Maoni yangu kuhusu sahaba- Sheikh Ayub

Na Samahat Sheikh Ayub Rashid, Muslim Community of England

“Mimi naamini kuwa kuna baadhi ya sahaba ambao, walisimama katika mwendo wa sawa na wengine walikengeuka baada ya Bwana Mtume (s.a.w.w. kufariki dunia). Baadhi yao walizua mambo kinyume cha dini yake; ndiyo sababu wasiruhusiwe kumfikia hata baada ya yeye mwenyewe kukumbusha kwamba hao walikuwa sahaba zake!”

Je sahaba ni nani?

Kwa mujibu wa taarifa ya Imam Ibn Hajar al-Asqalani, iliyomo uk. 10 wa Juzuu ya Kwanza ya kitabu chake kiitwacho al-lsaba, ‘sahaba ni yule aliyemkuta Mtume (s.a.w.w), sahaba ni yule aliyemuona Mtume akawa amemwamini, na akafa katika Uislamu.

 Sheikh ayubu.jpgHivyo, kwa waliomkuta (Mtume s.a.w.w.), aingia yule aliyekaa naye muda mrefu au mfupi; (aingia) na yule aliyepokea kwake au hakupokea; (aingia) na yule aliyepigana jihadi pamoja naye au hakupigana; na yule aliyemwona kwa macho japo iwe hakukaa naye, na (hata) yule ambaye hakumwona kwa kizuizi kama (cha) upofu.

Ibn Hajar katika uk. 5 wa Juzuu ya Saba ya Fathul Bari, amesema kwamba imepokewa kwa Ali b. al-Madini kuwa amesema: ‘Yeyote aliyefuatana na Mtume (s.a.w.w) au aliyemwona japo ni kwa saa moja mchana, ni miongoni mwa sahaba wa Mtume s.a.w.w.’

Na Imam Nawawi naye, katika uk. 14 wa Juzuu ya Kwanza ya Tahdhibul Asmaa Wal Lugh-ghaat, amesema: ‘Kuhusu sahaba kuna madhehebu mbili: lililo muhimu kati yao nayo ni madhehebu ya Bukhari na wanazuoni wengine wote wa Hadith, na jamaa katika wanazuoni wa fiqhi na wasiokuwa wao — ni kwamba kila Mwislamu aliyemwona Mtume s.a.w.w. japo ni kwa saa moja, na hata kama hakukaa naye na kuingiliana naye, (ni sahaba).’

Tunaposoma uk. 4 wa Juzuu ya Saba ya Fathul Bari na uk. 12 wa Juzuu ya Kwanza ya al-lsaba, tunamwona Imam Ibn Hajar al-Asqalani akisema: ‘…Lau mtu aliritadi, halafu akarejea katika Uislamu, lakini akawa hakumwona (Mtume s.a.w.w.) mara ya pili baada ya kurejea kwake (Uislamuni); lililo sahihi ni kwamba (mtu) huyo huhesabiwa ni sahaba kwa vile ambavyo wanazuoni wa Hadith wamemuhesabu hivyo Ash’ath b. Qays na mfano wake.

KISUNNI sahaba ni;

(i) yeyote yule aliyemwona Bwana Mtume s.a.w.w. na akafa hali yu Mwislamu;

(ii) wala si lazima awe amekaa naye sana, bali hata kama amemwona kwa saa moja tu inatosha;

(iii) na wala si lazima awe ni mtu mzima, bali hata kama alimwona utotoni au uchangani, na hata kama alikuwa bado yu utotoni au uchangani wakati Bwana Mtume s.a.w.w. alipofariki dunia; na

(iv) hata kama mtu huyo aliritadi, kisha akarejea Uislamuni, lakini asiwahi kumwona tena Bwana Mtume s.a.w.w. baada ya kurejea kwake huko!

Je sahaba wote ni waadilifu? Na je sahaba hawafanyi makossa? Na je haifai sisi kuzungumza yalewaliyoyafanya?

Imani yangu ni kuwa baadhi tu ya sahaba ndio waadilifu, na baadhi nyingine si waadilifu. Naamini kuwa wako masahaba wengi waliokuwa watu wazuri sana, na naamini pia wako baadhi yao waliokengeuka na kumuasi Mola wao kama binadamu wa kawaida. Kwa mfanoo;

(i) Qudaama b. Madh’un: Huyu ni miongoni mwa Waislamu wa mwanzo mwanzo. Alihama hijra mbili, akawahi hata kupigana katika Vita vya Badr. Lakini pamoja na yote hayo aliwahi kushikwa amelewa, zama za Ukhalifa wa Umar b. al-Khattab, akapigwa haddi! Jee, sahaba huyu bado ni mwadilifu? (Taz. al-lsaba, Juzuu ya Tatu, uk. 219-221; na al-lsti’ab, iliyo chini ya al-lsaba, Juzuu ya Tatu, uk. 247-251)

(ii) Abdulrahman (al-Awswat) b. Umar b. al-Khattab: Huyu, kama jina lake lionyeshavyo, alikuwa ni mtoto wa Khalifa wa Pili, na alikuwa ni sahaba vile vile. Yeye naye alikamatwa amelewa, na babake akampiga haddi! Hata inasemekana kwamba alikufa kwa kipigo hicho. (Taz. uk. 405-406 wa Juzuu ya Pili ya al-lsaba; na uk. 395-396 wa Juzuu ya Pili ya al-lsti’ab, iliyo chini ya al-Isaba) Jee, na huyo naye atakuwa ni mwadilifu?

(iii) Abu Mihjan: Huyu ni sahaba mwingine aliyekuwa akinywa pombe sana na kuzini; hata imeeelezwa kwamba Khalifa Umar b, al-Khattab aliwahi kumpiga viboko mara saba au nane kwa hilo! Akawahi hata kumfunga! (Taz. al-lsaba, Juzuu ya Nne, uk. 173-175; na uk. 181-187 wa Juzuu ya Nne ya al-lsti’ab iliyo chini ya hiyo al-lsaba.) Jee, sahaba kama huyo vipi huendelea kuwa mwadilifu?

(iv) Nu’aiman b. Amr. Huyu ni sahaba ambaye amepigana jihadi vita vyote. Lakini pamoja na hivyo, alikuwa mlevi! Mara nne Mtume Muhammad’ s.a.w.w. alimkamata sahaba huyo amelewa! Kati ya hizo, mara tatu alimpiga haddi! Mara ya nne, ndipo Umar b. al-Khattab alipotaka akatwe kichwa chake, lakini Bwana Mtume s.a.w.w. hakumkubalia. (Taz. chini ya jina la Marwan b. Qais al-Aslami katika uk. 384 wa Juzuu ya Tatu ya al-lsaba; na pia juzuu hiyo hiyo, uk. 540-541, chini ya jina la huyo Nu’aiman. Vile vile taz. Usudul Ghaba, Juzuu ya Nne, uk. 199 – 200, na Juzuu ya Tano, uk. 36 – 37.)

(v) Samura b. Jundub: Huyu ni mmoja ya wale watu watatu walio ambiwa na Bwana Mtume s.a.w.w. kwamba, wa mwisho wao kufa, ataingia Motoni. Yeye alikiuza pombel (Taz. chini ya Hadith Na. 61 katika uk. 82-84 wa Mujallada wa Kwanza wa Silsilatul Ahadithidh Dhaifa Wal Mawdhu’a ya Muhammad Nasiruddin al-Albani.)

(vi) al-Walid b. Uqba: Huyu ndiye yule ambaye Mwenyezi Mungu amemwita fasiq katika Sura 32:18 na Sura 49:6. Isitoshe; na ndiye yeye, pale alipokuwa Gavana wa mji wa Kufa zama za Ukhalifa wa Uthman bin Affan, aliyeswalisha watu swala ya asubudhi rakaa nne, na huku amelewa! Kisha akatapika kibulani, akatoa salamu na kuwauliza walioswali naye: Jee, niwaongezee? Kwa hivyo akapigwa haddi na kuondolewa kwenye Ugavana!

Ibn Abdilbar amesema amesema kwamba hakuna hitilafu baina ya wanazuoni kuwa aya hiyo iliteremshwa kwa ajili yake sahaba al-Walid bin Uqba, kama ilivyo tajwa katika uk. 601 wa Juzuu ya Tatu ya al-lsaba.

Je Mtume kasemaje kuhusu Masahaba?

Turejee Sahih Bukhari na Sahih Muslim:

(i) Imepokewa kwa Anas kwamba Mtume s.a.w.w. amesema: Watu miongoni mwa sahaba zangu watanijia kwenye Hodhi[7]. Nitakapowaona, na watakapokuwa waletwa kwangu, watazuiwa ili wasinifikie. Hapo nitasema: Sahaba zangu, sahaba zangu! Nami nitaambiwa: Wewe hujui walizua nini baada yako.

Hadith hiyo utaiona katika Sahih Muslim, ‘Kitabul Fadhaail’, Mlango wa ‘Hawdhu Nabiyyina (s.a.w.w) Waswifaatuhu.’ Kwa Kiingereza ni Hadith Na. 5706 kwenye ukurasa 1239 wa Juzuu ya Nne.

Hali kadhalika, Hadith yenye maneno karibu kama hayo yaweza kuonekana katika Sahih Bukhari, ‘Kitaabur Riqaaq’, Mlango wa ‘al-Hawdh’. Na kwa Kiingereza, ni hadith namba Na. 584 kwenye uk. 381 wa Juzuu ya Nane.

Hitimisho

Mimi naamini kuwa kuna baadhi ya sahaba ambao, walisimama katika mwendo wa sawa na wengine walikengeuka baada ya Bwana Mtume (s.a.w.w. kufariki dunia). Baadhi yao walizua mambo kinyume cha dini yake; ndiyo sababu wasiruhusiwe kumfikia hata baada ya yeye mwenyewe kukumbusha kwamba hao walikuwa sahaba zake!

Ma hiyo ni nature ya binaadamu wote. Wengine husimama mstari wa sawa na wengine hupotoka. Kwani wao hawakuwa Malaika!

 Je tuyazungumze ya masahaba au tusiyazungumze? Sisemi tuwatukane!

Kwangu ni muhimu sana kuyasimulia yaliyofanywa na masahaba bila ya kupendelea na kutia chumvi!

Kwa mfano, inajulikana kwamba miongoni mwa sahaba wako waliomsingizia bibi Aisha, mke wa Bwana Mtume (s.a.w.w) mambo machafu!

Wako waliotoka msikitini, wakamwacha Mtume (s.a.w.w) anahutubu juu ya mimbari siku ya Ijumaa, na wao wakakimbilia biashara

Mwisho

Mwenyezi Mungu anasema;

تِلْكَ أُمَّةٌ قَدْ خَلَتْ ۖ لَهَا مَا كَسَبَتْ وَلَكُمْ مَا كَسَبْتُمْ ۖ وَلَا تُسْأَلُونَ عَمَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ

‘Hao ni watu walio kwisha pita. Watapata waliyo yachuma, nanyi mtapata mtakayo yachuma; wala hamtaulizwa nyinyi waliyo kuwa wakiyafanya wao’

Sura al Baqara aya 134

Naamini kuwa wengi wa masahaba walikuwa ni watu wema sana na Mola amewaridhia na atawalipa mema kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kuuhami Usilamu na kumfuata Mtume Muhammad (s.a.w.w) na wakajitolea mali zao na maisha yao.

Msimamo wangu ni wa kati na kati, na maana yake ni kuwa, si vibaya nionavyo kuyazungumza mambo yaliyopita kwa na kati ya masahaba. Naamini pia kuwa ni vibaya kuwatukana na kuwalaani bila ya kosa lolote ambalo hawakulifanya. Naamini pia ni vizuri kuzungumza yaliyopita kati yao kwa ajili ya kupata ibra na mazingatio katika maisha yao. Siamini kuwa kukaa kimya ndio tiba. Kama kuna sahaba alifanya jambo jema ni vizuri kulisimulia, na kama kuna aliyefanya baya pia ni vizuri kulijua. Kama kuna aliyeritadi ni vizuri kujua huyo alikuwa nani na kwa nini? Mwendo huu utatusaidia kurekebisha mambo katika masiha yetu, kwani mara nyingine isi hujifunza kutokana na makossa ya watu wengine. Kama inavyosemwa ‘we learn through mistakes!

Mola awalipe mema maswahaba wema na akipenda kuwasamehe waliomkosea basi Yeye Allah ni Rauufun Rahiim.

Si kazi yangu mimi kumuingiza yeyote kati yao peopni au motoni!.

Sheikh Ayub Rashid, Muslim Community Uk.

 

UISLAMU DINI YA DUNIA

Kwa jinsi dunia a sasa ilivyo kuna kila haja ya walimwengu kurudi kwenye mfumo wa kimungu na kwa sababu hiyo Uislamu ni dini inayohitajika na walimwengu wote, Uislamu dini ya Dunia

MAUAJI YA HUSSEIN,NANI WA KULAUMIWA? KWANINI YAKUMBUKWE?

Waislamu duniani wameendelea kuyakumbuka na kuyaenzi mapinduzi ya Imam Hussein kwa kuweka vikao mbalimbali katika misikiti na sehemu zingine, Maswali yamebaki kwa

sheikh ayub rashid

baadhi ya waislamu na hata wasiokuwa waislam wanajiuliza kwanini Hussein, na je nani wa Kulaumiwa ? na kwanini Mauaji hayo yakumbukwe?

Hujjatul Islamu, Sheikh Ayub Rashid anaandika haya yafutayo kujibu swali hilo hapo juu

Mauji ya Imam Hussein, nani wa kulaumiwa? Na kwa nini yakumbukwe?

Ilikuwa tarehe 7 Muharram 61 AH ipokuja amri ya kuzuia maji yasiwafikie watu ya kambi ya Imam Hussein na wenzake! Wao walikuwa katika ardhi ya Karbala.Walikaa hivyo bila ya maji kwa muda wa siku tatu!

Asubuhi ya tarehe 10 Muharram 61 AH ilikuja amri kupitia kwa mwanajeshi mwenye amri ya yote siku hiyo, huyo hakuwa mwingine bali Umar bin Saad, mtoto wa swahaba Saad bin Abi Waqqas. Huyu aliteuliwa na Ubeidullah bin Ziyaad, kuliwakilisha kundi la Yazid dhidi ya mjukuu wa Mtume (saw).Amri aliyopewa Umar bin Saad ni kumlazimisha Imam Hussein kutoa baia kwa Yazid, na kama akikataa basi auwawe! Yaani Imam Hussein mjukuu wa Mtume amuunge mkono Yazid kama kiongozi wake! Imam Hussein alikataa amri hiyo!

Wakati hayo yote yakiendelea, mwanajeshi mmoja aliyejuliakana kama Hur bin Yazid al Riyaahi alijikuta haamini aliyokuwa akiyasikia yakiamuliwa ya kumuua imam Hussein, mjukuu wa Mtume.Mazungumzo yakaanza ya pande mbili, kambi ya Umar bin Saad na ya Imam Hussein,hiyo ikiwa ni siku ya 10 Muharram, siku ijulikanayo kama Ashura, katika mwaka wa 61 wa Hijiriyyah.

Kambi ya Yazid ikiongozwa na Umar bin Saad ikimtaka Imam Hussein kutoa baia (Kiapo cha utii) kwa Yazid, na Imam Hussein alikataa ombi hilo kata kata! Kwa sababu kubwa kuwa Yazid hakuwa na sifa za kuwa kiongoz wa Waisilamu. Yazid alikuwa mtu fasiq (muovu)!

Ndipo ilipofika baada ya Adhuhuri ikaja amri ya kuanza vita! Mshale wa kwanza ukatupwa kutokea katika kambi ya Kina Yazid dhidi ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saww).

Mapigano

Kabla ya mapigano hayaja anza, yule mwanajeshi, Hur bin Yazid al Riyaahi, alipo ona kuwa wenzake wameazimia kumpiga vita Imam Hussein, na baada ya kuzungumza nao na kuona kuwa maamuzi yao ni ya kweli, aliamua kuikimbia kambi yake na kujiunga na kambi ya Imam Hussein. Rehema ya Allah iwe juu yake.

Mapigano yaka anza ya mtu mmoja mmoja, waka uana wengi wa pande mbili. Jeshi la Yazidi likiua kwa kuwa ni amri ya Yazid dhidi ya waliokosa kutoa baia, na la Imam Hussein likipigana na maadui wa mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) kwa kujihami. Lakini kwa kuwa jeshi la Yazid lilikuwa kubwa mno kulinganisha na jeshi la wafuasi wa Imam Hussein, jeshi la watu 72 Au watu 100 na kidogo. Takriban watu wote wanaume waliokuwa wakimuhami Imam Hussein waliuliwa.

Mwisho wa Imam Hussein

Baada ya kubakia pekee yake, Imam Hussein alipigana kiume kujilinda na kujihami na maadui hao, lakini alizidiwa nguvu na majangili hao wengi.

Mwisho aliangushwa chini kwa kupigwa na mti wa chuma, na pia baada ya kupigwa na jiwe kubwa. Akiwa hapo chini aliomba maji ya kunywa, lakini, mjukuu wa Mtume (saw) hakupewa na badala yake akawa akipigwa mateke na kutukanwa matusi makubwa makubwa.

Mwisho Umar bin Saad akatoa amri; “Mmalizeni”!

Ndipo alipokuja Shimri bin Dhil Jaushan, kama wana historia wengi walivyo eleza. Shimri akiwa ameshika kisu kikubwa! Akashika ndevu za Imam Hussein, akaweka kisu hicho kwenye shingo ya mjukuu wa Mtume! Aka anza kukikata…mpaka akakitenganisha na mwili wake!

Inna lillahi wa inna ilaihi rajiuun!

Kichwa cha Imam Hussein

Maharamia hao, laana ya Mola iwe juu yao! Wakakitundika kichwa cha mjukuu wa Mtume juu ya mkuki! Wakakata na vichwa vya wafuasi wengine wa Imam Hussein, wakavitundika kwenye mikuki! Wakachoma moto kambi ya Imam Hussein, wakawateka wanawake waliokuwemo humo! Akiwemo mjukuu wa Mtume, bibi Zainab binti Ali bin Abi Twalib, Wakawapeleka kwa liwali au gavana Ubeidullah bin Ziyaad, katika mji wa Kufa.

Ubeidullah bin Ziyaad

Gavana huyu wa Yazid aliyekuwa katika mji wa Kufa, katika nchi ya Iraq, alifurahi sana kukiona kichwa cha mjukuu wa Mtume kimekatwa na vichwa vingine vimepangwa pembeni na wanawake wametekwa nyara. Akatoa maneno mengi ya kashfa na matusi!

Mwisho, akaamua kichwa cha Imam Hussein na vingine vilivyokuwa hapo, pamoja na wanawake hao na mwanamume mmoja tu aliyesalimika kuuliwa siku hiyo, wapelekwe Shaam kwa Yazid bin Muawiya. Huyo aliyesalimika alikuwa ni Ali bin Hussein maarufu kama Imam Sajjad.

Safari ya Shaam ika anza kuelekea kwa Yazid, na hii ilikuwa ni safari ya shida na madhila makubwa kwa walioitwa mateka!

Shaam

Msafara huo wa mateka ulipofika Shaam, watu waliamuriwa wajipange kusherehekea kushindwa kwa wapinzani wa Yazid, amir wa waisilamu, kama alivyo itwa!

Pindi Yazidi alipopelekewa kichwa cha Imam Hussein, alichukua fimbo, akapiga piga mdomo wake, huku akisema “hiki ndicho kimdomo alichokuwa akikibusu Muhammad’!

Akasema maneno ya kufru, kuwa yote hayo ni kisasi cha kulipiza mauaji ya mababu zake waliouliwa katika vita vya Badr! Laiti wangelikuwa hai wangelishuhudia mapigo yake!

Inna Lillahi wa inna ilaihi rajiuun!

Kwa nini kumlilia Hussein na sio Hassan?

Baadhi ya watu wameuliza kwa nini kumlilia Hussein na sio kumlilia ndugu yake Hassan au mashahidi wengine waliouliwa kabla yake?

Majibu

Kila mtu mwenye hisia za kibinadamu humlilia Hussein kwa namna alivyouliwa kinyama yeye pamoja na waliokuwa nao. Na kumlilia Hussein alianza babu yake, Mtume Muhammad (saw) kama ilivyokuja katika Hadith ya bibi Ummu Salama, mke wa Mtume (saw).

Na wafuasi wa Ahlulbayt huwalilia wote katika maimamu wao waliouliwa kishahidi na kwa dhulma. Huanza kwa kumlilia Mtume, kisha Ali bin Abi Twalib, kisha Hassan bin Ali na kisha Hussein na wale waliomfuatia miongoni mwa viongozi waliokuja baada yake.

Na hayo unaweza kuyashuhudia katika misikiti ya Mashia na katika kalenda zao ambazo huandika siku za maadhimisho ya kuzaliwa kwa maimamu wao na kuomboleza vifo vyao. Kwa hivyo si kweli kuwa wao humlilia Hussein peke yake!

Kwa nini ikawa msiba wa Imam Hussein umapewa siku nyingi zaidi?

Majibu

Ni kwa sababu ya kuelezea jinsi ya dhulma aliyofanyiwa mjukuu wa Mtume na wale waliodai kuwa wao ni watawala waadilifu wa Kiislamu. Na jinsi watawala hao walivyowalaghai watu na kuwadanganya kwa hila mbali mbali.

Na kuomboleza huku ni kueleza namna Umma ulivyokuwa umelala wakati huo mpaka ukaruhusu mjukuu wa Mtume auwawe kinyama, na kichwa chake kitundikwe katika mkuki na kipitishwe mitaani na watu kushangilia.

Na pia kuelezea namna Yazid, aliyekuwa ‘Amir al Muminin’, alivyokifanyia istihzai kichwa hicho kitukufu! Hayo yote hayatoshi kuomboleza kwa siku moja tu!

Sasa hivi msiba huu unaombolezwa kwa siku unazo ombolezwa ili kuwazindua watu kutoka katika ghafla waliyokuwemo ndani yake! Kwani kuna waisilamu wengi leo hata hawamjui Hussein alikuwa nani? Na Yazid alikuwa nani? Wala hawamjui muovu Ubeidullah bin Ziyad aliyetumwa na Yazid kusimamia mauaji ya mjukuu wa Mtume alikuwa ni mtu wa aina gani na aliamrisha maovu makubwa kiasi gani?

Historia ya kuuliwa Hussein mjukuu wa Mtume ni historia muhimu sana kujulikana leo, ili watu wasije kudanganyika na kuwafuata viongozi kama kina Yazid ambao hawakuwa na sifa ya kuongoza Umma wa Mtume Muhammad, swallallahu alaihi wa aalihi wa sallam.

Naamini hata haya tunayoyaelezea hapa wako watu wengi hawayajui!

Ya Allah tuonyeshe haki kuwa ni haki na uturuzuku kuifuata, na utonyeshe batwil kuwa ni batwil na utuwezeshe kuiepuka.

Imeandikwa na Hujjatul Islam,

Sheikh Ayub Rashid

 

 

elbinawi

To interact with humanity & share ideas...

felicity114

felicity is the purpose of everybody

Ladakh Express

Ladakh's 1st political and cultural online journal.

Islamic Library

Shia Islamic PDFs - Now in Collaboration with ShiaTranslate.org!

zahraa Foundation

Fatima bint Muhammad is the Symbolization of Women's Power in Islam

mmubaraka1

A fine WordPress.com site

The Pilgrim Log

Helping you live your daily pilgrimage

World Shia Forum

Identity, Equality, Unity

Source of Inspiration

All is One, co-creating with the Creator

Bill Langill's Blog

Love is the Answer

Interrupting the Silence

An Episcopal Priest's Sermons, Prayers, and Reflections on Life, Becoming Human, and Discovering Our Divinity

Morgan L. Busse

In Darkness there is Light

YOGA

When unconscious became conscious this is Samadhi

Zoroastrians.net

Parsis, Iranis, Zarathushtis, All Under One Roof

Islamic Laws

Raising Awareness on Fiqh and the Ulema

Tech Cloud

Imagine | Innovate | Implement

Mujtaba Somji

Islamic sayings

%d bloggers like this: