MAANA SAHIHI YA ITIKADI YA KUMSUBIRI IMAM MAHDI (AS) (MAHADAWIYYAT)

image

Shaban_15: Tunatoa mkono wa Pongezi na Hongera kwa Wanaadamu wote kwa kuzaliwa Muokozi Imam Mahdi (Aharakishe mwenyezi mungu kudhihiri kwake)

MAANA SAHIHI YA ITIKADI YA KUMSUBIRI IMAM MAHDI (AS) (MAHADAWIYYAT)

Leo ni Shaabn 15 siku kama ya leo mwaka 255 Hijiria alizaliwa Imamu wa 12 wa watu wa nyumba ya Mtume (saw). Jina lake kamili ni Muhamad, lakini majina yake mengine ni Mahdi, Sahib uz Zaman. Al-Hujjah, baba yake alikuwa Imamu wa 11 Imam Hassan al-Askari (as) na Mama yake alikuwa Nargis Khatoon. Suala la Itikadi ya Imam mahd limekuwa likizua utata mkubwa sana baina ya Madhehebu ya waislamu duniani.

Leo katika kusherehekea kuzaliwa Imam Mahd (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake) tumekusudia kueleza kwa ufasaha maana halisi na sahihi ya Itikadi ya kumsubiri Imam Mahd (as). Tutajibu sintofamu kuwa kumsubiri Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake) ni kubweteka na kukaa kiuzembe bila kufanya harakati tukimsubiri muokozi huyu kuja kutukomboa, pia tutafafanua na kuweka wazi kauli zisemazo kuwa Mahd muokozi yupo pangoni na baadhi ya viongozi wa irani humtembelea na kuwapa muongozo.
Makala haya yamechukua sehemu kubwa ya fikra na maelezo kutoka katka Hotuba ya Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyoitoa mbele ya hadhara ya Wahadhiri, Wasomi, Watunzi na Watu Waliohitimu Masomo ya “Mahdawiyaat” (itikadi kuhusu Imam Mahdi).

Amma suala la Mahdawiyyat (yaaani itikadi juu ya Imam Mahdi AS) katika masiku haya kwa mnasaba wa kumbukumbu ya tarehe 15 Shaabani na sikukuu kubwa ya Kiislamu – bali ya wanaadamu wote – ni mahala pake kuzungumzia suala hili, tunapaswa kusema kwa kiwango hiki kwamba, suala la Mahdawiyyat liko katika faharasa ya masuala kadhaa ya kimsingi na silsila ya maarifa muhimu ya kidini;

Kama lilivyo suala la Utume, inapaswa kulitambua suala la Mahdawiyyat katika daraja ya umuhimu huu. Kwa nini? Kwa sababu kile kitu ambacho kinabashiriwa na Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake) ni kile kile kitu ambacho kililetwa na Manabii wote ambao walibaathiwa kwa ajili ya jambo hili nalo ni kuufanya ulimwengu kuwa ni wa tauhidi na kuhakikisha uadilifu unatawala katika jamii kwa kutumia vipawa vyote ambavyo Mwenyezi Mungu amempatia mwanaadamu; kipindi cha kuja na kudhihiri Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake) ni duru ya namna hii.

Kipindi cha kudhihiri Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake) ni duru ya jamii ya tauhidi, zama za utawala wa tauhidi, kipindi cha utawala wa kweli wa umaanawi na dini katika nyanja zote za maisha ya wanaadamu na ni duru ya kuweko uadilifu kwa maana kamili na halisi ya neno. Vizuri, Manabii wa Mwenyezi Mungu walibaathiwa na kutumwa kwa ajili ya lengo hili.

Sisi tumesema mara kadhaa kwamba, harakati zote zilizofanywa na mwanaadamu ziko katika kivuli cha mafundisho ya Manaabii katika kipindi cha karne zote, zilikuwa ni harakati za kuelekea upande wa bararaba pana ya kipindi cha Mtukufu Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake) ambacho ni kipindi cha kuelekea katika malengo muhimu ambayo mwanaadamu anataka kuyafikia kupitia barabara hiyo. Ni kama vile watu walioko msituni na katika njia ngumu ambao wanafanya harakati kwa muongozo wa watu fulani ambao wanafahamu njia; lengo la watu hao ni kuhakikisha kwamba, wanatokea katika njia kuu.

Wakati wanapofika katika njia kuu, hupata njia ikiwa wazi mbele yao, kuna njia iliyonyooka na ya wazi; hivyo kutembea na kufaanya harakati wakati huo kwao litakuwa ni jambo jepesi; wataweza kufanya harakati na kusonga mbele kwa wepesi zaidi kwani mbele yao kuna njia ya wazi na iliyonyooka. Na sio kwamba wanapofika katika njia na barabara kuu wasimame na kutofanya harakati; hapana, kimsingi ni kuwa, wanapofika hapo ndio kwanza harakati ya kuelekea katika malengo makuu na muhimu huanza; kwani uwezo wa mwanaadamu ni uwezo usiokwisha. Katika kipindi cha karne zote hizi, mwanaadaamu alifanya harakati katika njia zilizopinda, alifanya harakati bila ya kuwa na njia, au alifanya harakati katika njia ngumu huku akikabiliwa na vizingizi tofauti na huku mwili wake ukitaabika kwa majeraha na maumivu.

Hata hivyo alifanya harakati katika mazingira hayo ili aweze kufika katika barabara kuu. Barabara hii kuu ndio ile njia na kipindi cha kudhihiri Imam Mahdi Baqiyatullah (roho zetu ziwe fidia kwake); ndio kile kipindi cha kudhihiri mwokozi wa ulimwengu ambacho kimsingi ni kipindi cha kuanza harakati ya kweli ya mwaanadamu. Kama “Mahdawiyyat” na imani kuhusu Imam Mahdi isingelikuwepo, basi juhudi na jitihada zote za Manabii, harakati zote za da’awa (kuwalingania watu), kubaathiwa Mitume (Alayhims Salaam) na idili pamoja na juhudi kubwa zilizofanywa na waja wateule wa Mwenyezi Mungu (Mitume) zisingelikuwa na faida wala taathira yoyote.

Hivyo basi suala la Mahdawiyyat yaani itikadi juu ya Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake) ni moja ya masuala ya kimsingi; ni miongoni mwa maarifa ya kimsingi ya Mwenyezi Mungu. Ndio maana katika dini zote za Mwenyezi Mungu kuna imani ya kudhihiri Imam Mahdi AS japo ni kiujumla mno, lakini katika Uislamu jambo hilo ni katika itikadi zisizo na shaka hata kidogo ; amma kati ya madhehebu za Kiislamu pia, Waislamu wa madhehebu ya Kishia wanalichukulia suala la “Mahdawiyyat” (kuwa na imani ya Imam Mahdi AS) kwa uzito wa hali ya juu wakilitekeleza wazi kivitendo na kulipa nafasi kubwa katika maisha ya familia na shakhsia za watu wenye kusubiri kudhihiri Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake); jambo ambalo limethibitishwa pia katika hadithi zenye itibari na ushahidi madhubuti wa Waislamu wa madhehebu ya Kishia na wasio Waislamu wa Kishia.

Hivyo basi itikadi kuhusiana na Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake) sio makhsusi kwa Waislamu wa madhehebu ya Kishia tu, hapana. Bali madhehebu yote ya Kiislamu yanakubaliana na suala la kusimamisha utawala wa haki na kiadilifu kazi ambayo itafanywa na Imam Mahdi (Baqiyyatullah katika ardhi) pindi atakadhihiri na kuja kuujaza ulimwenguuadilifu na usawa baada ya kuwa umejaa dhulma na uonevu. Hivyo hakuna shaka yoyote kuhusiana na jambo hilo hasa kutokana na kuthibitishwa na riwaya mbalimbai zenye itibari.

Kwa upande wa Waislamu wa madhehebu ya Kishia kwao wao hili ni jambo ambalo liko wadhiha. Yaani sisi Mashia tunafahamu jambo hili kwa undani, sifa za Imam Mahdi, baba zake, familia yake, tarehe ya kuzaliwa kwake na tunafahamu mambo ya ndani yanayomhusu Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake) mwokozi wa ulimwengu. Katika maarifa haya pia sio riwaya zilizopokelewa na upande wa Mashia tu ndizo zinazobainisha na kuthibitisha hili; hapana, bali kuna riwaya na hadithi zilizopokelwa na wasiokuwa Mashia ambazo zinabainisha na kuweka wazi maarifa haya na ni lazima kwa watu wa madhehebu mengine kuwa makini na wawe ni wenye kuzingatia mambo ili waweze kuufahamu na kuudiriki uhakika na ukweli huu.

Hivyo basi, umuhimu wa suala hili uko katika daraja hii na sisi tunapaswa kujihusisha na suala hili kuliko watu wengine; kuna ulazima wa kufanyika kazi za kielimu, makini na zenye thamani katika suala hili. Suala la kusubiri kudhihiri Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake) ni uhakika usiotenganishika na “Mahdawiyyat” (itikadi kuhusu Imam Mahdi) na ni miongoni funguo kuu za kufahamu dini, harakati ya kimsingi, jumla na ya kijamii ya umma wa Kiislamu kuelekea katika malengo muhimu na matukufu ya Kiislamu; Maana ya kusubiri kudhihiri Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake) ni kusubiri kwa hamu kudhihiri mtu aliye hai na kungojea kudhihirika uhakika usio na shaka hata kidogo.

Maana hii ya kusubiri ina na mahitaji yake ya lazima yaani mambo ya lazima ambayo yanapaswa kufanywa, ambapo miongoni mwa mahitaji hayo ya lazima ni kujiweka tayari kiroho na batini ya mtu na pia jamii nzima ya mwanaadamu kwa minajili ya kuingia kwenye kipindi hicho kinachosubiriwa kutokea, na mazingira maalumu ya kipekee yatakayoambatana na kipindi hicho. Na sio watu waseme kwamba, atazaliwa mtu na atakuja mtu; hapana, bali mtu huyu msubiriwa yupo baina ya watu.

Katika riwaya imekuja kwamba, watu wanamuona kama ambavyo yeye anawaona watu; isipokuwa watu hawamjui lakini yupo baina yao. Katika riwaya jambo hilo limeshabihishwa na kadhia ya Nabii Yusuf AS na nduguze ambapo ndugu zake walikuwa wakimuona, alikuwa baina yao, kando yao, walikuwa wakitembea juu ya busati lake lakini walikuwa hawamjui. Ni hakika ya namna hii iliyo wazi, wadhiha na ya kustaajabisha; hii inasaidia maana ya kusubiri. Mwanaadamu anahitajia kusubiri huku; amma umma wa Kiislamu wenyewe unahitajia zaidi hili. Kusubiri huku ni taklifu na jukumu ambalo liko katika mabega ya mtu. Wakati huo mtu huwa na yakini na mustakabali kama huu; kama ambavyo Mwenyezi Mungu anasema katika kitabu chake kitakatifu cha Qur’ani kwamba:
“Na hakika tulikwisha andika katika Zaburi baada ya Kumbukumbu, ya kwamba nchi watairithi waja wangu walio wema. Hakika katika haya yapo mawaidha kwa watu wafanyao ibada.” (al-Anbiyaa 21:105-106).

Hivyo haya yanafahamiwa na watu wafanyao ibada na kwa muktadha huo wanapaswa kujiandaa na ni lazima wawe ni wenye kusubiri. Kuhusiana na suala la kusubiri kamwe haipaswi kufikiria kwamba, kutatokea baada ya kupita muda mrefu na kwa upande mwingine kamwe haipaswi kudhani kuwa kutokea kwake kuko karibu mno. Daima mtu anapaswa kuwa ni mwenye kusubiri. Mtu mwenye kusubiri na kutegemea kutokea kitu fulani, basi wakati wote anapaswa kujipamba kwa sifa maalumu anazotakiwa kuwa nazo wakati wa kipindi cha kudhihiri anachokitarajia.

Kuna sifa maalumu za kipindi cha kudhihiri Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake). Kipindi cha kudhihiri mtukufu huyo ni kipindi cha utawala wa tauhidi, uadilifu, haki, ikhlasi na ibada ya Mwenyezi Mungu Mmoja, hivyo watu wanaosubiri kudhihiri kipindi hicho nao wanapaswa wakati wote kufanya hima ya kujikurubisha kwenye sifa hizo maalumu na wasitosheke na hali waliyo nayo. Wakati inapokuwa kwamba tunasubiri kuja kutokea kipindi cha uadilifu, haki, tauhidi, ikhlasi na kumuabudu Mwenyezi Mungu, sisi ambao ni wenye kusuburi, tunapaswa kujikurubisha na mambo haya, tunapaswa kufahamu uadilifu na hivyo tujiandae kuipokea haki. Kusubiri kunaleta hali kama hii.

Moja ya sifa za kusubiri ni kwamba, mtu hapaswi kuridhika na hali ya maendeleo iliyopatikana leo; bali anatakiwa atake maendeleo zaidi yapatikane siku baada ya siku hasa katika jamii yake hususan katika kufahamika uhakika, umaanawi na maarifa juu ya Mwenyezi Mungu. Haya ni mambo ya lazima katika hali ya kusubiri.

Vizuri, Alhamdulilahi leo kuna watu ambao wanafanya kazi katika suala la kusubiri tena kwa njia ya kielimu; Kwa hakika kuna udharua wa kufanya kazi za kitaalamu, za kina na zenye ushahidi thabiti na haipaswi kughafilika na hilo. Aidha kuna haja ya kujiepusha na kazi za kiuwanagenzi, zisizo za kielimu, zisizo na ushahidi imara na madhubuti na zinazotegemea mawazo na fikra zisizo na mashiko.

Kwa hakika moja ya hatari kubwa katika kadhia ya “Mahdawiyyat” ni kazi za kiuwanagenzi, zisizo za kielimu, ambazo zinaandaa uwanja wa kudhihiri watu waongo wanaodai Uimamu wa Mahdi ambao wanawakanganya na kuwapotosha watu wanaosubiri kikweli kweli kudhihiri Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake).
Katika kipindi chote cha historia kulijitokeza watu mbali mbali wakiwa na madai ya uongo ya Uimamu wa Imam Mahdi AS wakijinasibisha na baadhi ya alama za kudhihiri mtukufu huyo au kuwanasibisha watu wengine na alama na dalili hizo. Ni dhahiri shahiri kwamba, mambo yote haya si sahihi na ni upotofu; kwani baadhi ya masuala yanayodaiwa kuwa ni dalili na alama za kudhihiri Imam Mahdi AS si za kutegemewa, ni dhaifu na ni vigumu mtu kuzitabikisha na masuala yenye itibari yanayohusiana na jambo hilo.

Masuala kama haya yasiyo sahihi na ya upotofu, hupelekea kuguriwa uhakika halisi wa “Mahdawiyyat” na uhakika wa kusubiri kudhihiri Imam Mahdi AS, hivyo inabidi kujiepusha kikamilifu na kazi zenye kutegemea uvumi usio na mashiko wala misingi yoyote. Hata katika mambo ambayo yana mashiko, sio kwamba, ni rahisi kutabikisha alama hizo. Daima kuna watu mbalimbali katika karne tofauti walitabikisha mashairi ya Shah Neematullah – katika kipindi cha miaka mingi na katika mambo mengi – kwa watu mbalimbali katika karne tofauti, ambapo hili mimi nimeliona.

Walijitokeza na kusema, hii kwamba imeelezwa mtu fulani, basi mtu huyo ni huyu; wakaja na kumtaja mtu fulani wakimnasibisha na kumtabikisha sifa za Imam Mahdi AS zilizotajwa.

Kisha katika kipindi kingine, cha baada ya miaka mia moja kwa mfano, wakampata mtu mwingine na kumtabikisha na sifa hizo! Haya ni mambo yasiyo sahihi hizi ni kazi za kipotofu na za upotoshaji. Wakati upotofu na jambo lisilo sahihi linapojitokeza, wakati huo hakika na ukweli huhajiri na kugura, huingiwa na shubha na hivyo hupatikana wenzo wa kuwaposha watu.

Kwa muktadha huo kuna ulazima mno wa kujiepusha na kazi za kijahili, ambazo hazijakomaa kifikra na zisizo na mashiko ya kielimu na hivyo kutosalimu amri mbele ya uvumi wa kijinga. Hapana shaka kuwa, kazi za kielimu na zenye ushahidi thabiti kuhusu maudhui ya “Mahdawiyyat” na kusubiri kudhihiri Imam Mahdi AS ni jukumu la wataalamu na watu wa fani hiyo ambao wamebobea kielimu katika uga wa elimu ya hadithi na ilmu-rrijaal (elimu zinazohusiana na wapokezi wa hadithi na usahihi wa hadithi za maasumu) na ambao pia wana uwelewa kuhusu masuala ya fikra za kifalsafa. Hivyo watu hawa ndio wanaopaswa kufahamu uhakika na wakati huo wanaweza kuingia katika uga na medani hii na hivyo kufanya kazi ya uhakiki na utafiti katika uga huu.

Wigo wa Uga wa kazi hii unapaswa kuongezwa zaidi kadiri inavyowezekana ili Inshallah, njia iwafungikie watu; kadiri nyoyo zitakavyokuwa na ufahamu kuhusiana na Mahdawiyyat yaani itikadi juu ya Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake), zikaathirika na mtukufu huyo na mtukufu huyo akawa katika nyoyo zetu katika kipindi hiki cha kughibu (ghaiba) kwake, bila shaka tutazidi kumhisi zaidi na tutakuwa na mawasiliano naye zaidi na kwa msingi huo ile harakati yetu ya kuelekea upande wa malengo muhimu katika dunia yetu hii na kwa ajili ya maendeleo itakuwa bora zaidi na zaidi. Huku kutawasali kwa aina tofauti kunakopatikana katika ziara ambapo baadhi yake kuna hoja nzuri, kwa hakika haya ni mambo ambayo yana thamani mno.

Njia ya kweli ni njia ya kimantiki. Kitu kilicho sahihi na kinachotakiwa katika suala la kuwa na ukuruba na mapenzi makubwa na mtukufu huyo (Imam Mahdi) pamoja na kutawasali kwa jina lake, ni kuzingatia na kutawasali kwa njia ya mbali na ya ghaibu na Inshaallah Imam Mahdi AS analikubali jambo hilo, lakini kuna baadhi ya madai ya uongo na masuala ya kiuwanagenzi yanayohusishwa na kuwa na mfungamano na ukuruba na mtukufu huyo kupitia kuonana naye uso kwa uso madai ambayo aghlabu yake ni uongo na yanayotokana na dhana zisizo na mashiko wala msingi wowote ule.
Mwenyezi Mungu Mtukufu anafikisha salamu za wasailimiaji na ujumbe wa watoaji ujumbe kwa mtukufu Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri wake). Kutawasali na kujirubisha huku kwa kimaanawi ni jambo zuri na la lazima.

Tuna matarajio kwamba, Mwenyezi Mungu atakufanya kudhihiri kwa Baqiyatullah Imam Mahdi (roho zetu ziwe fidia kwake) kuwe karibu na atatufanya sisi kuwa miongoni mwa masahaba na wafuasi (wa kweli) wamtukufu huyo, katika ghaiba yake na katika kipindi cha kudhihiri kwake; na Inshallah tutakuwa miongoni mwa mujahidina (wa kweli) watakaokuwa pamoja na Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake) na watakaouawa shahidi wakiwa pamoja na mwokozi huyo wa ulimwengu.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

About Asadiq Media

Media for publicise the message of Wilaya under Imam Swadiq

Posted on May 22, 2016, in Uncategorized. Bookmark the permalink. Leave a comment.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Elijah J. Magnier

Middle East Politics

elbinawi

To interact with humanity & share ideas...

felicity114

felicity is the purpose of everybody

Ladakh Express

Ladakh's 1st political and cultural online journal.

Islamic Library

Shia Islamic PDFs - Now in Collaboration with ShiaTranslate.org!

zahraa Foundation

Fatima bint Muhammad is the Symbolization of Women's Power in Islam

mmubaraka1

A fine WordPress.com site

Pilgrim Center of Hope

Catholic Evangelization Ministry

World Shia Forum

Identity, Equality, Unity

Source of Inspiration

All is One, co-creating with the Creator

Bill Langill's Blog

Love is the Answer

Interrupting the Silence

An Episcopal Priest's Sermons, Prayers, and Reflections on Life, Becoming Human, and Discovering Our Divinity

Morgan L. Busse

In Darkness there is Light

YOGA

When unconscious became conscious this is Samadhi

Zoroastrians.net

Parsis, Iranis, Zarathushtis, All Under One Roof

Islamic Laws

Raising Awareness on Fiqh and the Ulema

Tech Cloud

Imagine | Innovate | Implement

Mujtaba Somji

Islamic sayings

%d bloggers like this: