipomasia na kisiasa ndio wanaobadilisha mapato na mali hizo kuwa fursa za kudhamini manufaa ya kitaifa ya nchi husika.
Vile vile amesema: Mkono mtupu wa nchi yoyote ile katika medani ya awali, huibana nchi hiyo na kuikwamisha pamoja na kuipoka nguvu katika medani ya pili na ni kwa kuzingatia mantiki hiyo ndio maana Iran imeingia kwenye mazungumzo ya nyuklia ikiwa na mafanikio makubwa na ikiwa imara na yenye nguvu na mfano wa jambo hilo ni uwezo wa Iran wa kuzalisha asilimia 20 ya fueli nyuklia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbusha kuwa, madola yote ya nyuklia yalikuwa yanakataa kuiuzia Iran asilimia 20 ya fueli nyuklia kwa ajili ya kuzalishia dawa za nishati ya nyuklia kwenye kituo cha nyuklia cha Tehran. Madola hayo yalikwenda mbali zaidi na kufikia hata kuzizuia nchi nyingine zisituuzie mafuta hayo ya nyuklia. Lakini wanasayansi na wataalamu wetu vijana ambao ni fakhari ya Iran wameweza kuzalisha fueli hiyo inayohitajiwa na Iran na kukamilisha mchakato mzima wa fueli nyuklia, jambo ambalo limeushangaza na kuustaajabisha mno upande wa pili.
Ameongeza kuwa: Mbali na kuzalisha fueli nyuklia ya asilimia 20, kuna mafanikio mengine makubwa na ya kimsingi iliyopata Iran katika medani nyinginezo na kwa hakika mkakati wa kusimama kidete Iran katika kukabiliana na mashinikizo imetoa majibu mazuri na kwamba Wamarekani sasa wametambua kuwa, mashinikizo na vikwazo haviwezi kufanikisha mambo wanayoyataka na hawana njia nyingine ila kutafuta mbinu tofauti na hiyo kuamiliana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia namna Iran inavyouangalia upande wa pili wa mazungumzo kwa shaka na wasiwasi mkubwa na kusema: Pamoja na kuwepo jambo hilo, sisi tulisema kwamba, kama Wamarekani wataheshimu matamshi na ahadi zao walizompa kiongozi huyo aliyekuja kuzungumza nasi, sisi pia tuko tayari kujaribu jambo hilo kwa matarijio kuwa mazungumzo hayo yatafanyika chini ya msingi wa mantiki na kwa kuzingatia uhalisia wa mambo, lakini muda mrefu wa mazungumzo hayo haukupita ila tuliona namna Wamarekani walivyoanza kujivutia upande wao kila kitu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia kwamba, makubaliano mazuri kwa mtazamo wa Iran ni makubaliano ya kiuadilifu na yenye insafu na kuongeza kuwa: Wakati mazungumzo yakiendelea, Wamarekani waliibadilisha miezi sita iliyoahidiwa kwa ajili ya kuanza kuondolewa vikwazo vya Iran na kuifanya mwaka na baadaye wakaanza siasa za kujivutia kila kitu upande wao na kuyarefusha mazungumzo hayo na hata kutishia kuiwekea Iran vikwazo vingi zaidi na kutoa pia vitisho vya kijeshi na kudai pia kuwa machaguo yote yako juu ya meza kwa ajili ya kukabiliana na Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei ametoa muhtasari wa namna fulani wa mada hiyo ya mazungumzo akisisitiza kwamba: Mtu anapoutalii na kuuzingatia mchakato wa matakwa ya Wamarekani ataona kuwa lengo lao ni kuiangamiza kikamilifu teknolojia na miradi yote ya nyuklia nchini Iran, kuangamiza kabisa utambulisho wa nyuklia wa Iran na kuugeuza kuwa mwanasesere na kibonzo kisicho na chochote ndani yake.
Vile vile ameashiria namna utafiti wa kina unavyoonesha kuwa Iran inahitajia megawati 20 elfu za umeme utokanao na nishati ya nyuklia na kuongeza kuwa: Mbali na Wamarekani kufanya njama za kuangamiza miradi ya nyuklia na kutaka kuizuia Iran isinufaike na faida nyingi zilizomo kwenye sekta hiyo, wanataka pia kuendeleza kwa namna fulani mashinikizo na vikwazo vyao dhidi ya Iran.
Ameongeza kuwa: Kama Wamarekani wataweza kufikia malengo yao kwenye mazungumzo, basi watakuwa wamepata ushindi mkubwa kwani watakuwa wamelipigisha magoti taifa la Iran linalopigania uhuru na kujitegemea na kuishinda nchi ambayo inaweza kuwa kigezo na ruwaza njema kwa nchi nyingine duniani na kwamba ahadi zote mbaya za Wamarekani na kuzungusha zungusha kwao mambo kunafanyika kwa ajili ya kufanikisha malengo yao hayo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitizia pia matakwa ya kimantiki ya Iran tangu mwanzoni kabisa mwa mazungumzo hayo hadi hivi sasa na kuongeza kuwa: Sisi tangu awali kabisa tulisema kuwa, tunataka mashinikizo na vikwazo vya kidhulma vilivyowekwa dhidi yetu viondolewe, ambapo tab’an katika mkabala wa jambo hilo, tuko tayari kutoa baadhi ya vitu kwa sharti kwamba sekta ya nyuklia nchini Iran isisimame na wala isipate madhara yoyote yale.
Ayatullah Udhma Khamenei ameendelea na hotuba yake kwa kuchora kwa uwazi kabisa mistari myekundu ya nyuklia ya Iran. Amesema kuhusu mstari mwekundu wa kwanza kabisa kwamba: Sisi, tofauti na wanavyong’ang’ania Wamarekani, hatukubaliani na mpaka wa muda mrefu wa miaka 10 na 12 na tayari tumeshawaeleza mpaka wa muda huo tunaoukubali sisi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kuendelea kazi za utafiti na ustawishaji wa miradi ya nyuklia ya Iran hata katika wakati na muda huo wa utekelezaji wa makubaliano yanayotarajiwa, kuwa ni mstari wa pili mwekundu wa Iran na kuongeza kuwa: Wamarekani wanasema tusifanye kazi yoyote katika kipindi chote hicho cha miaka 12 lakini hayo ni maneno ya kibeberu kupindukia na ghalati kupita kiasi.
Akitolea ufafanuzi mstari wa tatu mwekundu wa nyuklia, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kwa kusisitiza kwamba: Vikwazo vya kiuchumi, kifedha na kibenki, viwe ni vile vilivyowekwa na Baraza la Usalama (la Umoja wa Mataifa) au vile vilivyowekwa na Congress ya Marekani au vile vilivyowekwa na serikali ya Marekani, lazima vyote viondolewe mara baada ya kutiwa saini makubaliano na vikwazo vinginevyo viondolewe katika kipindi cha muda unaokubalika.
Vile vile amesema: Wamarekani wanatoa fomula tata, yenye tabaka kadhaa na ya ajabu mno kuhusu vikwazo, na haijulikani kitu gani kitatokea baadaye, lakini sisi tunatangaza waziwazi matakwa yetu bila ya kupindisha maneno.
Ayatullah Udhma Khamenei ameendelea na mada hiyo kuhusu mitari myekundu ya nyuklia ya Iran kwa kusema: Suala la kuondolewa vikwazo halipaswi kushurutishwa na kutekeleza Iran ahadi zake yaani wasije wakasema kuwa, kwanza wewe tekeleza ahadi zako baada ya hapo wakala wa IAEA utoe ripoti ya kuthibitisha kuwa umetekeleza ahadi zako hapo ndio vikwazo viondolewe. Sisi hatuwezi kabisa kukubaliana na suala hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Mchakato wa kuondolewa vikwazo nao inabidi uende sambamba na utekelezaji wa Iran wa ahadi ulizotoa.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amesisitiza kuwa: Sisi tunapinga suala la kuakhirisha utekelezaji wa ahadi za upande wa pili hadi pale wakala wa IAEA utakapotoa ripoti na kuthibitisha kutekeleza Iran ahadi zake kwani wakala huo umethibitisha mara nyingi sana kwamba hauko huru na hauna uadilifu, hivyo sisi tuna mtazamo mbaya kuhusu wakala huo na hatuna imani nao.
Ameongeza kuwa: Wanasema inabidi Wakala upate yakini kuhusu kutekeleza Iran ahadi zake. Maneno gani hayo yasiyoingilika akilini! Vipi inataka kupata yakini? Hivi kwani si wakala huo huo unaofanya ukaguzi wake katika kila kona ya Iran?
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, Iran inakataa na kupinga vikali ukaguzi usio wa kawaida, au kusailiwa shakhsia wa Iran au kukaguliwa maeneo ya kijeshi ya Iran na kulitaja suala hilo kuwa ni mstari mwengine mwekundu wa nyuklia wa Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha kwa uwazi kwamba: Watu wote nchini Iran nikiwemo mimi, Serikali, Bunge, Mahakama na taasisi nyingine za kiusalama na kijeshi na taasisi nyinginezo zote, kila mtu anataka kufikiwe makubaliano mazuri, makubaliano ambayo yatalinda heshima ya Iran, yatakuwa ya kiinsafu na kiuadilifu na yatakayoendana na maslani na manufaa ya Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Ijapokuwa tunapigania kuondolewa vikwazo, lakini katika upande fulani tunavihesabu vikwazo kuwa ni fursa nzuri kwetu kwani vimetufanya tuzingatie zaidi nguvu na uwezo wetu wa ndani.
Aidha mwanzoni mwa hotuba yake Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitizia wajibu wa kuzitumia vizuri baraka za mwezi Mtukufu wa Ramadhani hususan faida zilizomo kwenye dua za mwezi huu na maana zake pana na kusema: Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni mwezi wa khushuu na unyenyekevu, ni mwezi wa istighfari na kurejea kwa Mwenyezi Mungu na ni mwezi wa kujijenga kiimani na kimaadili na kuitakasa nafsi.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam Walmuslimin Rouhani, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa hotuba fupi na ndani yake ameshiria kuanza kazi za Serikali ya 11 ya Iran miezi 22 iliyopita na kuutaja mkakati wa serikali yake katika masuala ya ndani kuwa ni kuleta kuaminiana, miamala ya amani, kupunguza mianya baina ya matabaka ya wananchi na kujiweka mbali na misimamo mikali na ya kufurutu ada.
Vile vile amesema: Msimamo wa serikali yake katika siasa za nje ni kuamiliana kwa njia bora na mataifa mengine duniani kwa kuchunga mstari mwekundu ambao ni kulinda uhuru, heshima na ghera ya taifa la Iran na katika upande wa masuala ya kiutamaduni ni kuandaa mazingira yaliyo wazi kwa watu wote wanaohusiana na masuala ya kiutamaduni na sanaa sambamba na kuchunga mstari mwekundi wa kimaadili na wa hukumu za dini tukufu ya Kiislamu.
Rais Rouhani amesema kuwa, suala la kutatuliwa kadhia ya mazungumzo ya nyuklia katika kalibu ya kufanikisha haki za nyuklia za Iran na kudhamini mahitaji yake ya kijamii ni vipaumbele viwili vikuu vya serikali yake na kuongeza kuwa: Jambo ambalo limeyalazimisha madola makubwa kuja kwenye meza ya mazungumzo ni muqawama na kusimama kidete taifa la Iran mbele ya mashinikizo ya wanaolitakia mabaya taifa hili na kufanikiwa taifa la Iran kuvishinda vikwazo vya watu hao.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa, kamwe vikwazo havitafanikiwa kufikia malengo yake na kwamba hata kama vikwazo vitaendelea kuwepo, taifa Iran litaweza kuendesha vizuri na kutatua masuala yake yote ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni na kuongeza kuwa: Tumefanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei kwa msaada wa wananchi licha ya kuwa vikwazo dhidi ya nchi yetu bado vipo na tumefanikiwa kutoka katika uzorotaji wa kiuchumi na kukuza uwekezaji licha ya kwamba bado tumo ndani ya vikwazo.
Rais Rouhani amelitaja suala la kuongezeka akiba ya bidhaa za kiistratijia, kuondoa vizuizi vya kusafirisha nje bidhaa, kuwasilisha mkakati wa kutoka kwenye uzorotaji wa uchumi, kupunguza kiwango cha bidhaa zinazoagiziwa kutoka nje ya nchi, kubadilisha kigezo cha ukulima na upandaji mimea, kupanua wigo wa huduma za tiba, kuwasaidia wananchi wa matabaka ya kipato cha chini na kutoa ruzuku kwa ajili ya bidhaa, kupungua utegemezi wa mafuta katika bajeti, kubana matumizi katika mambo mbali mbali, kufungua viwanda elfu nane vya uzalishaji wa bidhaa za kila namna na kupigwa hatua nzuri katika masuala ya kulinda mazingira kuwa ni miongoni mwa hatua za maendeleo zilizopigwa na serikali yake licha ya Iran kuwa bado imo ndani ya vikwazo.
Rais Rouhani amelitaja suala la kupunguza serikali utegemezi wa pato litokanalo na mafuta kuwa ni hatua muhimu mno iliyochukuliwa na serikali mwaka huu na kuongeza kuwa: Ni lazima kufanyike bidii na jitihada kubwa zaidi za kujiletea maendeleo sambamba na kulindwa umoja, mshikamano na maelewano ili tuweze kuvuuka vizuri kwenye kipindi cha matatizo na kwamba jambo hilo halitowezekana bila ya kuweko msaada wa wananchi.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza pia kuwa, hatupaswi kuruhusu kutokea mivutano isiyo ya lazima katika jamii hususan kwenye kipindi hiki nyeti na muhimu. Amesema, kama upande wa pili wa mazungumzo ya nyuklia utaachana na siasa zake za kujivutia kila kitu upande wake, basi kuna uwezekano mkubwa wa kufikia makubaliano na kuvuuka vizuri kwenye kipindi hiki muhimu cha historia.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake hiyo, Rais Hassan Rouhani amebainisha kuwa, mataifa ya eneo la Mashariki ya Kati leo hii yako chini ya mashinikizo makubwa sana kutokana na uingiliaji wa baadhi ya nchi na makundi ya kigaidi kwenye masuala ya eneo hili na kuongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko mstari wa mbele katika kupambana na ugaidi na kuyaunga mkono mataifa ya eneo hili suala ambalo amesema, Iran itaendelea nalo.

 

About Asadiq Media

Media for publicise the message of Wilaya under Imam Swadiq

Posted on June 29, 2015, in Uncategorized. Bookmark the permalink. Leave a comment.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Elijah J. Magnier

Middle East Politics

elbinawi

To interact with humanity & share ideas...

felicity114

felicity is the purpose of everybody

Ladakh Express

Ladakh's 1st political and cultural online journal.

Islamic Library

Shia Islamic PDFs - Now in Collaboration with ShiaTranslate.org!

zahraa Foundation

Fatima bint Muhammad is the Symbolization of Women's Power in Islam

mmubaraka1

A fine WordPress.com site

Pilgrim Center of Hope

Catholic Evangelization Ministry

World Shia Forum

Identity, Equality, Unity

Source of Inspiration

All is One, co-creating with the Creator

Bill Langill's Blog

Love is the Answer

Interrupting the Silence

An Episcopal Priest's Sermons, Prayers, and Reflections on Life, Becoming Human, and Discovering Our Divinity

Morgan L. Busse

In Darkness there is Light

YOGA

When unconscious became conscious this is Samadhi

Zoroastrians.net

Parsis, Iranis, Zarathushtis, All Under One Roof

Islamic Laws

Raising Awareness on Fiqh and the Ulema

Tech Cloud

Imagine | Innovate | Implement

Mujtaba Somji

Islamic sayings

%d bloggers like this: