Mjue Imam Ruhullah al-Musawi al-Khomeini

Imam Ruhullah al-Musawi al-Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu), mwasisi na mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, alizaliwa tarehe 20 Jamadi Thani (Mfungo Tisa) mwaka 1320 Hijria, mwafaka na tarehe 24 Septemba mwaka 1902 Miladia.

ayatollah-ruhollah-khomeini-13680544-1-402.jpg

Alizaliwa katika mji wa Khomein moja ya viunga vya Mkoa wa Kati nchini Iran. Imam Alizaliwa katika familia ya wasomi, wahajiri na wajahidi katika kizazi cha Mtukufu Fatima AS binti wa Bwana Mtume SAW. Alirithi tabia njema kutoka kwa baba na mababu zake ambao kwa hakika walitumia sehemu kubwa ya umri wao kujifunza maarifa juu ya Mwenyezi Mungu na kuwaongoza watu katika njia ya haki.

Baba mtukufu wa Imam Khomeini, marehemu Ayatullah Sayyid Mustafa Musawi aliishi katika zama za akina marehemu Ayatullah Udhma Mirza Shirazi ambaye baada ya kusoma kwa miaka mingi katika Hawza (chuo kikuu cha kidini) ya Najaf al-Ashraf nchini Iraq na kupata shahada ya ijtihadi (na kuwa mujtahidi), alirejea nchini Iran. Akiwa mjini Khomein, Ayatullah Mustafa Musawi alikuwa ni marejeo ya watu kutaaradhia shida zao na kuwaongoza katika mambo mbalimbali ya dini. Imam Khomeini alikuwa na umri wa miezi isiyozidi mitano wakati madhalimu na makabaila waliokuwa wakiungwa mkono wa utawala wa kidhalimu wa wakati huo nchini Iran waliukabili wito wake wa kulingania haki na kusimama dhidi ya dhulma kwa kumpiga risasi na kumuua shahidi akiwa njiani kuelekea Arak kutokea Khomein. Jamaa wa shahidi Ayatullah Mustafa walielekea Tehran ili kuhakikisha uadilifu unatendeka na waliotenda mauaji hayo wanahukumiwa kwa mujibu wa sheria kwa kutekelezwa hukumu ya kisasi dhidi yao.

Kwa utaratibu huo, Imam Khomeini alianza kuonja ladha ya uyatima tangu akiwa mtoto mdogo na kujua maana ya kufa shahidi. Utotoni na uchipukizini mwake alilelewa na mama yake muumini, Bibi Hajar ambaye alitoka katika ukoo wa elimu na takwa na alikuwa katika wajukuu wa Ayatullah Khonsari (mtungaji wa kitabu kiitwacho Zubdatu ‘t-Tasanif). Vilevile alilelewa na shangazi yake, Bibi Sahiba ambaye kwa hakika aliondokea kuwa mwanamke shujaa na mwenye kutetea haki. Lakini alipofikisha umri wa miaka 15 aliwapoteza mama na shangazi yake waliofariki dunia na kumuacha peke yake.

Kuhajiri, Kumaliza Masomo na Kufundisha Mjini Qum

Kitambo kidogo tu baada ya kugura al-Haj Sheikh Abdul Karim Hairi Yazdi (katika mwaka mpya wa Kiarani wa 1300 mwafaka na mwezi wa Rajab 1340), Imam Khomeini alikata shauri na kuelekea mjini Qum na kujiunga katika Hawza. Alifanikiwa kukamilisha kwa haraka viwango vya elimu za Hawza kupitia maustadhi wa Hawza. Alijifunza kitabu cha mwisho cha Mutawwal (kuhusu elimu ya balagha) kwa marehemu Agha Mirza Muhammad Ali Abid Tehrani na masomo ya kati (sat’h) kwa marehemu Ayatullah Sayyid Muhammad Taqi Khonsari, na zaidi alisoma masomo hayo kwa marehemu Ayatullah Sayyid Ali Yathribi Kashani. Hao ni baadhi ya maustadhi wake (Mwenyezi Mungu awe radhi nao). Aidha alisoma masomo ya fikihi na usuli kwa mwasisi na mkuu wa Hawza ya Qum – Ayatullah Abdul Karim Hairi Yazdi.

Baada ya kuaga dunia Ayatullah Udhma Hairi, jitihada za Imam Khomeini na kundi la mujtahidi wa Hawza ya Qum zilizaa matunda, na Ayatullah Burujerdi akaelekea Qum na kuwa mkuu na kiongozi mpya wa Hawza ya Qum. Katika kipindi hicho, Imam Khomeini alikuwa akitambulikana kama mmoja wa wadarisi (waalimu) na mujtahidi mwenye kutoa fatwa na kuwa rai katika elimu za fikihi, usuli, falsafa, irfani na maadili (akhlaq). Katika kipindi cha miaka mingi katika Hawza ya Qum, Mtukufu Imam alifanya hima kubwa kufundisha mifululizo kadhaa ya darsa za fikihi, usuli, falsafa, irfani na maadili ya Kiislamu katika Madrasa ya Faydhiyyah, Msikiti wa A’dham, Msikiti wa Muhammadiyyah, Madrasa ya Haj Mulla Sadiq, Msikiti wa Salmasi, n.k. Fauka ya hayo, Imam alifundisha maarifa ya Ahlul Bait na fikihi katika kwango cha juu kabisa cha mosomo ya Hawza ya Najaf nchini Iraq kwa karibu na miaka 14 katika Msikiti wa Sheikh Adham Ansari. Ni katika kipindi hicho ndipo kwa mara ya kwanza kuzungumzia kuhusu misingi ya nadharia ya utawala wa Kiislamu katika mfululizo wa darsa zake za Utawala wa Fakihi (wilayat-e faqih).

Imam Khomeini katika Kitovu cha Harakati na Mapambano

Moyo wa mapambano na jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu ulikuwa na msingi unaotokana na mtazamo wa kiitikadi, kimalezi na mazingira ya kifamilia; na hali ya kisiasa na kijamii ndiyo iliyotawala katika kipindi chote cha maisha yake ya Imam Khomeini. Alianza harakati zake za mapambano tangu akiwa katika rika la ujana, na hali hiyo kuchukua mkondo wa kukamilika kulingana na vipengee vya kiroho na kielimu kwa upande mmoja, na mazingira pamoja na hali ya kisiasa na kijamii nchini Iran kwa upande mwingine. Katika miaka ya 1961 na 1962, tukio la kupendekezwa muswada wa kubadilishwa sheria za uchaguzi wa serikali za majimbo na wilaya ilikuwa fursa nzuri kwake ya kuwa na nafasi muhimu katika kuongoza harakati za maulamaa. Kwa utaratibu huo, harakati za maulamaa na wananchi nchi kote zilizotekea tarehe 5 Juni 1963 zilikuwa na sifa mbili maalumu: Mosi, uongozi mmoja (mutlaki) wa Imam Khomeini; na pili, kuwa na malengo na mwelekeo wa Kiislamu kwa msukumo, nara na kauli mbiu. Kwa hakika, hiyo ilikuwa mwanzo wa kufunguliwa ukurasa mpya wa mapambano ya taifa la Iran, mapambano ambayo yalikuja kujulikana ulimwenguni kwa jina la Mapinduzi ya Kiislamu. Imam Khomeini anaelezea baadhi ya kumbukumbu za Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia wakati akiwa na umri wa miaka 12.

‘‘Bado nakumbuka vita vyote vikuu vya kwanza na vya pili vya dunia….. Nilikuwa mdogo lakini nilikuwa nikienda skuli na nilikuwa nikiwaona askari wa Umoja wa Sovieti katika makao makuu ya mji wetu wa Khomein. Kwa hakika nilikuwa nikiona jinsi tukivamiwa na kushambuliwa katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia.”

Katika sehemu ya masimulizi yake mengine, Imam Khomeini amewataja baadhi ya makabaila na waasi madhalimu ambao wakiwa chini ya himaya ya serikali, walikuwa wakipora mali za raia na kuvunja heshima za watu, na akasema:

“Kwa hakika mimi nilikuwa katika vita tangu nikiwa mdogo…. Tulikuwa tukishambuliwa na akina Mazalaqi na Rajabali. Sisi wenyewe tulikuwa na bunduki na mimi nikiwa na umri wa miaka takriban 12 – labda mwanzoni mwa kubaleghe kwangu, nilikuwa mtoto – tulikuwa tukipiga duru katika mahandaki ya mitaa yetu ili kujikinga na mashambulio ya waporaji hao.”

Mapinduzi ya kijeshi ya Reza Shah mnamo tarehe 22 Februari 1920 ambayo kwa mujibu wa nyaraka na ushahidi wa kihistoria na usioweza kukanushika yalipangwa na kufanywa kwa himaya ya Waingereza, licha yakuwa yalihitimisha usultani wa (ukoo wa) Qajari na kwa kiwango fulani kukomesha pia utawala wa machifu makabaila na kuwabana waasi waliokuwa wameenea kila mahali nchini, lakini badala yake (Reza Shah) alianzisha udikteta uliokuja kufanya dhulma kubwa zaidi na koo elfu moja chini ya himaya ya udikteta wake zilikuwa na amri juu ya wananchi wanyonge wa Iran. Kuanzia hapo, ukoo wa Kipahlavi peke yake ukachukua nafasi ya zamani ya makabaila na waasi. Katika mazingira kama hayo, ingawa baada ya mapambano ya Mashrutiyyah (ya kupigania kuwepo utawala wa kikatiba nchini) harakati za wanazuoni (maulamaa) wa Iran zilikuwa zikikabiliwa na mashambulio yasiyosita ya tawala za wakati huo wa vibaraka wa Uingereza kwa upande mmoja; na kwa upande wa pili, maadui wasomi waliokuwa na kasumba za Kimagharibi, hata hivyo, harakati hizo zilianza kutafuta njia za kuutetea Uislamu na kuihifadhi nafasi ya maulamaa.

Ayatullah Udhma Sheikh Abdul Karim Hairi aliitwa na maulamaa mashuhuri wa wakati huo wa Qum, na akahajiri Arak na kuelekea katika mji huo mtakatifu. Baada ya muda si mrefu, Imam Khomeini ambaye kutokana na kipaji chake cha ajabu alifanikiwa kumaliza kwa haraka masomo ya kimsingi na ya kati ya Hawza za Arak na Khomein, alielekea mjini Qum ambako akawa na nafasi muhimu katika ushirikiano wa kuimarisha nafasi ya Hawza mpya iliyoasisiwa muda si mrefu katika Qum. Haukupita muda, Imam Khomeini akatambulikana kuwa ni miongoni mwa wanazuoni wachache waliokuwa wamebobea na kutopea katika elimu za irfani, falsafa, usuli na fikihi katika Hawza ya Qum. Baada ya kufariki dunia Ayatullah Hairi mnamo tarehe 10 Januari 1937, Hawza ya Qum ikakabiliwa na hatari ya kusambaratika. Maulamaa wakakamavu waliamua kutafuta ufumbuzi wake. Katika kipindi cha miaka minane, uongozi wa Hawza ya Qum ulikuwa chini ya usimamizi wa Ayatullah Udhma Sayyid Muhammad Hujjat, Sayyid Sadruddin Sadr, na Sayyid Muhammad Taqi Khonsari (radhi za Mola ziwe juu yao).

Katika kipindi hicho, hasa baada ya kuangushwa utawala wa Reza Khan, mazingira kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Marjaa mkubwa wa kidini yakawa tayari. Ayatullah Udhama Burujerdi alikuwa shakhsia mtukufu wa kielimu ambaye alikuwa na sifa za kuchukua nafasi ya uongozi wa Hawza ya Qum iliyoachwa tupu na marehemu Ayatullah Hairi, na hivyo kuhifadhi na kulinda misingi na jina la chuo hicho kikuu cha kidini. Pendekezo hilo ambalo lililotolewa na wanafunzi wa Ayatullah Hairi akiwemo Imam Khomeini lilifuatiliwa kwa haraka. Imam Khomeini mwenyewe alifanya jitihada kubwa kumwalika Ayatullah Burujerdi ahajiri na kwenda Qum ili akachukue jukumu zito la uongozi na kuwa mkuu wa Hawza ya Qum. Alikuwa akifahamu vyema hali nyeti ya kisiasa iliyokuwa ikitawala katika jamii na vyuo vya kidini katika kipindi hicho. Alikuwa akiifahamu hali pamoja na mazingira hayo yaliyokuweko kutokana kuwa makini katika kufuatilia mambo na alikuwa akipata habari kwa kusoma kwake daima vitabu vya historia vya zama hizo na majarida pamoja na magazeti yaliyokuwa yakichapishwa na kutolewa wakati huo. Aidha safari zake za kwenda na kurudi Tehran na kuhudhuria vikao na majlisi za wanazuoni wakubwa kama Ayatullah Moddaresi ni miongoni mwa mambo yaliyomsaidia kuongeza maarifa yake na kufahamu hali halisi ya mambo yalivyo. Hivyo, alifikia natija hii kwamba tumaini pekee la kuiokoa jamii kutokana na madhila baada yakushindwa kwa harakati za Mashrutiyyat, na hasa baada ya tuko la kuja madarakani Reza Khan, lilikuwa ni kuleta mwamko katika vyuo vya kidini. Na lililokuwa la msingi zaidi kabla ya hilo ni kudhamini uhai wa vyuo hivyo vya kidini na kuweka uhusiano wa kimaanawi (kiroho) baina ya wananchi na viongozi wa kidini. Akifuatilia malengo yake matukufu, katika mwaka 1949, Imam Khomeini aliandaa mpango wa marekebisho ya kimsingi ya mfumo wa Hawa kwa kushirikiana na Ayatullah Murtadha Hairi na kuwasiliana na Ayatullah Burujerdi. Mapendekezo ya mpango huo ulipokewa na kuungwa mkono na wanafunzi wa Imam pamoja na matalaba (wanafuzi wa Hawza) waliokuwa na dhamira safi ya mwamko.

Hata hivyo, utawala wa Kifalme wa Shah ulikosea katika mipango yake. Muswada wa uchaguzi uitwao “Serikali za Majimbo na Wilaya” ambao uliondosha masharti ya mgombea au mpiga kura kuwa Mwislamu, kula kiapo cha Qur’ani Tukufu, na kuwa mwanamume, ulipasishwa katika Baraza la Mawaziri la Amir Asadullah Alam mnamo tarehe 8 Oktoba 1962. Uhuru wa kuchaguliwa wanawake ulikuwa ni kisingizio chakutekeleza malengo mengine. Kufutwa na kubadilishwa masharti mawili ya mwanzo (yaani ulazima wa kuwa Mwislamu na kula kiapo kwa Qur’ani), kulikuwa na lengo hasa ya kuandaliwa uwanja na kuhalalisha kuingia katika vyombo vya dola Bahai. Kama ilivyokuwa imeashiriwa hapo kabla, uungaji mkono wa Shah wa utawala wa Kizayuni ulikuwa katika mpango wa kustawishwa uhusiano baina Iran na Israel, na kwamba ulikuwa ni sharti la Marekani la kumwunga mkono Shah. Kwa hakika, malengo hayo ya yangetimia kwa kupenya na kuingizwa wafuasi wa pote la kikoloni wa Kibahai katika vyombo vikuu vitatu vya dola.

Mara tu baada ya kutangazwa habari ya kupasishwa muswada huo, Imam Khomeini akiwa na maulamaa wakubwa wa Qum na Tehran, wakakaa kubadilishana mawazo na kuamua kuanza upinzani kutoka kila upanda. Katika mazingira hayo, nafasi ya Imam Khomeini katika kuweka wazi na kubainisha malengo halisi ya utawala wa Shah na kukumbusha ujumbe muhimu wa maulamaa viongozi wa vyuo vya kidini ilikuwa na taathira kubwa. Telegrafu na barua wazi za upinzani za maulamaa kwa Shah na (Waziri Mkuu) Asadullah Alam, zilisababisha wimbi la uunaji mkono wa matabaka tofauti ya wananchi. Imam Khomeini alitumia lugha kali na ya kutahadharisha katika telgrafu zake kwa Shah na Waziri Mkuu. Katika mojawapo wa telegrafu hizo, Imam Khomeini aliandika haya:

“Ninakuusieni mtiini Mwenyezi Mungu, mfuateni Katiba ya nchi na mwogopeni matokea mabaya ya kwenda kinyume na Qur’ani, hukumu (fatwa) za maulamaa wa taifa na viongozi wa Waislamu na kwenda kinhyume na Katiba. Msiitumbukizeni nchi katika hatari kwa makusudi na bila ya sababu, ama sivyo, maulamaa wa Kiislamu hawatoacha kutoa matamshi dhidi yenu.”

Kwa utaratibu huo, kadhia ya Muswada wa Majimbo na Wilaya ikawa ni uzoefu wa ushindi wenye thamani kwa taifa la Iran, hasa kwa kuzingatia kwmaba kwa namna fulani sifa zinazomstahikia shakhsia zilitambulika kwa ajili ya uongozi wa Umma wa Kiislamu. Licha ya Shah kushindwa katika kadhia hiyo, mashinikizo ya Marekani kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho inayoyataka yaliendelea. Mwezi wa Januari mwaka 1962, Shah aliitaja Misingi Sita ya Marekebisho na kutaka ipigiwe kura ya maoni.

Kwa mara nyingine, Imam Khomeini aliwaita Marjaa Taklidi na maulamaa wa Qum wakutane katika kikao kutafuta ufumbuzi. Kwa pendekezo la Imam Khomeini, sikukuu ya Nairuzi (mwaka mpya wa Kiirani) ya mwaka 1963 ikasusiwa ili kuonyesha upinzani dhdi ya hatua ya utawala wa Shah. Katika taarifa yake, Imam Khomeini aliyaita Mapinduzi Meupe ya Shah kuwa ni Mapinduzi Meusi, na akafichua kuweko njama za pamoja kati ya Shah, Marekani na Israel. Kwa upande mwingine, Shah alikuwa amekwishawahakikishia wakuu wa Washington kwamba wananchiwa Irano wako tayari kwa ajili ya kufanya marekebisho ya Marekani, na akayaita marekebisho hayo – Mapinduzi Meupe. Upinzani wa maulamaa dhidi yake ulionekana ungempelekea pabaya mfalme huyo. Imam Khomeini alikuwa akimtaja waziwazi Shah katika mikusanyiko ya watu kuwa ni chanzo cha jinai na kwamba ni muitifaki na mshirika wa Israel, nakuwataka wananchi wasimame dhidi yake. Katika hotuba yake ya tarehe mosi Aprili mwaka 1963, Imam aliukosoa vikali ukimya wa maulamaa wa Qum, Najaf na miji mengine ya Kiislamu mbele ya jinai mpya za utawala wa Shah, na akasema: “Leo kunyamaza kimya kunamaanisha kukubaliana na utawala wa dhalimu.”

Siku iliyofuatia (Aprili pili) alisambaza taarifa yake maarufu iliyoitwa, “Kumpenda Shah Kunamaanisha Kupora.” Siri ya taathira ya kustaajabisha yaujumbe wa Imam na maneno yake katika nyoyo za wananchi waliokusudiwa hadi kuwa tayari kufidia roho zao, lazima iangaliwe katika huko kuwa na fikra halisi, uamuzi madhubuti pamoja na ukweli usiona shaka aliokwa nao katika kuamiliana na wananchi. Mwaka mpya wa Kiirani wa 1342 (1963) ulianza kwa kususiwa sherehe za sikukuu ya Nairuzi pamoja na umwagaji wa damu wa (wanafunzi) walioonewa wa (Madrasah ya) Faidhiyyah (mjini Qum). Shah alikuwa aking’ang’ania na kusisitiza kutekelezwa marekebisho kufuatanana matakwa ya Marekani wakati Imam Khomeini alikuwa akikazana kuwaamsha wananchinakuwataka wasimame kukabiliana na Marekani na khiyana na usaliti wa Shah.

Tarehe 3 Aprili mwaka huohuo wa 1963, Ayatullah Udhma Hakim alituma telegrafu kutoka mjini Najaf kuwataka maulamaa na Marjaa wa Iran wote wa kidini wahajiri kwa pamoja kuelekea Najaf. Pendekezo hilo lilitolewa ili kuzisalimisha roho za maulaamaa na nguzo za vyuo vikuu vya kidini. Lakini Imam Khomeini hakujali vitisho hivyo, bali aliijibu telegrafu ya Ayatullah Udhma Hakim na kusisitiza kwamba hakuna maslahi kuhajiri kwa pamoja maulamaa wote na kuiacha tupu Hawza. Katika risala yake (ya tarehe 2 Mei 1963) kwa mnasaba wa (siku) arobaini ya mauaji katika Faydhiyyah, Imam Khomeini alisisitiza maulamaa na wananchi wa Iran kusimama bega kwa bega pamoja na viongozi wa nchi za Kiislamu na Kiarabu kukabiliana na utawala ghasibu wa Isarael. Aidha alilaani mikataba na makubaliano bainaya Shah na Israel.

Mapambano ya Khordad 15:

Mwezi wa Muharram wa mwaka 1963 ambao ulisadifiana na mwezi wa Khordad uliwadia. Imam Khomeini aliitumia ipasavyo fursa hiyo kuwahamasisha wananchi kwa ajili ya kusimama dhidi ya utawala wa kidikteta wa Shah.

Alasiri ya siku ya Ashura ya tarehe 13 Khordad mwaka 1342 (21 Mei 1963) Imam Khomeini alitoa hotuba ya khistoria katika madrasa ya Feidhiyya ambayo ilikuwa mwanzo wa mapambano ya Khordad 15 (Mei 23).

Ilikuwa ni katika hotuba hiyo pale Imam Khomeini alipotamka kwa sauti ya juu kumwambia Shah: “Ee bwana ninakuasa! Ewe bwana Shah! Ewe mheshimiwa Shah! Mimi ninakupa nasaha acha mambo hayo, Ee bwana wanakuzuga na kukubabaisha hao. Mimi nisingependa kama itafika siku watake uondoke, watu wote washukuru (kwa kutokea hilo)… Kama wanakuamrisha na kukwambia soma, jaribu kutafakari ya kando yake. Zisikilize nasaha zangu… kwani kuna uhusiano gani kati ya Shah na Israel mpaka idara ya usalama inasema msizungumze chochote kuhusu Israel… Kwani Shah ni Muisrael?” Shah alitoa amri ya kuzimwa maandamano ya upinzani. Idadi kubwa ya wafuasi wa Imam Khomeini walitiwa nguvuni usiku wa tarehe 14 Khordad (Mei 24); na saa tisa ya alfajiri (ya tarehe 15 Khordad 1342) mamia ya makomandoo waliotoka makao makuu waliizingira nyumba ya Imam Khomeini, wakamkamata yeye mwenyewe hali ya kuwa yumo ndani ya ibada ya sala za usiku, wakamchukua katika hali ya kukanganya hadi Tehran na kumweka kwenye mahabusu ya kituo cha maafisa wa jeshi na kisha magharibi ya siku ile ile wakamhamishia jela ya Kasri. Asubuhi ya tarehe 15 Khordad habari za kutiwa nguvuni kiongozi wa Mapinduzi zilifika na kueneo katika miji ya Tehran, Mashhad, Shiraz na miji mingine, na hali (katika miji hiyo) ikafanana na ile ya Qum.

Mshauri wa karibu zaidi na wa siku zote wa Shah, kamanda Hussein Fardust ameeleza wazi katika kumbukumbu zake kuhusu utumiaji wa uzoefu na ushirikiano wa maafisa wenye vipawa vya juu kabisa wa kisiasa na kiusalama wa Marekani kwa ajili ya kuzima mapambano, na vile vile kuhusu kukanganyikiwa kwa Shah, maafisa wa Ikulu yake na wakuu wa jeshi na wa (idara ya usalama) Savak katika nyakati hizo na kubainisha ni vipi Shah na majenerali wake wakiwa kama watu waliopatwa na kichaa walivyotoa amri za kuzimwa maandamano?

Baada ya kuwekwa kwenye jela ya Kasri kwa muda wa siku 19 Imam Khomeini alihamishiwa jela moja katika kambi ya kijeshi ya Eshratabad.

Ilionekana kana kwamba mapambano yamezimwa baada ya kutiwa nguvuni kiongozi wa harakati na kuuawa kinyama wananchi siku ya tarehe 15 Khordad. Akiwa mahabusu Imam Khomeini aliepuka kujibu maswali ya wasaili badala yake kwa ushujaa aliwaambia kuwa utawala wa Iran na vyombo vyake vya mahakama si halali na havina ustahiki. Usiku wa tarehe 18 Farvardin mwaka 1343 (25 Machi 1964) na pasina kupewa taarifa kabla, Imam Khomeini aliachiwa huru na kupelekwa Qum. Mara tu watu walipopata taarifa, shangwe na furaha zilienea mjini na sherehe kubwa zikafanyika kwa muda wa siku kadhaa huko kwenye madrasa ya Faidhiya na maeneo mengine ya mji. Maadhimisho ya mwaka wa kwanza wa tukio la Khordad 15 yalifanyika mwaka 1343 (1964) kwa taarifa ya pamoja iliyotolewa na Imam Khomeini na Marjaa Taklidi (viongozi wakuu wa kidini) wengine, na vile vile taarifa mbali mbali zilizotolewa na vyuo vya kidini na kutangazwa siku hiyo kuwa siku ya maombolezo.

Tarehe 4 Aban mwaka 1343 (13 Oktoba 1964) Imam Khomeini alitoa taarifa ya kimapinduzi ambayo ndani yake aliandika kuwa: “Dunia ielewe kwamba masaibu yote liliyonayo taifa la Iran na mataifa mengine ya Kiislamu yanatokana na madola ya kigeni; yanatokana na Marekani; mataifa ya Kiislamu yanachukiza mbele ya madola ya kigeni kiujumla na hasa hasa Marekani; Marekani ambayo inaiunga mkono Israel na wafuasi wake. Ni Marekani ndiyo inayoitia nguvu Israel za kuwafanya Waarabu Waislamu wapoteze makaazi yao.”

Ufichuaji uliofanywa na Imam Khomeini dhidi ya mswaada wa Capitulation (Mkataba wa kuwaruhusu wageni kutumia sheria za nchi zao katika nchi nyingine na kufanya lolote wanalotaka katika nchi hizo kama vile kutumia sheria za nchi zao za mahakama katika nchi nyingine, kusimamia mikataba ya nchi nyingine n.k) uliifanya Iran katika mwezi wa Aban mwaka 43 (Oktoba 64) ikaribie kuingia kwenye vuguvugu jengine la mapambano.

Alfajiri ya tarehe 13 Aban mwaka 1343 (22 Oktoba 1964) makomandoo wenye silaha waliotumwa kutoka Tehran walikwenda kuizingira tena nyumba ya Imam Khomeini huko Qum. Ajabu ni kuwa mara hii pia wakati wa kutiwa nguvuni Imam Khomeini, ulisadifiana na wakati mwanachuoni huyo akiwa katika ibada kama ilivyokuwa wakati alipotiwa nguvuni mwaka wa kabla yake. Imam Khomeini alitiwa nguvuni na huku akiongozwa na askari usalama alipelekwa moja kwa moja hadi uwanja wa ndege wa Mehrabad huko Tehran, akatiwa kwenye ndege ya kijeshi iliyokuwa imeshaandaliwa kabisa, na huku akiwa chini ya ulinzi wa maafisa wa kijeshi na kiusalama akasafirishwa kuelekea Uturuki. Jioni ya siku ile Idara ya usalama ya Savak ikatangaza magazetini habari ya kupelekwa uhamishoni Imam Khomeini kwa tuhuma za kutishia usalama wa nchi!

Licha ya kuweko mazingira kama hayo ya ukandamizaji, lakini wimbi la malalamiko lilizidi kushuhudiwa kupitia maandamano katika maeneo ya biashara ya Tehran, kusimamishwa kwa muda mrefu masomo katika vyuo vya kidini pamoja na kuandikwa barua za wazi kwa jumuiya za kimataifa na Marjaa Taklidi.

Imam Khomeini alikaa Uturuki kwa muda wa miezi kumi na moja. Katika muda huo utawala wa Shah ulichukua hatua kali ambazo zilikuwa hazijawahi kushuhudiwa mfano wake, na kukandamiza cheche za mapambano zilizosalia nchini Iran; na kutokana na kutokuwepo Imam Khomeini utawala huo ulichukua hatua za haraka za kutekeleza mageuzi yaliyotakiwa na Marekani. Ukaazi wa lazima huko nchini Uturuki ulitoa fursa nzuri kwa Imam kwa ajili ya kuanza kuandika kitabu adhimu cha Tahrir ul’ Wasilah.

Kuondolewa Imam Khomeini (Quddisa Sirruh) Uturuki na Kuhamishiwa Iraq

Siku ya tarehe 13 Mehr mwaka 1343 (Oktoba 5, 1964) Imam Khomeini akiwa pamoja na mwanawe Ayatullah Haj Mustafa waliondolewa Uturuki na kupelekwa kwenye kituo cha pili cha uhamishoni ambacho ni nchi ya Iraq. Baada ya kuwasili Baghdad, Imam Khomeini alielekea kwenye miji ya Kadhimain, Samarrah na Karbala kwa ajili ya kuzuru haram tukufu za Maimamu watoharifu, na wiki moja baada ya hapo ndipo alipoelekea mahali pa makaazi yake halisi yaani Najaf.

Kipindi cha miaka 13 cha ukaazi wa Imam Khomeini huko Najaf kilianza katika hali ambayo pamoja na kwamba kidhahiri hakukuwepo mashinikizo na vizuizi kwa kiwango kama kile cha Iran na Uturuki, lakini upinzani, ukorofi, masimango na “kupiga vijembe,” na licha ya kwamba mambo hayo hayakufanywa na pote la adui rasmi, bali yalitoka kwa watu waliojifanya maulamaa ambao walikuwa ni wapenda dunia waliojificha kwenye vazi la dini yalikuwa makubwa na ya kuumiza kiasi kwamba pamoja na kuwa maarufu kwa subira na stahamala, Imam alikuwa mara kadha wa kadha akisimulia kwa uchungu mkubwa hali ngumu ya mapambano katika miaka hiyo. Hata hivyo hakuna lolote kati ya mashaka na masaibu hayo yaliyoweza kumzuia kuendelea na njia yake aliyokuwa ameichagua kwa uelewa kamili.

Pamoja na kila aina ya pingamizi na upinzani wa watu wenye utashi wa binafsi, mnamno mwezi wa Aban mwaka 1344 Imam Khomeini aliweza kuanzisha mfululizo wa darsa zake za Fikhi ya daraja ya ijtihad katika msikiti wa Sheikh Ansari (Rahmatullah Alayh) huko Najaf, ambazo ziliendelea hadi alipoondoka Iraq na kuelekea Paris Ufaransa. Darsa zake ndizo zilizokuwa zikiongoza huko Najaf katika upande wa ubora na idadi ya wanafunzi.

Tokea alipowasili Najaf Imam Khomeini alikuwa akituma barua na wajumbe nchini Iran na hivyo kudumisha mawasiliano yake na wanamapambano ambapo katika kila mnasaba aliitumia fursa hiyo kuwataka wasimame imara katika kuendeleza malengo ya mapambano ya Khordad 15.

Katika kipindi chote cha kuweko uhamishoni, Imam Khomeini hakuacha kuendelea na mapambano licha ya taabu na mashaka yote yaliyojitokeza, ambapo kupitia ujumbe na hotuba zake aliyafanya matumaini ya ushindi yaendelee kubaki ndani ya nyoyo za watu.

Katika mahojiano aliyofanya tarehe 19 ya mwezi wa Mehr mwaka 1347 (Oktoba 11, 1968) na mwakilishi wa harakati ya Fat-h ya Palestina, Imam Khomeini alibainisha mitazamo yake kuhusiana na masuala ya ulimwengu wa Kiislamu na jihadi ya taifa la Palestina, ambapo katika mahojiano hayo hayo alitangaza fatwa ya kuwajibisha kutenga fungu katika nguzo ya Zaka kwa ajili ya mujahidina wa Palestina.

Mwanzoni mwa mwaka 1348 hitilafu zilishtadi kati ya utawala wa Shah na ule wa chama cha Baath nchini Iraq juu ya mpaka wa majini wa nchi mbili. Utawala wa Baath uliwafukuza kinyama raia wa Iran waliokuwa wakiishi huko Iraq. Katika mazingira hayo chama cha Baath kilijaribu kwa kila njia kuutumia kwa maslahi yake uadui wa Imam Khomeini kwa utawala wa Iran.

Kutokana na miaka minne ya usomeshaji na juhudi alizofanya za kuwaamsha watu Imam Khomeini aliweza kwa kiwango fulani kubadilisha hali ya Chuo Kikuu cha kidini (Hawza) cha Najaf. Ambapo katika mwaka 1348 mbali na wapiganaji wasio na idadi waliokuweko ndani ya Iran, huko Iraq, Lebanon katika miji mingine ya Kiislamu nako, Waislamu wengi waliichukulia harakati ya Imam Khomeini kama kigezo kwao.

Imam Khomeini (Quddisa Sirruh) na Kuendelea Mapambano (1350-1356)

Katika nusu ya pili ya mwaka 1350 hitilafu kati ya utawala wa kibaathi wa Iraq na Shah zilipamba moto na kupelekea kutimuliwa na kuachwa bila makaazi Wairan chungu nzima waliokuwa wakiishi Iraq. Katika ujumbe wa telegrafu alioutuma kwa Rais wa Iraq, Imam Khomeini alilaani vikali hatua za utawala huo. Katika kulalamikia hali hiyo iliyojitokeza Imam Khomeini aliamua kuondoka Iraq, lakini kutokana na kuelewa athari zitakazojitokeza kutokana na kuhama Imam katika mazingira hayo, watawala wa Kibaathi hawakumruhusu kuondoka. Katika mwaka 1354 wakati wa maadhimisho ya mapambano ya Khordad 15 Madrasa ya Feidhiyya ya Qum ilishuhudia kwa mara nyingine maandamano ya wanafunzi wanamapinduzi wa kidini. Nara za adumu Khomeini na mauti kwa silsila ya Kipahlavi zileendelea kwa muda wa siku mbili. Kabla ya hapo makundi ya wapiganaji wa chini kwa chini yalisambaratishwa, na shakhsiya wanamapambano wa kidini na kisiasa waliwekwa kwenye jela za utawala wa Shah.

Katika kuendeleza siasa zake za kupiga vita dini, mnamo mwezi wa Esfand mwaka 1354 Shah aliamua kufanya usafihi wa kubadilisha kalenda rasmi ya nchi ambayo hesabu yake inaanzia kwenye Hijra ya Mtume na kuifanya ianzie wakati wa kuasisiwa ufalme wa Hakhan Maneshi. Katika radiamali yake kali dhidi ya hatua hiyo, Imam Khomeini alitoa fatwa ya kuharamisha utumiaji wa kalenda hiyo ya kifalme isiyo na maana. Wananchi wa Iran waliupokea vizuri mwito wa kususia utumiaji wa kalenda hiyo isiyo na msingi kama walivyokisusia chama cha Rastakhiz, na kesi zote mbili hizo ziliufedhehesha utawala wa Shah, kiasi kwamba mnamo mwaka 1357 utawala huo ulilazimika kusalimu amri na kuifuta kalenda hiyo ya kifalme.

Kufikia Kileleni Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1356 (1977)

Imam Khomeini ambaye alikuwa akifuatilia kwa makini matukio yaliyokuwa yakijiri ulimwenguni pamoja na Iran aliitumia kikamilifu fursa iliyojitokeza. Katika mwezi wa Mordad mwaka 1356 (Agosti 1977) alitoa ujumbe akitangaza kuwa: Hivi sasa fursa imepatikana kwa jumuiya za kielimu na kiutamaduni, wazalendo na wanachuo walioko ndani na nje ya nchi pamoja na mabaraza ya Kiislamu yaliyoko kila mahala kutumia fursa hiyo na kufichua kila kitu hususan kutokana na hali iliyojitokeza ndani na nje ya nchi na kuakisiwa jinai za utawala wa Shah katika mashirika ya kimataifa na vyombo vya magazeti ya nje.

Kuuawa shahidi Ayatullah Haj Mustafa Khomeini mnamo tarehe Mosi Aban mwaka 1356, (Oktoba 23, 1977) na maombolezo yaliyofana yaliyofanyika nchini Iran ilikuwa cheche ya kuanza tena mwamko wa mapambano katika vyuo vya kidini pamoja na jamii ya kidini ya Iran. Katika hali ya kustaajabisha Imam Khomeini alilitaja tukio hilo la wakati huo kuwa ni miongoni mwa rehma zilizojificha za Mwenyezi Mungu. Utawala wa Shah uliamua kuchukua hatua ya kulipiza kisasi kwa kuchapisha kwenye gezati la Ettelaat makala ya kumtusi Imam Khomeini. Malalamiko dhidi ya makala hiyo yaliibua maandamano ya mapambano ya tarehe 19 Dei mwaka 1356 (Januari 9, 1978) huko Qum ambapo katika maandamano hayo idadi kadhaa ya wanamapinduzi wanachuo wa kidini waliuawa na kujeruhiwa. Licha ya kuchuku hatua ya kuua umati wa watu lakini Shah hakuweza kuuzima moto wa mapambano. Kwa mtazamo wa Imam Khomeini njia pekee iliyokuwa imesalia wakati huo ilikuwa ni kujiandaa kijeshi na kuendesha jihadi ya mtutu wa bunduki endapo Marekani ingeamua kuingilia kati na kufanya mapinduzi ya kijeshi.

Kuhama Imam Khomeini (Quddisa Sirruh) Iraq na Kuelekea Paris

Katika mazungumzo yaliyofanyika huko New York kati ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Iraq ulichukuliwa uamuzi wa kumfukuza Imam Khomeini nchini Iraq. Tarehe Pili Mehr 1357 (Oktoba 10, 1978) nyumba ya Imam huko Najaf ilizingirwa na vikosi vya utawala wa Baath. Kutangazwa habari hiyo kuliamsha ghadhabu kubwa za Waislamu nchini Iran, Iraq na katika nchi nyinginezo.

Tarehe 12 Mehr mwaka huo Imam Khomeini aliondoka Najaf na kuelekea kwenye mpaka wa Kuwait. Kwa agizo iliyopewa na utawala wa Iran, Serikali ya Kuwait ilimzuia Imam Khomeini asiingie nchini humo. Kabla ya hapo lilizungumziwa suala la Imam kuelekea Lebanon au Syria. Lakini baada ya yeye mwenyewe kushauriana na mwanawe (Hujjatul Islam Sayyid Ahmad Khomeini) alichukua uamuzi wa kulekea Paris. Tarehe 14 Mehr aliwasili mjini humo. Na siku mbili baadaye akahamia kwenye nyumba ya mmoja wa Wairan huko Neauphle-le-Château (kwenye viunga vya mji wa Paris). Maafisa wa Ikulu ya Ufaransa (Elizze) walimfikishia Imam Khomeini ujumbe wa Rais wa nchi hiyo wa kumtakaa asijishughulishe na harakati zozote za kisiasa. Imam alieleza wazi kupitia radiamali kali aliyotoa kwamba kuwekewa mipaka ya aina hiyo kunakinzanana madai ya (kutetea) demokrasia na kwamba kama atakuwa hana budi kutoka kiwanja kimoja cha ndege na kuelekea kingine, na nchi moja hadi nyingine (atafanya hivyo) lakini hatoacha kupigania malengo yake.

Mnamo mwezi wa Dei mwaka 1357 (Januari 1979) Imam Khomeini aliunda Baraza la Mapinduzi. Mnamo tarehe 26 Dei, 1357 (Januari 16, 1979) Shah alikimbia nchini baada ya kuunda baraza la kifalme na baraza la mawaziri la Bakhtiyar kupigiwa kura ya kuwa na imani nalo. Habari zilianza kuenea katika mji wa Tehran na kisha katika miji mingine ya Iran, na wananchi wakaingia mabarabarani kusherehekea kwa nderemo na vifijo kukimbia Shah.

Kurejea Imam Khomeini Nchini Iran baada ya Miaka 14 ya Uhamishoni

Mwanzoni mwa Bahman mwaka 1357 (Mwishoni mwa Januari 1979) zilitangazwa habari za uamuzi wa Imam Khomeini wa kurejea nchini Iran. Kila aliyesikia habari hiyo alitokwa na machozi ya shauku na furaha. Wananchi walikuwa katika hali ya kusubiri kwa muda wa miaka 14. Lakini pamoja na hayo wananchi hao pamoja na watu wa karibu na Imam walikuwa wakimhofia maisha yake, kwa sababu serikali kibaraka ya Shah bado ilikuweko madarakani, na sheria ya hali ya hatari ilikuwa imetangazwa nchini. Pamoja na hayo Imam Khomeini alikuwa ameshachukua uamuzi, na katika ujumbe mbali mbali aliotoa kwa wananchi wa Iran alieleza kwamba anataka kuwa pamoja na wananchi katika siku hizo nyeti na zenye umuhimu mkubwa. Serikali ya Waziri Mkuu Bakhtiyar kwa mashauriano na Jenerali Haizer wa Kimarekani ilikuwa imevifunga viwanja vyote vya ndege kuzuia ndege zote za kigeni zisitue nchini.

Lakini baada ya siku chache ililegeza msimamo na kulazimika kukubali matakwa ya wananchi. Hatimaye asubuhi ya siku ya Alkhamisi ya tarehe 12 Bahman 1357 (Februari 1, 1979) Imam Khomeini aliwasili nchini Iran baada ya miaka 14 ya kuwa mbali na nchi yake. Mapokezi makubwa ya wananchi wa Iran ambayo hayakukanushika kuwa yalikuwa hayajawahi kushuhudiwa mfano wake yaliripotiwa na vyombo vya habari vya Magharibi ambavyo vililazimika kukiri na kuripoti kuwa idadi ya wapokezi ilikuwa kati ya watu milioni 4 hadi 6.

Kuaga Dunia Imam Khomeini (Quddisa Sirruhu), Kukutana na Mola Mpenzi, Kutengana na Wananchi Wapenzi

Imam Khomeini alifikisha na kubainisha kila kilichohitajika kufikishwa katika malengo na makusudio yake; na katika utekelezaji alifanya kila aliloweza kwa ujudi na uwepo wake wote ili kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa. Wakati ilipokaribia Khordad 15 mwaka 1368 (Juni 5, 1989) alikuwa tayari amejiandaa kwa ajili ya kwenda kukutana na Mola wake mpenzi. Uhai wake wote alikuwa ameutumia kwa ajili ya kupata radhi Zake Mola, na ghairi ya Kwake Yeye hakujidhalilisha mbele ya mwenye nguvu yoyote yule, na machozi yake hayakububujika kwa ajili ya yeyote ghairi Yake Yeye. Mashairi yake yote ya kiirfani yalikuwa yanadhihirisha machungu ya lahadha na sekunde ya kutengana na umma, na kubainisha kiu aliyokuwa nayo ya kukutana na Mola wake mpenzi. Lakini katika lahadha hiyo ukawa umewadia ule wakati wa adhama kubwa kwake na mgumu usiosthamalika kwa wafuasi wake. Yeye mwenyewe ameandika hivi katika wasia wake: “Kwa moyo mtulivu na nafsi iliyotua, roho yenye furaha na dhamira yenye matumaini, ninakuageni kwa fadhila za Mwenyezi Mungu ndugu zanguni, na ninaanza safari ya kuelekea makao ya milele; ninahitajia mno dua zanu za kheri, na namwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu anikubalie udhuru wangu kwa mapungufu na kasoro zote nilizokuwa nazo katika kutekeleza utumishi wangu, na natumai wananchi nao watanikubalia udhuru wangu kutokana na mapungufu na kasoro zote nilizokuwa nazo na wataendelea kusonga mbele kwa uwezo, irada na azma thabiti.”

Nukta ya kustaajabisha ni kuwa katika moja ya beti za mashairi yake ya kiirfani aliyoandika miaka michache kabla ya kuaga dunia, Imam Khomeini alisema hivi:

Katikati ya Khordad nasubiri faraja, miaka inapita na matukio yanakuja.

Saa nne na dakika ishirini usiku wa Jumamosi ya tarehe 13 Khordad mwaka 1368 (Juni 3, 1989) ilikuwa ndiyo lahadha ya makutano. Moyo ukasita kupiga; moyo ambao ulihuisha mamilioni ya nyoyo kwa nuru ya Mwenyezi Mungu na umaanawi. Kipindi cha kuugua kwake Imam, upasuaji aliofanyiwa na mpaka sekunde ya kuaga dunia, yote hayo yamerikodiwa kwa kutumia kamera zilizokuwa zimewekwa kwa siri ndani ya hospitali. Wakati sehemu tu ya picha hizo ziliporushwa hewani kupitia televisheni zikionyesha hali ya utulivu na umaanawi aliyokuwa nayo Imam, nyoyo za watu zilibadilika kwa namna ambayo hawezi kuielezea ila mtu aliyekuwepo katika mazingira hayo. Midomo yake Imam ilikuwa muda wote ikitikisika kwa kumdhukuru na kumtaja Mwenyezi Mungu.

Katika usiku wa mwisho wa uhai wake, na katika hali ambayo alikuwa ameweza kuvumilia operesheni kadhaa, ngumu na zilizochukua muda mrefu za upasuaji akiwa katika umri wa miaka 78, huku dripu kadhaa zikiwa zimetiwa mikononi mwake, Imam alikuwa akiendelea kusoma Qur’an na kusali sala zake za usiku. Katika saa za mwisho alikuwa na utulivu maalumu wa kimaanawi, na muda wote alikuwa akimunyamunya kwa kutamka shahada na ni akiwa katika hali hiyo ndivyo roho yake ilivyotoka kuelekea ulimwengu wa malakuti (wa Akhera). Wakati zilipotangazwa habari za kuaga dunia Imam, ilikuwa kana kwamba limetokea tetemeko kubwa la ardhi. Watu waliangua vilio, kuanzia ndani ya Iran nzima hadi katika kila pembe ya dunia ambako jina na ujumbe wa Imam Khomeini ulikuwa ukijulikana, kote huko watu walilia na kuomboleza. Hakuna maneno wala maandishi yoyote yanayoweza kuelezea hali za tukio hilo na uzito wa huzuni na majonzi waliyokuwa nayo watu katika siku zile.

Wananchi wa Iran na Waislamu wote wanamapinduzi walikuwa na haki ya kulia na kuomboleza hivyo na kuweka kumbukumbu ya maombolezo ambayo ukubwa na adhama yake haijawahi kushuhudiwa mfano wake katika historia. Walikuwa wamempoteza mtu ambaye aliwarudishia izza na utukufu wao uliokuwa umekanyagwa, aliyekata minyororo ya wafalme madhalimu, na kung’oa makucha ya waporaji wa Kimarekani na Wamagharibi katika ardhi zao, aliyehuisha Uislamu, akawapa utukufu na heshima Waislamu wenyewe, akaasisi Jamhuri ya Kiislamu, aliyesimama imara kukabiliana na madola yote ya kishetani ya dunia, kwa muda wa miaka kumi akaweza kusimama kidete na kukabiliana na mamia ya njama za mapinduzi, vitimbi na fitna za ndani na nje, na kwa miaka minane akaongoza (vita) vya kujihami dhidi ya adui aliyekuwa akipata uungaji mkono wa waziwazi na wa hali zote wa madola makuu mawili ya Mashariki na Magharibi. Wananchi walikuwa wameondokewa na kiongozi wao mpenzi, marjaa wao wa kidini na mlinganiaji wa Uislamu sahihi.

Huenda wale watu ambao wanashindwa kuelewa na kuyafahamu kwa undani masuala hayo, wakashindwa kupata tafsiri na maana ya matukio hayo kama wataona hali walizokuwa nazo watu katika filamu ya maombolezo na mazishi ya Imam Khomeini na kusikia habari za vifo vya makumi ya watu waliopata mshtuko wa moyo kutokana na kushindwa kuvumilia uzito wa msiba huo, na wakashuhudia pia katika picha na filamu jinsi viwiliwili kimoja baada ya kingine vya watu waliozirai kutokana na athari ya uzito wa majonzi vikibebwa juu kwa juu kwa mikono ya umati mkubwa wa watu vikikimbizwa mahospitalini.

Ama wale wanaoelewa maana ya kupenda na kuwa na uzoefu nako hawatokuwa na mushkeli wowote. Kwa hakika wananchi wa Iran walikuwa wakimpenda vilivyo Imam Khomeini kiasi kwamba katika mwaka wa kumbukumbu ya kufariki kwake walitoa nara na kaulimbiu ya kuvutia kuhusiana na yeye kwa kusema:

“Kumpenda Khomeini ni sawa na kupenda mazuri yote”

Siku ya tarehe 14 khordad 1368 (Juni 4, 1989), kilifanyika kikao cha Baraza la Maulamaa la Kumchagua Kiongozi Mkuu, na baada ya kusomwa wasia wa Imam Khomeini na Ayatullah Khamenei uliochukua muda wa masaa mawili na nusu, ukaanza mjadala juu ya kumchagua atakayeshika wadhifa wa kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu baada ya Imam Khomeini, na baada ya masaa kadhaa hatimaye Ayatullah Khamenei (Rais wa wakati huo wa Iran) ambaye yeye mwenyewe alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa Imam Khomeini (quddisa sirruh), aliyekuwa pia miongoni mwa shakhsiya wa mbele katika Mapinduzi ya Kiislamu na mapambano ya Khordad 15 na ambaye pia pamoja na wanamapinduzi wengine alijitolea nafsi yake katika mashaka na misukosuko ya vipindi vyote vya harakati ya Imam, ndiye aliyechaguliwa kwa kauli moja kubeba wadhifa huo nyeti. Kwa miaka kadhaa Wamagharibi na vibaraka wao wa ndani waliokuwa wamekata tamaa ya kumshinda Imam walikuwa wakijipa tamaa na kuwapa tamaa wanaowaunga mkono na walikuwa kwa miaka mingi wakisubiri kwa hamu kifo cha Imam.

Hata hivyo kuwa macho kwa taifa la Iran na chaguo sahihi na la haraka lililofanywa na maulamaa wanaomchagua Kiongozi, na vile vile uungaji mkono wa watoto na wafuasi wa Imam kwa Kiongozi mpya ulivunja tamaa zote walizokuwa nazo wapinga mapinduzi; na sio tu kwamba kuaga dunia kwa Imam hakukuwa mwisho wa njia yake, bali hakika ni kwamba huo ulikuwa mwanzo wa zama za Imam Khomeini katika uwanja mkubwa na mpana zaidi ya huko nyuma. Hivi kwani upo uwezekano wa kutoweka fikra, hakika, mazuri na umaanawi?

Usiku na mchana katika siku ya tarehe 15 Khordad mwaka 1368 mamilioni ya wakaazi wa mji wa Tehran na waombolezaji wengine waliotoka miji na vijiji mbali mbali walikusanyika kwenye uwanja mkubwa wa sala ya Ijumaa wa jiji la Tehran ili kwa mara ya mwisho waagane na kiwiliwili kitoharifu cha mtu ambaye mapambano yake yalihuisha thamani tukufu na heshima ya mwanadamu katika zama za giza la dhulma na akaanzisha katika ulimwengu harakati ya imani ya Mwenyezi Mungu na kurejea kwenye fitra na maumbile ya mwanadamu.

Katika maziko ya Imam Khomeini hazikuwepo ada na taratibu zozote rasmi za kiutawala zilizofanyika. Mambo yote waliyafanya wananchi wenyewe kwa mapenzi na kwa kujitolea. Kiwiliwili kitoharifu kilichofunikwa kwa kitambaa cha kijani cha Imam kilichoinuliwa juu kwa juu na umati wa mamilioni ya waombolezaji waliojawa na majonzi kilikuwa kiking’aa mithili ya kito. Kila mtu alikuwa akinong’ona na Imam wake mpenzi kwa lugha yake maalumu huku akimlilia na kububujikwa na machozi. Barabara kuu na njia zote zilizokuwa zikiishia kwenye uwanja mkuu wa sala ya Ijumaa zilifurika watu waliovaa nguo nyeusi za maombolezo.

Bendera za maombolezo zilitundikwa kwenye milango na kuta za nyumba za miji mbali mbali na sauti ya Qur’an tukufu ilisikika kwenye misikiti yote, nyumba, vituo na idara zote za serikali. Usiku ulipoingia maelfu kwa maelfu ya mishumaa iliwashwa kwenye barabara za uwanja wa sala ya Ijumaa na maeneo ya kando kando yake, ikiwa ni kukumbuka mwenge wa mapambano uliowashwa na Imam Khomeini. Familia zilizojawa na majonzi ziliketi zikiwa zimeizunguka mishumaa hiyo huku macho yao yakikodolea kilele hicho chenye nuru.

Mayowe ya Ya Hussein! Ya askari wa jeshi la kujitolea la Basiji waliokuwa wakijihisi wamekuwa mayatima, ambao walikuwa wakiomboleza kwa kujipiga vichwani na vifuani yaliifanya hali kuwa mithili ya siku ya Ashura. Lilikuwa ni jambo zito kwao wao kuamini kuwa hawatoisikia tena huko katika Husainiyya ya Jamaran sauti murua ya Imam Khomeini. Watu walikesha hadi asubuhi wakiwa wameketi kando ya mwili mtoharifu wa Imam. Asubuhi na mapema siku ya tarehe 16 Khordad (Juni 6), huku wakibubujikwa na machozi, mamilioni kwa mamilioni ya watu, wakiongozwa na Ayatullah Udhma Golpaigani (rahmatullah alayhi), walisimama kumsalia sala ya maiti Imam.

Umati mkubwa wenye hamu na shauku wa watu waliojitokeza siku Imam Khomeini alipowasili nchini tarehe 12 Bahman 1357 (Februari 1, 1979), na umati mkubwa zaidi uliojitokeza siku ya maziko ya Imam, ni miongoni mwa maajabu ya historia. Mashirika rasmi ya kimataifa ya habari yalikadiria kuwa watu milioni sita walijitokeza kumlaki Imam mwaka 1357 watu milioni tisa walihudhuria maziko yake. Na hii ni katika hali ambayo katika kipindi cha miaka 11 ya uongozi wa Imam Khomeini, wananchi wa Iran walikabiliwa na tabu, shida na matatizo mengi kutokana na uadui uliofanywa kwa ushirikiano wa nchi za Mashariki na Magharibi dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran pamoja na vita vya miaka minane na njama nyingine chungu nzima, kiasi cha kupoteza vipenzi na jamaa zao wengi sana katika njia hiyo; na kwa msingi huo ingelitarajiwa kuwa baada ya muda taratibu watu hao wangeanza kuchoshwa na hali hiyo na kuvunjika moyo; lakini katu haikuwa hivyo. Kizazi kilicholelewa kwenye Chuo cha Mafundisho ya Kiislamu cha Imam Khomeini kilikuwa kimeyaamini kikweli kweli maneno ya Imam kwamba:

“katika dunia (hii) kiwango cha kuvumilia mashaka, machungu na kujitolea muhanga kinalipa thamani yake kwa kiwango cha ukubwa wa lengo lililokusudiwa, thamani yake na daraja ya utukufu unaofikiwa.”

Baada ya shughuli za mazishi kusitishwa kutokana na hali nzito ya majonzi waliyokuwa nayo waombolezaji,  zilitolewa taarifa mfululizo kwa njia ya redio kwamba wananchi warudi majumbani kwao na kwamba maziko yameakhirishwa hadi wakati mwingine ambao utatangazwa hapo baadaye. Viongozi hawakuwa na shaka yoyote kuwa kadiri muda utakavyozidi kusonga mbele ndivyo maelfu kwa maelfu ya wananchi wenye mapenzi makubwa na Imam waliotoka miji mingine ya mbali kuelekea Tehran wataongezeka na kujiunga na umati wa watu kushiriki kwenye mazishi; hivyo ikawa hapana budi shughuli ya maziko ifanyike mchana wa siku ile ile katika hali hiyo nzito ya majonzi na kwa taabu kubwa. Baadhi ya taswira ya hali ya mambo ilivyokuwa iliakisiwa na kuripotiwa ulimwenguni na waandishi wa habari; na kwa njia hiyo kuaga dunia kwa Imam Khomeini, nako pia kama ulivyokuwa uhai wake kukawa ni chemchemu na chachu ya mwamko na harakati mpya, na kumbukumbu yake ikabaki kuwa ya milele. Na hii ni kwa sababu yeye alikuwa ni nembo ya haki; na haki kamwe haitoweki bali hubaki hai milele.

About Asadiq Media

Media for publicise the message of Wilaya under Imam Swadiq

Posted on June 2, 2018, in Habari na Matukio. Bookmark the permalink. Leave a comment.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Elijah J. Magnier

Middle East Politics

elbinawi

To interact with humanity & share ideas...

felicity114

felicity is the purpose of everybody

Ladakh Express

Ladakh's 1st political and cultural online journal.

Islamic Library

Shia Islamic PDFs - Now in Collaboration with ShiaTranslate.org!

zahraa Foundation

Fatima bint Muhammad is the Symbolization of Women's Power in Islam

mmubaraka1

A fine WordPress.com site

Pilgrim Center of Hope

Catholic Evangelization Ministry

World Shia Forum

Identity, Equality, Unity

Source of Inspiration

All is One, co-creating with the Creator

Bill Langill's Blog

Love is the Answer

Interrupting the Silence

An Episcopal Priest's Sermons, Prayers, and Reflections on Life, Becoming Human, and Discovering Our Divinity

Morgan L. Busse

In Darkness there is Light

YOGA

When unconscious became conscious this is Samadhi

Zoroastrians.net

Parsis, Iranis, Zarathushtis, All Under One Roof

Islamic Laws

Raising Awareness on Fiqh and the Ulema

Tech Cloud

Imagine | Innovate | Implement

Mujtaba Somji

Islamic sayings

%d bloggers like this: