Blog Archives

MAUAJI YA HUSSEIN,NANI WA KULAUMIWA? KWANINI YAKUMBUKWE?

Waislamu duniani wameendelea kuyakumbuka na kuyaenzi mapinduzi ya Imam Hussein kwa kuweka vikao mbalimbali katika misikiti na sehemu zingine, Maswali yamebaki kwa

sheikh ayub rashid

baadhi ya waislamu na hata wasiokuwa waislam wanajiuliza kwanini Hussein, na je nani wa Kulaumiwa ? na kwanini Mauaji hayo yakumbukwe?

Hujjatul Islamu, Sheikh Ayub Rashid anaandika haya yafutayo kujibu swali hilo hapo juu

Mauji ya Imam Hussein, nani wa kulaumiwa? Na kwa nini yakumbukwe?

Ilikuwa tarehe 7 Muharram 61 AH ipokuja amri ya kuzuia maji yasiwafikie watu ya kambi ya Imam Hussein na wenzake! Wao walikuwa katika ardhi ya Karbala.Walikaa hivyo bila ya maji kwa muda wa siku tatu!

Asubuhi ya tarehe 10 Muharram 61 AH ilikuja amri kupitia kwa mwanajeshi mwenye amri ya yote siku hiyo, huyo hakuwa mwingine bali Umar bin Saad, mtoto wa swahaba Saad bin Abi Waqqas. Huyu aliteuliwa na Ubeidullah bin Ziyaad, kuliwakilisha kundi la Yazid dhidi ya mjukuu wa Mtume (saw).Amri aliyopewa Umar bin Saad ni kumlazimisha Imam Hussein kutoa baia kwa Yazid, na kama akikataa basi auwawe! Yaani Imam Hussein mjukuu wa Mtume amuunge mkono Yazid kama kiongozi wake! Imam Hussein alikataa amri hiyo!

Wakati hayo yote yakiendelea, mwanajeshi mmoja aliyejuliakana kama Hur bin Yazid al Riyaahi alijikuta haamini aliyokuwa akiyasikia yakiamuliwa ya kumuua imam Hussein, mjukuu wa Mtume.Mazungumzo yakaanza ya pande mbili, kambi ya Umar bin Saad na ya Imam Hussein,hiyo ikiwa ni siku ya 10 Muharram, siku ijulikanayo kama Ashura, katika mwaka wa 61 wa Hijiriyyah.

Kambi ya Yazid ikiongozwa na Umar bin Saad ikimtaka Imam Hussein kutoa baia (Kiapo cha utii) kwa Yazid, na Imam Hussein alikataa ombi hilo kata kata! Kwa sababu kubwa kuwa Yazid hakuwa na sifa za kuwa kiongoz wa Waisilamu. Yazid alikuwa mtu fasiq (muovu)!

Ndipo ilipofika baada ya Adhuhuri ikaja amri ya kuanza vita! Mshale wa kwanza ukatupwa kutokea katika kambi ya Kina Yazid dhidi ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saww).

Mapigano

Kabla ya mapigano hayaja anza, yule mwanajeshi, Hur bin Yazid al Riyaahi, alipo ona kuwa wenzake wameazimia kumpiga vita Imam Hussein, na baada ya kuzungumza nao na kuona kuwa maamuzi yao ni ya kweli, aliamua kuikimbia kambi yake na kujiunga na kambi ya Imam Hussein. Rehema ya Allah iwe juu yake.

Mapigano yaka anza ya mtu mmoja mmoja, waka uana wengi wa pande mbili. Jeshi la Yazidi likiua kwa kuwa ni amri ya Yazid dhidi ya waliokosa kutoa baia, na la Imam Hussein likipigana na maadui wa mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) kwa kujihami. Lakini kwa kuwa jeshi la Yazid lilikuwa kubwa mno kulinganisha na jeshi la wafuasi wa Imam Hussein, jeshi la watu 72 Au watu 100 na kidogo. Takriban watu wote wanaume waliokuwa wakimuhami Imam Hussein waliuliwa.

Mwisho wa Imam Hussein

Baada ya kubakia pekee yake, Imam Hussein alipigana kiume kujilinda na kujihami na maadui hao, lakini alizidiwa nguvu na majangili hao wengi.

Mwisho aliangushwa chini kwa kupigwa na mti wa chuma, na pia baada ya kupigwa na jiwe kubwa. Akiwa hapo chini aliomba maji ya kunywa, lakini, mjukuu wa Mtume (saw) hakupewa na badala yake akawa akipigwa mateke na kutukanwa matusi makubwa makubwa.

Mwisho Umar bin Saad akatoa amri; “Mmalizeni”!

Ndipo alipokuja Shimri bin Dhil Jaushan, kama wana historia wengi walivyo eleza. Shimri akiwa ameshika kisu kikubwa! Akashika ndevu za Imam Hussein, akaweka kisu hicho kwenye shingo ya mjukuu wa Mtume! Aka anza kukikata…mpaka akakitenganisha na mwili wake!

Inna lillahi wa inna ilaihi rajiuun!

Kichwa cha Imam Hussein

Maharamia hao, laana ya Mola iwe juu yao! Wakakitundika kichwa cha mjukuu wa Mtume juu ya mkuki! Wakakata na vichwa vya wafuasi wengine wa Imam Hussein, wakavitundika kwenye mikuki! Wakachoma moto kambi ya Imam Hussein, wakawateka wanawake waliokuwemo humo! Akiwemo mjukuu wa Mtume, bibi Zainab binti Ali bin Abi Twalib, Wakawapeleka kwa liwali au gavana Ubeidullah bin Ziyaad, katika mji wa Kufa.

Ubeidullah bin Ziyaad

Gavana huyu wa Yazid aliyekuwa katika mji wa Kufa, katika nchi ya Iraq, alifurahi sana kukiona kichwa cha mjukuu wa Mtume kimekatwa na vichwa vingine vimepangwa pembeni na wanawake wametekwa nyara. Akatoa maneno mengi ya kashfa na matusi!

Mwisho, akaamua kichwa cha Imam Hussein na vingine vilivyokuwa hapo, pamoja na wanawake hao na mwanamume mmoja tu aliyesalimika kuuliwa siku hiyo, wapelekwe Shaam kwa Yazid bin Muawiya. Huyo aliyesalimika alikuwa ni Ali bin Hussein maarufu kama Imam Sajjad.

Safari ya Shaam ika anza kuelekea kwa Yazid, na hii ilikuwa ni safari ya shida na madhila makubwa kwa walioitwa mateka!

Shaam

Msafara huo wa mateka ulipofika Shaam, watu waliamuriwa wajipange kusherehekea kushindwa kwa wapinzani wa Yazid, amir wa waisilamu, kama alivyo itwa!

Pindi Yazidi alipopelekewa kichwa cha Imam Hussein, alichukua fimbo, akapiga piga mdomo wake, huku akisema “hiki ndicho kimdomo alichokuwa akikibusu Muhammad’!

Akasema maneno ya kufru, kuwa yote hayo ni kisasi cha kulipiza mauaji ya mababu zake waliouliwa katika vita vya Badr! Laiti wangelikuwa hai wangelishuhudia mapigo yake!

Inna Lillahi wa inna ilaihi rajiuun!

Kwa nini kumlilia Hussein na sio Hassan?

Baadhi ya watu wameuliza kwa nini kumlilia Hussein na sio kumlilia ndugu yake Hassan au mashahidi wengine waliouliwa kabla yake?

Majibu

Kila mtu mwenye hisia za kibinadamu humlilia Hussein kwa namna alivyouliwa kinyama yeye pamoja na waliokuwa nao. Na kumlilia Hussein alianza babu yake, Mtume Muhammad (saw) kama ilivyokuja katika Hadith ya bibi Ummu Salama, mke wa Mtume (saw).

Na wafuasi wa Ahlulbayt huwalilia wote katika maimamu wao waliouliwa kishahidi na kwa dhulma. Huanza kwa kumlilia Mtume, kisha Ali bin Abi Twalib, kisha Hassan bin Ali na kisha Hussein na wale waliomfuatia miongoni mwa viongozi waliokuja baada yake.

Na hayo unaweza kuyashuhudia katika misikiti ya Mashia na katika kalenda zao ambazo huandika siku za maadhimisho ya kuzaliwa kwa maimamu wao na kuomboleza vifo vyao. Kwa hivyo si kweli kuwa wao humlilia Hussein peke yake!

Kwa nini ikawa msiba wa Imam Hussein umapewa siku nyingi zaidi?

Majibu

Ni kwa sababu ya kuelezea jinsi ya dhulma aliyofanyiwa mjukuu wa Mtume na wale waliodai kuwa wao ni watawala waadilifu wa Kiislamu. Na jinsi watawala hao walivyowalaghai watu na kuwadanganya kwa hila mbali mbali.

Na kuomboleza huku ni kueleza namna Umma ulivyokuwa umelala wakati huo mpaka ukaruhusu mjukuu wa Mtume auwawe kinyama, na kichwa chake kitundikwe katika mkuki na kipitishwe mitaani na watu kushangilia.

Na pia kuelezea namna Yazid, aliyekuwa ‘Amir al Muminin’, alivyokifanyia istihzai kichwa hicho kitukufu! Hayo yote hayatoshi kuomboleza kwa siku moja tu!

Sasa hivi msiba huu unaombolezwa kwa siku unazo ombolezwa ili kuwazindua watu kutoka katika ghafla waliyokuwemo ndani yake! Kwani kuna waisilamu wengi leo hata hawamjui Hussein alikuwa nani? Na Yazid alikuwa nani? Wala hawamjui muovu Ubeidullah bin Ziyad aliyetumwa na Yazid kusimamia mauaji ya mjukuu wa Mtume alikuwa ni mtu wa aina gani na aliamrisha maovu makubwa kiasi gani?

Historia ya kuuliwa Hussein mjukuu wa Mtume ni historia muhimu sana kujulikana leo, ili watu wasije kudanganyika na kuwafuata viongozi kama kina Yazid ambao hawakuwa na sifa ya kuongoza Umma wa Mtume Muhammad, swallallahu alaihi wa aalihi wa sallam.

Naamini hata haya tunayoyaelezea hapa wako watu wengi hawayajui!

Ya Allah tuonyeshe haki kuwa ni haki na uturuzuku kuifuata, na utonyeshe batwil kuwa ni batwil na utuwezeshe kuiepuka.

Imeandikwa na Hujjatul Islam,

Sheikh Ayub Rashid

 

 

SHAHADA YA IMAM MOHAMMAD TAQI AL-JAWAD (AS)

kazmain

Waislamu duniani kote na wapenzi wa Nyumba tukufu ya Mtume (saw) siku ya leo wanaingia katika maombolezo ya kifo cha Mjukuu wa Mtume na Imamu wa Tisa (9) aliyefariki Shahidi Tarehe 29th Dhulqa’ada  akiwa na umri wa miaka 25 kwa kuwekewa sumu na khalifa (Mfalme) wa zama zake.

JINA: Muhammad bin Ali (a.s.)

MAMA: Sakina

KUNIYA (PATRONYMIC): Abu ‘Abdillah

WASIFU (TITLE): Al Jawad

KUZALIWA: Alizaliwa Madina 195 A.H.

SHAHADA: Alifariki kwa kuwekewa Sumu huko Baghdad mwaka 20 A.H. na kuzikwa karibu na babu yake hapo Kazimiyyah in Iraq.
Mtume Muhammad (saww) anasema:

“Baba yangu awe ni kafara kwa Mama yake Imamu wa 9,mwanamke ambaye ni Twahara na Mnubi mweusi.”
Historia yake

Imam Musa Alkadhim (s.a) alimwambia mmoja wa wafuasi wake kuwa mkwewe (Sabika) atakuwa mmoja ya wanawake wachamungu na wamfikishie salamu zake. Anatokana na kabila moja sawa na kabila la mke wa Mtume, Sayyida Mariam Kibtiya ambaye alimzalia mtume mtoto wa kiume Ibrahim (Aliyefariki akiwa mdogo)
Imam Muhammad Taqi (s.a) alizaliwa wakati baba yake akiwa na Umri wa Miaka 45. Mpaka wakati huo imam alikuwa akishutumiwa kuwa hana mtoto. Wakati Imam wa Tisa (9) alipozaliwa, aliyekua kaka yake Imam Ridha (a.s) alikasirika  kwa kuwa alijua atakosa kurithi Mali za Imam na kwa wivu wake akaanza kusambaza uzushi kuwa Imam Ridha (a.s) sio baba wa Mtoto. Lakini hatimaye alishushuliwa na wataalamu wa Uzazi na ukoo.

UTOTO WAKE

Imam wa Jawaad (imam wa Tisa (9)) akiwa na Miaka mitano (5) baba yake alipata wito wa kwenda Tusi akiitwa na mtawala wa wakati huo Maamun Rashid ili akawe “Mteule Mkuu”. Wakati Imam Ridha (a.s) akiondoka alimuona mwanawe mdogo akiweka mchanga katika nywele zake. Akamuuliza kwanini anafanya hivyo na Imam mtoto akamjibu kuwa hivi ndivyo afanyavyo Yatima.

WADHIFA WAKE, MAISHA NA KAZI ZAKE:

Alikuja kuwa Imam akiwa na umri wa Miaka Tisa (9). Mtawala Maamun kwa kujua kuwa Watawala wengine waliomtangulia waliwanyanysa Maimamu na hivyo mipango yao kuharibika na wao kuangamia, Maamuni akaona ni fursa yake kumlaghai na kumhonga Imam. Akajaribu kumfanya Imamu wa Nane (8) kuwa Mteule wake mkuu pamoja na kumrundikia Vyeo, na utajiri lakini hata hivyo hakufanikiwa.

Kwa zama za Imam wa Tisa (9) akaamua kutumia mamlaka yake na utajiri wake, wakati Imam angali kijana mdogo kabisa akidhani angefanikiwa kumshawishi. Lengo lake kuu ilikuwa ni kuhakikisha anamuozesha binti yake Ummul Fazl kwa Imamu wa Tisa kwani alijua kuwa Imamu wa Kumi na Mbili (12) (Ambaye alikuwa akijua atakapokuja ataleta Amani duniani) atatokana na kizazi cha Imamu wa Tisa, wakati wote huo maamun alikuwa angali akiendelea kuwanyanyasa na kuwakandamiza familia na wafuasi wa Ahlulbayt.

Maamun akaamua kumuita Imam huyu kijana kwenda Baghdad akitokea Madina na akampa binti yake. Kitendo hiki kiliwaudhi ukoo wake wa Abbasiya. Ili kuwathibitishia utukufu wa Imam hata alipokuwa na umri mdogo akaandaa mkutano kati ya imam na Mwanazuoni mkubwa kabisa wa zama hizo Yahya bin Athkam. Ulikuwa ni mkutano mkubwa sana ulihudhuriwa na wanazuoni wengine takriban 900.  Mwanazuoni Yahya alianza kwa kumuuliza Imam maswali:

Ni ipi fidia (Kafara) kwa mtu aliye katika Ihram ambaye aliwinda na Kuua windo lake?

Imam akamjibu kuwa swali hilo lina maelezo mengine mengi yanayohitajika kabla ya kulijibu:

 • Je huyo mwenye Ihram, aliwinda ndani ya eneo la Haram au nje yake?
 • Je huyo mwenye Ihram, alikuwa anajua Sharia ya dini au hajui?
 • Je huyo mwenye Ihram, aliwinda kwa Makusudi au Bahati mbaya?
 • Je huyo mwenye Ihram, windo hilo lilikuwa la kwanza au lilikuwa miongoni mwa malindo mengi aliyofanya?
 • Je huyo mwenye Ihram, alikuwa Mtumwa au Mtu huru?
 • Je huyo mwenye Ihram, aliwinda Mnyama au Ndege?
 • Je huyo mwenye Ihram, windo lake lilikuwa la Kiumbe mkuwa au Mtoto
 • Je huyo mwenye Ihram, alifanya windo hilo Mchana au Usiku?
 • Je huyo mwenye Ihram, aliwinda alikuwa ameshabalegh au bado?
 • Je huyo mwenye Ihram, baada ya windo hilo alitubu au hakutubu?
 • Je huyo mwenye Ihram, Ihram hiyo ilikuwa ya Hijja au Umra?

Yahya alistaajabu sana. Aliinamisha uso wake chini akiinama na kuanza kutokwa na jasho.

Maamun akamtaka Imamu kulijibu swali hilo na vipengele vyake, Imam akajibu ipasavyo,  kisha akamtaka Imamu na yeye amuulize Yahya Swali, Imam akafanya hivyo lakini Yahya hakuweza kujibu.

Hapo ndipo Ukoo wa Abbasiya wakakubali kushindwa na Maamuni akachukua fursa hiyo kumtoa Binti yake na kumpa Imam. Imam (AS) akaisoma mwenyewe Ndoa yake kwa Khutuba ambayo leo ndio Maarufu inayotumika, kwa Mahari ya Dirham 500. Imam akaaandika barua kwa Maamun kuwa kama nyongeza pia Imam atampa Ummul Fazl Mahari ya Utajiri wa dunia nyingine (Akhera). Haya yalikuwa ni kwa mtindo wa Dua  kumi (10)* za kutekeleza haja yoyote na hiyo ndio sababu ya Jina lake Al-Jawad (aliye mkarimu).

*Dua hii inapatikana katika kitabu cha dua cha Mafatihul Jinaan (Uk. 447)

Imam aliishi kwa Mwaka mmoja hapo Baghdad pamoja na Ummul Fazl, alikuwa Mwanamke Mtukufu sana kwa Imamu. Alipokuja kugundua kuwa Imam alikuwa ana mke mwingine (Kutoka uzao wa Ammar bin Yasir) na pia tayari walikuwa na watoto, alipatwa na Wivu mkubwa na hasira akijua kuwa mtego wa baba yake umevurugika.

Akaenda kumshitakia kwa baba yake, ambaye na yeye alitambua kuwa mpango wake wa kumuingiza Imamu katika ukoo wake umeshavurugika, alighadhabika sana na kwa hasira alianza kunywa pombe kwa wingi sana na kisha akaenda nyumbani kwa Imam wa (9) na kumshambulia Imam kwa upanga. Ummul Fazl na watumishi wote walishuhudia shambulio hilo na kutokana na ukubwa wake walijua kuwa Imam amekufa.

Maamun alipoamka alifajiri ya siku iliyofuata akijua athari ya shambulizi lake akaanza kufikiria namna ya kuuzika mwili wa Imam, ghafla akamuona Imam akiwa salama kabisa na mwenye Siha nzuri pasina mkwaruzo hata chembe. Alichanganyikiwa na akamuuliza Imam kulikoni? Imamu akamuonyesha Hirzi (Ngao) iliyokuwa na jina “Hirzi Jawad” Imamu akamwambia Maamun Hirzi hiyo amepewa kutoka kwa Bibi yake Bi Fatma Zahraa (AS), Hirzi hiyo humkinga anayeivaa na kila kitu kasoro Malaika wa mauti Maamuni akamuomba imam ampe naye akampa.

Maamuni akaingiwa na woga na akaanza kujaribu mbinu nyingine. Akawa anajaribu kumrubuni Imam kwa kumpelekea Wanawake warembo na Wanamuziki. Alipoona hakuna anachofanikiwa akamruhusu Imam arejee nyumbani kwao Madina.

Imamu akaamua kutumia muda wake kuandaa kitabu cha Fiqhi na mapokeo (Taqleed na Ijtihaad) akimuandalia Imamu wa Kumi na Mbili (12) kwa kuwa alikuwa akijua kuwa Imam wa 10 na 11 watatumia muda wao wote wa maisha ndani ya Magereza ya watawala wa zama zao. Pia alikuwa akiwaandaa watu wa Madina kwa kuwafundisha Uislamu wa Asili na wa kweli, pia akijua huo ndio utakuwa wakati wao wa mwisho na itawachukua Miaka mingi ijayo wakaazi wa Madina kupokea mafundisho na muongozo moja kwa moja kutoka kwa Imamu.

Maamuni alifariki mwaka 218 A.H.  na alirithiwa ufalme wake na kaka yake Muutasim Billah. Huyu yeye alitangaza wazi wazi na hadharani kuwa mashia wote sio waislamu na akasema inapaswa watu wawaue  na kuwachinja na kuharibu mali zote zinazomilikiwa na Mashia.

Ummul Fazl wakati huo akahamishia Malalamiko yake kwa Mjomba wake ambaye alikuwa akimuonea huruma sana. Ndipo Muutasim akamuru Imamu aende Baghdad. Huko akamtaka Imam atoe Fatwa juu ya adhabu ya Mtu aliyeiba. Imam akasema kuwa Vidole tu ndio vikatwe kwani kiganja ni cha Mwenyezi mungu Imam (a.s) akasema Katika  Qur’an – Kiganja ndicho kiungo cha wajibu kugusa Ardhi wakati wa Sujudi) Fatwa hii ya Imamu ilikuwa ni tofauti kabisa na za wanazuoni wengine na iliimarisha sana nafasi ya Mashia.  Na ilipelekea wanazuoni wengine pia kumlalamika kwa Muutasim.

WAKE ZAKE NA WATOTO WAKE

Mke wa Imam al-Jawad alikuwa Umm al-Fadhl, binti wa mfalme Maamun. Hakuzaa nae hata mtoto mmoja. Imam Muhammad al-Taqi (as) alikuwa na mke mwingine akiitwa Samana Maghribiyya. Imeelezwa Imamu alikuwa na watoto wa kiume wanne na wa kike wanne:

 1. Abu al-Hasan Imam ‘Ali al-Naqi (Hadi) (as)
 2. Abu Ahmad Musa Mubarqa‘
 3. Abu Ahmad Husayn
 4. Abu Musa ‘Imran
 5. Fatimah
 6. Khadija
 7. Umm Kulthum
 8. Hakima

KIFO NA MAZIKO YAKE

Kutokana na fitina iliyokuwa ikifanywa na wanazuoni na Ummul Fazl kwa pamoja , Muutassim akaagiza Sumu ambayo Ummul Fazl alimtegea Imamu katika kinywaji na kumpa akanywa. Imamu akafariki Shahidi Tarehe 29th Dhulqa’ada  akiwa na Umri wa Miaka 25 na kuzikwa karibu kabisa na Kaburi la Babu yake huko Kadhimain. Mwanawe Imam wa kumi (10), Imam Hadi (AS) ndiye aliyemzika.

MUHTASARI WA KAZI ZAKE

Ni  yeye aaliyendaa na kuandika vitabu vya Rejea vya Fiqh (Masail) vya Ijtihad na Taqlidi ambavyo vilikuwa vitabu muhimu kwa ajili ya kuwaanda waumini kwa tukio la Ghaiba (Kificho) cha Imamu wa Kumi na Mbili (12).

 

elbinawi

To interact with humanity & share ideas...

felicity114

felicity is the purpose of everybody

Ladakh Express

Ladakh's 1st political and cultural online journal.

Islamic Library

Shia Islamic PDFs - Now in Collaboration with ShiaTranslate.org!

zahraa Foundation

Fatima bint Muhammad is the Symbolization of Women's Power in Islam

mmubaraka1

A fine WordPress.com site

The Pilgrim Log

Helping you live your daily pilgrimage

World Shia Forum

Identity, Equality, Unity

Source of Inspiration

All is One, co-creating with the Creator

Bill Langill's Blog

Love is the Answer

Interrupting the Silence

An Episcopal Priest's Sermons, Prayers, and Reflections on Life, Becoming Human, and Discovering Our Divinity

Morgan L. Busse

In Darkness there is Light

YOGA

When unconscious became conscious this is Samadhi

Zoroastrians.net

Parsis, Iranis, Zarathushtis, All Under One Roof

Islamic Laws

Raising Awareness on Fiqh and the Ulema

Tech Cloud

Imagine | Innovate | Implement

Mujtaba Somji

Islamic sayings

%d bloggers like this: