Blog Archives

Ghadir Katika Miongozo ya Ayatullah Udhma Khamenei

1360103/12/2009
Tukio la Kihistoria la Ghadir

Umuhimu wa Sikukuu ya Ghadir Khum

Umuhimu wa Kuwepo Usimamiaji na Uongozaji Unaotakiwa

Uhakika Ulio Wazi na Uliojificha wa Ghadir

Maana ya Wilaya katika Tukio la Ghadir

Maana ya Uimamu katika Ghadir

Ghadir na Suala la Umoja wa Umma wa Kiislamu

Tukio la Kihistoria la Ghadir [1]

Watu wote wanaofuatilia na wanaopenda kujua masuala ya historia ya Uislamu ni vyema wakijua kuhusu asili ya tukio la Ghadir kwamba tukio hilo limetokea kweli, na hakuna shaka hata chembe juu ya kutokea kwake. Aidha si Waislamu wa Kishia pekee walionukuu tukio hilo, bali wapokezi wa Kisuni pia, iwe ni katika vipindi vya huko nyuma kabisa, au katika vipindi vya katikati vya historia ya Kiislamu, wao aidha wamenukuu habari za kutokea tukio hilo. Yaani wote wamenukuu habari zisemazo kwamba tukio hilo lilitukia katika safari ya Hijjatul Wadaa [2], Hija ya Mwisho ya Bwana Mtume Muhammad SAW katika eneo linaloitwa Ghadir Khum. Wapokezi hao wa pande zote wamepokea kuwa, wakati msafara mkubwa wa Waislamu ambao walihiji na Bwana Mtume walipokuwa wanarejea Madina, baadhi yao wakiwa wameshatangulia mbele, Mtume Muhammad SAW aliwatumia wajumbe ili warejee nyuma, naye aliwasubiri hadi wote walipofika sehemu alipokuwepo. Mjumuiko mkubwa wa Waislamu ulikusanyika katika eneo hilo, baadhi ya wapokezi wanasema walikuwa ni watu elfu 90, wengine wanasema walikuwa ni laki moja na wengine wanasema Waislamu waliokusanyika hapo walikuwa ni laki moja na 20 elfu. Hali ya hewa wakati huo ilikuwa ya joto kali kiasi kwamba watu waliokuwa wakiishi Jaziratul Arab, ambao wengi wao ni wakazi wa majangwani waliozoea hali ya joto, wao pia walishindwa kuvumilia joto la sehemu hiyo. Ardhi ilikuwa inafuka moto na hivyo walilazimika kuvua majoho yao na kuyaweka chini ya miguu yao ili waweze kupunguza ukali wa joto hilo. Nukta hii imezungumziwa pia na wapokezi wa Kisuni. Baadaye Bwana Mtume Muhammad SAW alisimama na kumtaka pia Amirul Muminin Ali AS asimame, halafu alisimama juu ya kijukwaa na kuunyanyua mkono wa Imam Ali AS akisema:

«من كنت مولاه فهذا على مولاه، اللهم وال من والاه و عاد من عاداه»

Mtu ambaye mimi ninamsimamia mambo yake, (yaani ambaye mimi ni kiongozi wake) basi na huyu Ali naye anamsimamia mambo yake. Mwenyezi Mungu kuwa pamoja na aliye pamoja na Ali na kuwa adui wa anayemfanyia uadui Ali.

Tab’an maneno hayo yapo katikati ya maneno mengine yaliyotangulia na yaliyokuja baada ya matamshi hayo yaliyomo kwenye hotuba ndefu ya Bwana Mtume aliyoitoa siku hiyo. Hata hivyo sehemu hiyo ndiyo muhimu zaidi ambayo ndani yake Bwana Mtume Muhammad SAW alitangaza Wilaya – yaani utawala wa Kiislamu – kwa njia rasmi na ya wazi kabisa, na alimtangaza Amirul Muminin Ali AS kuwa mtu aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo. Hilo limezungumzwa pia kwa uwazi na ndugu zetu wa Kisuni katika vitabu vyao vinavyokubalika – wala si katika kitabu kimoja au viwili tu, bali katika makumi ya vitabu vinavyokubalika. Marhum Allama Amini amevijumuisha vitabu hivyo katika kitabu chake cha al Ghadir. Mbali na hivyo pia, kuna vitabu vingine mbalimbali kuhusu suala hilo.

Umuhimu wa Sikukuu ya Ghadir Khum

Ni jambo lisilo na shaka kwamba sikukuu ya Ghadir ina umuhimu mkubwa. Umuhimu wa siku hiyo umepokewa katika hadithi mbalimbali za Kiislamu na tunaweza kusema hata zaidi ya hadithi zinazohusiana na Idul Fitr na Idul Adh-ha. Hii haina maana kwamba umuhimu wa idi hizo mbili kubwa za Kiislamu ni mdogo au umepungua, hapana, bali ni kwa sababu idi hii ya Ghadir inahusiana na kitu kimoja muhimu zaidi. Kwa mujibu wa Hadithi za Kiislamu kinachofanya Idul Ghadir kuwa na umuhimu mkubwa ni kwa kuwa inahusiana na suala la Wilaya yaani uongozi wa Kiislamu. Labda tunaweza kusema kuwa, lengo la kazi yote kubwa ya Mitume na watu wakubwa wa dini na Manabii wa Mwenyezi Mungu (rehema na amani ziwaendee wote) ni huko kusimamisha Wilaya ya Mwenyezi Mungu. Ushahidi wa hayo umo katika Hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imam Sadiq AS ambaye anasema kuhusu nafasi ya lengo la jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu na jitihada nyinginezo katika dini kwamba lengo lake ni:

«ليخرج الناس من عبادة العبيد الى عبادت الله و من ولايت العبيد الى ولايت الله»

Yaani watu waweze kutoka kutoka katika ibada ya kiumbe na waingie katika ibada ya Mwenyezi Mungu na watoke kwenye Wilaya na uongozi wa kiumbe na waingie chini ya Wilaya na uongozi wa Mwenyezi Mungu.

Naam lengo ni kuwa watu watoke chini ya udhibiti na uongozi wa viumbe kwa maana yake pana na halisi na waingie chini ya uongozi wa Mwenyezi Mungu tu. Amma katika sikukuu ya Ghadir kuna na nukta nyingine muhimu nayo ni kwamba kuna mawanda aina mbili katika suala la Wilaya; mosi ni uwanda wa nafsi ya mwanaadamu yaani mwanaadamu mwenyewe aweze – kwa msaada wa Mwenyezi Mungu – kuidhibiti na kuiweka chini ya Wilaya nafsi yake yaani kuiweka nafsi yake hiyo chini ya udhibiti na Wilaya ya Mwenyezi Mungu na uwanda wa pili ni kuwa aweze kuyaingiza mazingira ya maisha yake chini ya utawala na Wilaya ya Mwenyezi Mungu. Hii ina maana kuwa, jamii ya mwanaadamu inatakiwa iende kwa mujibu wa uongozi wa Mwenyezi Mungu. Kusiwe na Wilaya yoyote itakayoweza kuizuia jamii kuwa chini ya utawala na Wilaya ya Mwenyezi Mungu, si Wilaya ya fedha, si Wilaya ya kabila na kaumu fulani, si Wilaya ya kutumia mabavu, si Wilaya ya mila, desturi na ada ghalati bali utawala pekee uwe wa Mwenyezi Mungu.

Mtu aliyetangazwa siku hiyo, ni mtu mtukufu, Imam Ali AS, walii wa wachaji Mungu ambaye ni kigezo bora cha kuigwa katika mawanda yote mawili ya Wilaya. Naam katika uwanda wa Wilaya ya nafsi binafsi ya mja na na suala zima la mtu kuidhibiti nafsi yake hiyo nao ndio huo uwanda wa kwanza wa Wilaya, na pia katika ruwaza na mfano aliouonyesha wa utawala wa Kiislamu wa Wilaya ya Mwenyezi Mungu katika miaka michache aliyotawala mtukufu huyo. Kigezo kilichoonyeshwa na mtukufu huyo kimebakia kuwa ruwaza njema hadi leo hii na kitaendelea kuwa hivyo katika historia kiasi kwamba mtu yeyote anayetaka kuijua vyema Wilaya ya Mwenyezi Mungu, anaweza kupata kigezo kilichokamilika kutoka kwa mtukufu huyo.

Umuhimu wa Kuwepo Usimamiaji na Uongozaji Unaotakiwa

Suala la Ghadir na hatua ya Mtume Muhammad SAW ya kumtangaza Amirul Muminin Ali bin Abi Talib AS kuwa kiongozi wa kusimamia na kuendesha masuala ya uma wa Kiislamu ni tukio kubwa na lenye umuhimu wa aina yake katika suala zima la kuhusika moja kwa moja Mtume Muhammad SAW katika masuala ya uongozi wa jamii ya Kiislamu. Maana ya hatua hiyo iliyochukuliwa na bwana Mtume siku ya mwezi 18 Mfunguo Tatu Dhilhijjah mwaka wa 10 Hijria ni kwamba Uislamu unalipa umuhimu mkubwa suala la uongozi wa jamii. Kadhia ya Uongozi katika mfumo wa Kiislamu na katika jamii ya Kiislamu si kitu cha kuachiliwa vivi hivi kingie mikononi mwa mtu yeyote tu asiye na sifa zinazotakiwa. Na sababu yake ni kuwa uongozi wa jamii ni moja ya mambo yanayoacha athari kubwa sana katika jamii. Kuteuliwa Amirul Muminin Ali bin Abu Talib AS kubeba jukumu hilo na ambaye ni nembo ya ucha Mungu, elimu, ushujaa, kujitolea katika njia ya Mwenyezi Mungu na uadilifu kati ya masahaba wa Bwana Mtume Muhammad SAW; kunazidi kuuweka wazi upeo mkubwa wa umuhimu wa jambo hilo. Uislamu hapo unatuwekea wazi kwamba sifa za kiongozi wa Kiislamu zinapaswa ziwe kama hizo alizojipamba nazo Imam Ali AS. Hata wale watu ambao hawakubali kwamba Imam Ali alikuwa wasii wa Bwana Mtume wa kuchukua uongozi mara baada ya kufariki dunia Mtume Muhammad SAW, nao hawana shaka hata chembe juu ya elimu, ucha Mungu, taqwa na ushujaa wa mtukufu huyo pamoja na kujitolea kwake katika njia ya Allah na katika kupigania haki na uadilifu. Waislamu wote wanaomtambua Amirul Muminin Ali bin Abi Talib AS wanakubaliana kwamba sifa hizo zilikuwa zimejikita katika shakhsia ya mtukufu huyo, Imam Ali AS. Aidha hatua hiyo inaonyesha ni aina gani ya jamii ya Kiislamu inayotakiwa na Uislamu na Bwana Mtume na ni uongozi wa aina gani unaopaswa kufanywa kuwa ndilo lengo la kupiganiwa.

Uhakika Ulio Wazi na Uliojificha wa Ghadir

Kuna uhakika mwingi umejikita ndani ya tukio la Ghadir. Ukweli wa tukio hilo ni kwamba kazi iliyofanywa na Bwana Mtume Muhammad SAW kwa ajili ya jamii changa ya Kiislamu ya wakati huo ambayo iliundika katika kipindi cha miaka kumi hivi tangu ulipopata ushindi Uislamu, ilikuwa ni kutatua suala la serikali, uongozi na Uimamu kwa maana yake pana na ndio maana katika tukio la Ghadir Khum baada ya kutekeleza ibada yake ya mwisho ya Hijja na wakati alipokuwa anarejea Madina, aliwatangazia Waislamu mtu wa kushika nafasi yake, naye ni Amirul Muminin Ali bin Abi Talib AS. Hata hii dhahiri ya tukio hilo pekee ambayo tab’an ni muhimu sana, pia ina mazingatio makubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya watu ambao wanayafanyia utafiti na kuyafuatilia masuala ya jamii ya kimapinduzi. Lakini pia kuna uhakika mwingine mkubwa umejificha ndani ya tukio hilo ambapo kama uma na jamii ya Kiislamu itaziangalia kwa kina nukta za uhakika huo, basi itafanikiwa kupata njia bora na ya wazi ya maisha. Kimsingi ni kwamba kama tukio la Ghadir litachukuliwa na Waislamu wote – wawe Waislamu wa Kishia ambao wanalijua vyema tukio hilo katika upande wake wa uongozi, uimamu na Wilaya, au Waislamu wengine ambao pamoja na kwamba wanakubali kuwa tukio hilo lililotokea lakini hawaliangalii kwa sura ya uongozi, uimamu na Wilaya – kama wote hao leo hii watazitilia maanani na kuzizingatia sana zile nukta muhimu zilizojikita katika tukio la Ghadir, basi wataweza kuwaletea mafanikio mengi Waislamu wote duniani.

Miongoni mwa nukta hizo ni kwamba mosi huko kuteuliwa tu mtu mtukufu kama Imam Ali kuwa kiongozi wa Waislamu, pekee kuliweka wazi vigezo anavyopaswa kuwa navyo kiongozi wa Kiislamu. Katika tukio hilo Mtume Muhammad SAW aliwateulia Waislamu mtu wa kuwaongoza ambaye alikuwa amekamilika katika sifa na thamani zote za Kiislamu. Alikuwa ni mtu muumini, aliyekuwa na kiwango cha juu kabisa cha taqwa na ucha Mungu, mwenye kujitolea katika njia ya Uislamu, ambaye hakuwa na tamaa hata chembe na mambo ya kidunia, aliyepata uzoefu na kushinda mitihani katika nyanja zote: nyanja hatari, nyanja za elimu na maarifa, nyanja za kutoa hukumu na kadha wa kadhalika. Yaani hatua ya Bwana Mtume SAW ya kumtangaza Amirul Muminin Ali AS kuwa kiongozi; awe Imam na walii wa Waislamu; kunawafunza Waislamu wote wa kipindi kizima cha historia kwamba mtawala wa Kiislamu lazima awe mtu ambaye atakuwa amepambika na sifa hizo hata kama hazitakuwa na ukamilifu kama aliokuwa nao Imam Ali AS. Maana ya maneno hayo ni kwamba mtu ambaye hana sifa hizo katika jamii za Kiislamu, ambaye hana welewa wa Uislamu, ambaye hatendi mambo yake kwa mujibu wa Uislamu na asiyezingatia jihadi, kutoa na kujitolea katika njia ya Uislamu, ambaye hana huruma wala unyenyekevu kwa waja wa Mwenyezi Mungu na ambaye hakujipamba kwa sifa yoyote katika sifa hizo za Amirul Muminin Imam Ali AS, mtu huyo hana haki ya kuongoza jamii za Kiislamu. Hilo ndilo alilotaka kutufunza Bwana Mtume na sifa na vigezo hivyo ndivyo ambavyo mtukufu huyo aliwabainishia Waislamu. Kwa kweli hilo ni somo lisiloweza kusahaulika.

Nukta nyingine ambayo tunaweza kuipata katika tukio la Ghadir ni kuwa, Amirul Muminin Ali bin Abi Talib AS hata katika ile miaka michache aliyojaaliwa kutawala na kuongoza jamii ya Kiislamu, alionyesha kivitendo jambo linalopaswa kupewa kipaumbele na kiongozi wa nchi na jamii, nalo ni uadilifu wa Mwenyezi Mungu na wa Kiislamu. Yaani uadilifu; yaani kufanikisha lengo ambalo Qur’ani imelieleza kuwa ndiyo shabaha ya kutumwa Mitume na Manabii na kuteremshwa Vitabu na sheria za Mwenyezi Mungu. Qur’ani Tukufu inasema kuhusu jambo hilo kwamba:

لِيَقُومَ النَّاسُ بِالْقِسْطِ

Ili wasimame watu katika uadilifu. al Hadidi (57:25)

Yaani uadilifu wa Mwenyezi Mungu usimame. Kwa hakika insafu na usawa kama ulivyoainishwa na Uislamu, ndiyo njia bora kabisa ya kudhamini na kuleta uadilifu na utangamano katika jamii. Kwa mtazamo wa Imam Ali bin Abi Talib AS, hilo ndilo jambo la kupewa kipaumbele cha kwanza katika uongozi.

Maana ya Wilaya katika Tukio la Ghadir

Katika tukio la Ghadir, Bwana Mtume Muhammad SAW alitekeleza moja ya majukumu yake makubwa kwa mujibu wa amri ya Mwenyezi Mungu iliyokuja katika Qur’ani Tukufu kama aya inavyosema:

وَإِن لَّمْ تَفْعَلْ فَمَا بَلَّغْتَ رِسَالَتَهُ

…na kama hukufanya basi utakuwa hukufikisha ujumbe Wake. al Maida (5:67)

Naam suala la kuteuliwa Amirul Muminin Ali AS kuwa walii na khalifa wa Waislamu lilikuwa muhimu kiasi kwamba kama Bwana Mtume asingelilifanya basi ingelikuwa ni sawa na kuwa hakufikisha risala na ujumbe aliotumwa na Mwenyezi Mungu kuufikisha! Yamkini makusudio ya aya hiyo ni kwamba atakuwa hakufikisha risala na ujumbe aliotumwa kuufikisha kuhusu amri hiyo yenyewe ya kumtangaza Imam Ali AS kuwa khalifa baada yake, kwani Mwenyezi Mungu amemuamrisha atekeleze wajibu huo. Aidha yamkini makusudio yakawa ni ya juu zaidi ya hivyo, kwa maana ya kwamba angelikuwa hakufikisha risala na ujumbe wote aliotumwa na Mwenyezi Mungu akiwa Mtume Wake kwa walimwengu, yaani kazi yote aliyotumwa ingeliingia dosari na doa kama asingelimtangaza Imam Ali AS kuwa kiongozi wa Waislamu baada yake. Uko uwezekano kwamba hiyo ndiyo maana ya maneno hayo ya Mwenyezi Mungu. Yaani ingelikuwa ni kana kwamba asili ya ujumbe wenyewe wa Utume haikufikishwa kwa walimwengu! Na kama tutasema ni hivyo, basi umuhimu wa tukio la Ghadiri utakuwa mkubwa maradufu. Yaani suala la kuunda serikali, suala la Wilaya na utawala wa Kiislamu ni jambo ambalo limo katika matini asili ya dini na mafundisho ya Bwana Mtume Muhammad SAW na limepewa umuhimu mkubwa na tunaona jinsi Bwana Mtume alivyolitekeleza na kulifikisha mbele ya macho ya matabaka mbalimbali ya watu kwa hima na namna ambayo pengine hakuna wajibu wowote mwingine alioufikisha namna hiyo! Si Sala, si Zaka, si Funga na si Jihadi! Katika kuzifikisha kwa watu ibada na nguzo zote hizo za Mwenyezi Mungu, Bwana Mtume hakufanya kama alivyofanya katika upande wa Uimamu na utawala wa Waislamu. Yaani aliwakusanya watu wa matabaka tofauti, wa makabila mbalimbali na wa maeneo yote katika makutano ya njia za baina ya Makka na Madina kwa nia ya kufikisha amri hiyo ya Mwenyezi Mungu. Jambo hilo likaenea katika ulimwengu mzima wa Kiislamu ya kwamba <>

Maana ya Uimamu katika Ghadir

Uimamu ni kilele cha maana inayotakiwa ya kuongoza jamii mbele ya anuwai kwa akisami za tawala za kibinaadamu zilizojaa udhaifu, hawaa za nafsi, ushaufu na kupenda jaha. Uislamu umemwonyesha mwanaadamu nuskha na namna ya Uimamu unavyopaswa kuwa. Yaani kiongozi inabidi awe mtu ambaye moyo wake umejaa baraka za uongofu wa Mwenyezi Mungu na awe na utambuzi kamili wa masuala ya dini. Yaani aweze kuainisha njia na kuongoza sirati vizuri, na awe na nguvu na uwezo mkubwa wa kiutendaji. Qur’ani Tukufu inasema:

يَا يَحْيَى خُذِ الْكِتَابَ بِقُوَّةٍ

Ewe Yahya! Kishike Kitabu kwa nguvu… Surat Maryam (19:12)

Aidha kiongozi anapaswa kuwa mtu ambaye hatajali zaidi nafsi yake, matakwa yake na maisha yake binafsi, bali roho, maisha na mafanikio ya wengine ndiyo yawe na umuhimu zaidi kwake. Jambo hilo lilionyeshwa kivitendo na Amirul Muminin Ali bin Abi Talib AS katika kipindi cha chini ya miaka mitano ya utawala wake. Naam, mnashuhudia wenyewe jinsi Imam Ali AS alivyofanikiwa katika kipindi kifupi cha chini ya miaka mitano kuunda na kuendesha serikali ambayo imekuwa ni kigezo na ruwaza bora isiyosahaulika kwa mwanaadamu na licha kupita karne nyingi tangu wakati huo, lakini hadi leo hii utawala huo umebakia hai na unang’ara mithili ya mbaamwezi. Hayo ndiyo matunda ya somo, maana na tafsili ya kweli ya tukio la Ghadir.

Ghadir na Suala la Umoja wa Umma wa Kiislamu

Kadhia ya Ghadir nayo inaweza kuwa chanzo cha kuleta umoja na mshikamano kati ya Waislamu. Yamkini mtu akaona kitu hicho ni cha ajabu na hakiwezekani, lakini huo ndio ukweli wenyewe. Suala lenyewe la Ghadir ukiachilia mbali ule upande ambao Waislamu wa Kishia wanauhesabu kuwa ni itikadi yao – yaani kuteuliwa Amirul Muminin Ali AS kuwa mtawala wa Waislamu baada ya Bwana Mtume Muhammad SAW kama inavyosema wazi hadithi ya Ghadir – kuna kitu kingine kinaonekana wazi katika tukio hilo nalo ni suala lenyewe la Wilaya na utawala wa Kiislamu. Suala hili la utawala wa Kiislamu halihusiani na Mashia au na Masuni peke yao. Kama leo Waislamu duniani, na kama mataifa yote ya Kiislamu yatashikamana katika kalima moja na iwapo wote watakuwa na kaulimbiu moja ya kusimamisha Wilaya na utawala wa Kiislamu, basi wataweza kufika mbali ambako hadi leo hawajafika, na watafanikiwa kuvuuka kwa fakhari vigingi vingi vinavyoukabili umma wa Kiislamu. Aidha watamudu kutatua matatizo mengi ya nchi za Kiislamu ambayo hadi leo yamekuwa vigumu kutatuka.

Tanbihi

==============

[1] Ghadir Khum ni jina la eneo lililoko baina ya Makka na Madina na lilikuwa ni makutano ya mahujaji wote. Kutokana na kuweko dimbwi la maji katika eneo hilo yaliyokusanyika kutokana na mvua, eneo hilo lilipata umashuhuri wa jina hilo la Ghadir Khum. Wakati Mtume Muhammad SAW alipokuwa anarejea Madina kutokea Makka alikotekeleza ibada yake ya mwisho ya Hija aliwakusanya mahala hapo Waislamu wote waliohiji naye na kumtangaza Ali bin Abi Talib kuwa ni wasii, ndugu na mtu wa kushika nafasi yake baada ya yeye kufariki dunia na kwamba hiyo ilikuwa ni amri kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Maneno maarufu yasemayo: Kila mtu ambaye mimi ni walii na kiongozi wake, basi na huyu Ali ni kiongozi wake ni sehemu ya hotuba ndefu aliyoitoa Bwana Mtume Muhammad SAW katika tukio hilo la Ghadir na imethibitishwa na kutiliwa mkazo na Waislamu wote wa Kisuni na Kishia.

[2] Tangu mwanzoni mwa Mfunguo Pili mwaka wa 10 Hijria ambayo ilisadifiana na mwaka wa mwisho wa maisha ya duniani ya Mtume Muhammad SAW, mtukufu huyo aliwatangazia Waislamu wa maeneo yote na wa makabila yote ya Hijaz (Saudi Arabia ya hivi sasa) kwamba mwaka huo aliazimia kwenda kuhiji Hija yake ya mwisho pamoja na kufanya Umra. Waislamu wengi mno waliungana na Bwana Mtume katika ibada hiyo na hivyo huo ukahesabiwa kuwa mjumuiko mkubwa zaidi kuwahi kukusanyika pamoja Waislamu katika zama hizo. Hija hiyo ni maarufu kwa jina la Hijjatul Wadaa.

Eid Al-Ghadir

Uteuzi wa Imam Ali (s.a) kuwa Mrithi wa Mtume

ghadirMiezi michache kabla ya kifo cha Mtume Muhammad (saw), alifanya hijja ya mwisho Makka ilijulikana kwa jina “Hijja ya kuaga”.  Akiwa anarejea Madina, msafara wake ulifikia eneo linalojulikana kwa jina “ Ghadir Khum” na ni katika eneo hilo alipokea ufunuo (Wahayi). Malaika mleta wahyi Jibril alishuka na kumletea mtume ujumbe kutoka kwa Mola wake: “Ewe Mtume! Fikisha kile ambacho kimeteremshwa kwako kutoka kwa mola wako; na usipofikisha, basi utakuwa hujafikisha ujumbe, na Hakika Allah atakulinda na watu; hakika Allah haongozi watu wasio na Imani”

Hivyo basi Mtume Muhammad (saw) akasimama eneo hilo la Ghadir Khum na kuamuru msafara wake kusimama hapo, Joto lilikuwa kali sana kiasi watu iliwabidi kufunga sehemu za miguu yao kwa nguo zao kwani Ardhi yote ilikuwa na joto kali sana.

Mtume Muhammad (saw) akaongoza swala ya jamaa, na kasha jukwaa likaandaliwa na mtume (saw) akapanda jukwaa hilo, Wanahistoria wanasimulia kuwa idadi ya waliohudhuria mkusanyiko huo walikuwa watu laki moja (100,000) au zaidi. Wote wakisikiliza kwa umakini nini mtume alitaka kuwaambia. Mtume akaanza kwa kuwaelezea juhudi alizozifanya katika kuwaongoza na akazitaja baadhi ya hukumu za kiislamu.
Katika hotuba yake hiyo, Mtume (saw) akataja hadithi ya Vizito viwili;akisema

“Inaonekana muda umewadia ambapo nitapokea wito kutoka kwa mola wangu na sinabudi kuukubakuliu wito huo. Ninakuachieni vizito viwili vyenye thamani kubwa, kama mtashikamana navyo vypote viwili, hamtapotea baada yangu. Vizito hivyo ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Watu wa kizazi changu (Ahlulbayt) Vizito hivi wiwili havitatengana  mpaka vinijie katika kisima (peponi)”

Kisha mtume akaendelea kusema:

“ Je mimi sina haki Zaidi kwa waumini kuliko haki walizonazo kwa nafasi zao”

Watu waliokusanyika wakajibu:

“Ndio bila shaka ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu”

Kisha mtume (saw) akaushika mkono wa Imam Ali (sa) na kuunyanyua juu kuuonyesha kwa watu kasha akaamuru kwa kusema:

“Yeyote yule ambaye mimi ni Bwana wake, Basi Ali ni bwana wake”

Kisha akasema: “Ewe Mola wangu! Mfanye rafiki atakayemfanya rafiki Ali! Na kuwa Adui na atakayemfanya Adui Ali! Ewe mola wangu mpende yule atakayempenda yeye na Mchukia yule atakaye mchukia Ali
Baada ya hotuba hii na uteuzi huo; Waislamu wote waliokusanyika wakamuelekea Imam Ali (as) na kumpa pongezi za uteuzi huo.

Zaidi ya hapo, baada ya kumalizika hotuba ya Mtume. Hassan ibn Thabit, Swahaba na Mshairi wa mtume (saw) akaomba ruhusa kwa mtume asome shairi lakle alilolitunga kwa ajili ya Imam Ali (as), Mtume (saw) akampa ruhusa; naye Hassan akalisoma shairi lake;

Aliwaita katika siku ya Ghadiri Mtume wao

Hapo Khum, hivyo sikiliza na zingatia Wito  wa mtume,

Alisema; Ni nani Bwana na Mtume wako?

Wakasema. Kwa uwazi Bila kuwa na kigugumizi

Mola wako, ndiye Bwana wetu, na wewe ndiye Mtume wetu

Na hutopa kwetu katika hilo upingaji

Akamwambia: Simama ewe Ali ninafuraha kukutangaza wewe kama Imam na Kiongozi baada yangu, Kwa hiyo yeyote ambaye nilikuwa Mimi ni kiongozi wake basi huyu ni kiongozi wake, Hivyo kuwa Msaidizi wake kwa Haki na Utii

Na katika siku hiyo hiyo Allah akashusha Aya katika Qurani tukufu ikisema:

Leo nimekukamilishieni dini yenu na nimetimiza neema yangu kwenu,  na nimeridhia Uislam uislamu kuwa dini yenu.

Hili ndilo Tukio la Ghadir

 

Kipindi cha tukio: Hijja ya Mwisho ya Matume

Miaka kumi baada ya Kuhama (hijrah), Mtume wa Allah [amani na baraka juu yake na kizazi chake] aliamuru wafuasi wake wa karibu kuwaita watu wote katika maeneo tofauti ili kujiunga nae katika Hijja yake ya mwisho. Katika safari hii aliwafundisha jinsi ya kutekeleza ibada ya Hijja kwa nidhamu na utaratibu sahihi.

Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Waislamu wengi kiasi hicho kukusanyika mahali pamoja mbele ya kiongozi wao, Mtume wa Mwenyezi Mungu. Njiani akielekea Makka, zaidi ya watu elfu sabini (70,000) walimfuata Mtukufu Mtume (saw). Ilipofika Siku ya nne ya Dhu’l-Hijjah Waislam zaidi ya laki moja (100,000) walikuwa wameingia mji wa Makkah.

Tarehe ya Tukio:

Tarehe ya tukio hili ilikuwa 18 ya Dhu’l-Hijjah ya mwaka 10 AH (10 Machi 632 CE).

Eneo la Tukio

Baada ya kumaliza Hijja yake ya mwisho (Hajjatul-Wada ‘), Mtume (saww) alikuwa akiondoka mji wa Makka kuelekea Madina, ambapo yeye na umati wa watu walifika mahali panaitwa Ghadir Khumm (karibu na al-Juhfah leo). Ilikuwa ni mahali hapo njia panda ambapo watu kutoka mikoa mbalimbali walikuwa wakiagana kabla ya kila mmoja kuchukua njia tofauti kuelekea majumbani mwao.

Aya iliyolazimu tukio la Ghadir

Quraa (5:67)

Wakiwa katika eneo hilo la Ghadir Khumm aya ifuatayo ilishuka

“Ewe Mtume! Fikisha uliyo teremshiwa kutoka kwa Mola wako Mlezi. Na ikiwa hukufanya hayo basi hukufikisha ujumbe wake. Na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu….” (Qur’an 5:67)

Sentensi ya mwisho katika aya hiyo hapo juu inaonyesha kuwa Mtume (saww) alikuwa akizingatia majibu ya watu wake watakayomjibu endapo atautoa ujumbe huo lakini Mwenyezi Mungu anamwambia asifadhaike, kwa kuwa atamlinda Mtume wake kutokana na watu.

Hotuba ya Mtume siku ya Ghadir

Baada ya kupokea aya hiyo, Mtume (saww) alisimama mahali hapo (Bwawa la Khumm) wakati huo kulikuwa na joto kali sana. Kisha akawatuma watu wawaite waliotangulia mbele kurudi nyuma, na kusubiri mpaka walio nyuma wote, wakafika na kukusanyika. Alimuamuru Salman [r.a] kutumia miamba na matandiko ya Ngamia kuandaa jukwaa (minbar) ili aweze kutangaza. Ilikuwa karibu wakati wa mchana Mwanzo wa msimu wa Maanguko (Fall), na kwa sababu ya joto kali katika bonde hilo, watu walikuwa wamesokota vilemba vyao kwenye miguu na mikono yao, na walikuwa wameketi karibu na mimbari, kwenye miamba iliyokuwa na joto kali.

Siku hii Mtume wa Allah (saww) alitumia saa takriban tano mahali hapo; saa tatu ambazo alikuwa kwenye mimbari. Alisoma zaidi ya aya mia moja kutoka katika Qur’ani tukufu, na kwa mara sabini na tatu aliwakumbusha na kuwaonya watu wa matendo yao na akhera yao. Kisha akatoa hotuba ndefu.

Ifuatayo ni sehemu ya hotuba yake ambayo imesimuliwa kwa kiasi kikubwa na wanazuoni wa kisunni:

Hadithi ya Vizito viwili vitakatifu (thaqalayn)

Mtume wa Allah (saww) alisema:

“….Inaonekana wakati umewadia wa mimi kuitwa (na Mwenyezi Mungu) na hakika nitajibu wito huo. Ninawachieni vitu viwili vya thamani na kama mtakamatana navyo vyote viwili, hamtaweza kupotea baada yangu, navyo ni kitabu cha Mwenyezi Mungu na Watu wa nyumba yangu, yaani, Ahlul Bayt wangu. Viwili hivyo havitatengana mpaka vije kwangu peponi.”

[Rejea: Hadith al-Thaqalayn: Utafiti wa Usahihi wake]

Kutambuliwa na kukiri mamlaka yake

Kisha mtume wa Mwenyezi mungu akaendelea: “Je, mimi sina haki zaidi juu ya waumini kuliko haki walizonazo juu yao wenyewe?”Waislamu walijibu wote kwa pamoja”Ndiyo bila shaka, Ewe ‘Mtume wa Mungu”

Tamko la mtume kumteua Mrithi wake

Kisha ikafuatiwa na sentensi muhimu iliyobainisha wazi wazi uteuzi wa Ali kuwa kiongozi wa Ummah wa Kiislamu. Mtukufu Mtume (saww) aliunyanyua juu mkono wa Ali bin Abi Talib a.s na kusema: “Kwa yeyote ambaye mimi ni Kiongozi wake (mawla), basi Ali ni Kiongozi wake (mawla).”

[Katika maelezo mengine neno lilitumiwa lilikuwa ni Wali badala ya mawla – kwa maana hiyo hiyo)

Kisha Mtume akaendelea;

“Eeh ‘Mwenyezi Mungu, wapende wale wanaompenda, na wachukie wale wanaomchukia.”].

Hizi ndio sehemu muhimu za hotuba ya Mtume. Pia kuna matoleo ya kina zaidi ya hutoba hii muhimu ya mtume ambayo yameandikwa na wanazuoni wengi wa kisunni.

Kushuka kwa Aya ya 5:3

Mara baada ya Mtume [saw] kumaliza maneno yake, aya ifuatayo ya Qur’ani ilishuka:

.. “Leo nimekukamiliishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni uislamu uwe ndiyo Dini. (5:3)

Aya hiyo hapo juu inaonyesha wazi kwamba Uislam bila kufuta suala la uongozi baada ya Mtume (saww) haujakamilika, na kukamilika kwa dini ni baada ya kutangazwa kwa mrithi wa Mtukufu Mtume.

Mshairi Hassan B. Thabit

Mara baada ya hotuba ya Mtume, Hassan b. Thabit, Sahaba na mshairi wa Mtume wa Allah (sw), aliomba ruhusa kwa mtume ya kutunga mistari michache ya mashairi kuhusu Imam Ali kwa ajili ya wasikilizaji. Mtume alisema: “Sema kwa baraka za Allah”.

Hassan alisimama akasema: “Enyi watu wa wa kabila la Quraishi.” Nilifuata kwa maneno yangu yale yaliyotangulia na kushuhudiwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu, kisha akaandika aya zifuatazo katika shairi lake:

Aliwaita siku ya Ghadir Mtume wao

Huko Khumm Sikilizeni (zingatieni) ujumbe wa Mtume (mawlakum wa waliyyukum)”

Akasema; Ni nani Muongozaji na kiongozi wenu? (mawlakum wa waliyyukum)”

Wakasema, na hakukuwa na wasiwasi juu ya hilo

Mola wako ndio Muongozaji wetu na wewe ndiye kiongozi wetu

Na hutopati  baina yetu kwenye hilo upinzani wowote

Akamwambi; Simama Ewe Ali kwa hakika nina furaha kutangaza wewe ni Imam na Kiongozi baada yangu (min ba’di imam(an) wa hadiy(an)),

Kwa hiyo yule ambaye nilikuwa mimi ni kiongozi wake, Basi huyu ndiye kiongozi wake

Basi shirikianeni nae katika Ukweli na Muwe wafuasi wake”

Kisha akamuombea dua: Mwenyezi Mungu kuwa rafiki na Muongozaji kwa wafuasi wake na kuwa Adui kwa wanaomfanya Adui Ali

Kiapo cha Utii21430462_1275216705921655_2151488920147441183_n

Baada ya hotuba yake, Mtume wa Allah (saww) aliwataka kila mtu kutoa kiapo cha utii kwa Ali na kumpongeza. Miongoni mwa wale waliofanya hivyo alikuwa Umar b. al-Khattab, ambaye alisema:

“Nimefanya hongera sana Ibn Abi Talib! Leo umekuwwa Kiongozi (mawla) wa wanaume na wanawake wote wanaoamini.”

Idadi ya maswahaba waliokuwepo Ghadir Khum

Mwenyezi Mungu aliamuru Mtume wake kuwajulisha watu wa tukio hili wakati wa watu wakiwa wengi wamezidi laki moja ili wote waweze kuwa wasimuliaji wa hadithi hii imesimuliwa na Zayd b. Arqam: Abu al-Tufayl alisema: “Nililisikia (tukio hilo) kutoka kwa Mtume Mwenyezi Mungu mwenyewe, na sio kwa mtu mwingine isipokuwa kwamba alimwona kwa macho yake na kumsikia kwa masikio yake.”

Kushuka kwa Aya ya Qur’ani 70: 1-3 Wafasiri wa kisunni zaidi wanasema kwamba mistari mitatu ya kwanza ya sura ya al-Ma’arij (70: 1-3) iliteremshwa wakati mgogoro ulipotokea baada ya Mtume (saww) kufika Madina. Imesimuliwa  kwamba:

Siku ya Ghadir Mtume wa Mwenyezi Mungu aliwaita watu kumuelekea Ali na kusema: “Ali ni mawla wa yule ambaye mimi ni mawla.” Habari zilienea haraka katika maeneo yote ya mijini na vijijini. Pindi Harith Ibn Nu’man al-Fahri (au Nadhr Ibn Harith kulingana na hadithi nyingine) alipokuja kulijua jambo hilo, alipanda ngamia wake na akaja Madina na akaenda kwa Mtume wa Allah akamwambia: “Wewe alituamuru sisi kushuhudia kwamba hakuna mungu ila Mwenyezi Mungu na kwamba wewe ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu tulikuitii, umetuamuru kusimamisha sala tano kwa siku na tuliitii, umetuamuru kufunga wakati wa mwezi wa Ramadhan na tuliitii, kisha ukatuamrisha kwenda Kuhiji Makka na tuliitii, lakini hujaridhika na haya yote na umeunyanyua mkono wa binamu yako na kumfanya awe bwana wetu kwa kusema “Ali ni mawla kwa ambaye Mimi ni mawla wake. Je, hii ni amri kutoka kwa Mwenyezi Mungu au kutoka kwako?

Mtukufu Mtume (saww) akasema: “Kwa jina la Mwenyezi Mungu ambaye ndiye Mola peke yake! Hili linatoka kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu na Mwenye utukufu.”

Aliposikia hayo Harith akageuka nyuma na akamuelekea ngamia wake akisema: “Ee Mwenyezi Mungu! Ikiwa kile hiki ambacho Muhammad anasema ni sahihi basi tupige kwa jiwe kutoka angani na na utusababishie maumivu makubwa na mateso.” Hakumfikia ngamia wake isipokuwa Mwenyezi Mungu, aliye juu ya kasoro zote, ataremsha jiwe ambalo lilimpiga kichwani mwake, na kupenya ndani ya mwili wake na kutokeza sehemu yake ya nyuma na kumuacha akiwa amekufa. Ilikuwa katika tukio hili ambalo Mwenyezi Mungu mtukufu alishusha aya zifuatazo: “Muulizaji aliuliza juu ya adhabu itakayo tokea, Kwa makafiri – ambayo hapana awezaye kuizuia, Kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mwenye mbingu za daraja”(70: 1-3)

Elijah J. Magnier

Middle East Politics

elbinawi

To interact with humanity & share ideas...

felicity114

felicity is the purpose of everybody

Ladakh Express

Ladakh's 1st political and cultural online journal.

Islamic Library

Shia Islamic PDFs - Now in Collaboration with ShiaTranslate.org!

zahraa Foundation

Fatima bint Muhammad is the Symbolization of Women's Power in Islam

mmubaraka1

A fine WordPress.com site

Pilgrim Center of Hope

Catholic Evangelization Ministry

World Shia Forum

Identity, Equality, Unity

Source of Inspiration

All is One, co-creating with the Creator

Bill Langill's Blog

Love is the Answer

Interrupting the Silence

An Episcopal Priest's Sermons, Prayers, and Reflections on Life, Becoming Human, and Discovering Our Divinity

Morgan L. Busse

In Darkness there is Light

YOGA

When unconscious became conscious this is Samadhi

Zoroastrians.net

Parsis, Iranis, Zarathushtis, All Under One Roof

Islamic Laws

Raising Awareness on Fiqh and the Ulema

Tech Cloud

Imagine | Innovate | Implement

Mujtaba Somji

Islamic sayings

%d bloggers like this: